Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bima ya afya kupunguza makali kwa mabondia

Muktasari:

  • BMT kwa kushirikiana na TPBRC ina mpango wa kuhakikisha inaweka ulazima wa kila bondia kuwa na bima ya afya itakayowawezesha kuwa na uhuru wa kupima afya zao.

KABLA ya kuweka sheria kuwabana mabondia kupima vipimo vya MRI/CT Scan, inapendekezwa kushughulikiwa kwanza suala la kila bondia wa ngumi za kulipwa kuwa na bima ya afya.

Kwa mujibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), linaandaa mchakato wa kushirikiana na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), ili kuwe na sheria ya lazima kwa kila bondia kuwa na bima ya afya itakayomsaidia kuwa huru kupima vipimo hivyo, ambavyo kwa mujibu wa mabondia ni vya gharama kubwa.

Katika uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, wadau wa ngumi wanaeleza kuwa gharama kubwa za vipimo vya MRI na CT Scan inayofikia hadi Sh1.5 milioni zinawafanya mabondia wengi kushindwa kuvifanya, jambo linaloweka maisha yao hatarini.

Wanasema baadhi ya mabondia huingia ulingoni wakiwa na majeraha yaliyofichika na baadaye hupata ulemavu au kupoteza maisha baada ya kupigwa, hivyo wameiomba Serikali, wadhamini na mamlaka za ngumi kupunguza gharama za vipimo.

Vilevile, wanaomba kuboreshwa upatikanaji wa bima na kuimarisha usimamizi wa uchunguzi wa afya ili kulinda maisha ya mabondia.

Daktari wa ngumi nchini, Khadija Khamis anasema vipimo vya MRI au CT Scan kwa hospitali za serikali ni takribani Sh800,000 na za binafsi ni Sh.1.5 milioni, gharama ambayo ni kubwa hivyo kuwa ngumu kwa mabondia kuzimudu.

Anamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kuwapa bima za afya mabondia zitakazowasaidia kupunguza gharama hata kama haitatibu kila kitu.


Ilichosema BMT

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha anasema afya kwa wanamichezo ndiyo msingi na mtaji mkubwa, kwani haiwezekani kucheza wakiwa na migogoro ya kiafya.

"Tunataka kushirikiana na TPBRC ili kuhakikisha tunaweka ulazima wa kila bondia kuwa na bima ya afya itakayowawezesha kuwa na uhuru wa kupima afya zao. Hilo linawezekana kwa pesa wanazolipwa katika mapambano wanayoyafanya," anasema na kuongeza:

"Ikifanikiwa kila bondia akawa na bima, basi tutaanza mjadala wa kuweka sheria ya ulazima wa kupima vipimo kama MRI/CT Scan. Kwa sasa itakuwa ngumu wao kulipa cash (fedha taslimu) vipimo hivyo ni gharama, lakini la msisitizo zaidi ni hizo bima kama Serikali inavyosema," anasema.

Kanuni za Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) za mwaka 2024, zinasisitiza umuhimu wa kila bondia kupima kabla na baada ya pambano, lakini hakuna ulazima wa kipimo cha MRI/CT Scan.

Kanuni 4.1.2 inasema siku 14 kabla ya kushiriki pambano lolote la ngumi za kulipwa bondia atawajibika kupimwa afya yake na daktari mwenye leseni ya kamisheni na anayetambulika na Chama cha Madaktari wa tiba za michezo (TASMA).

Kutokana na majibu ya vipimo daktari atashauri iwapo bondia husika anaweza au hawezi kushiriki pambano.

Kanuni za kimataifa za ngumi zinahitaji mabondia kufanyiwa uchunguzi wa afya, huku MRI au CT Scan ya ubongo ikihitajika katika mazingira maalumu au kwa vipindi vinavyowekwa na shirikisho au mamlaka husika; si lazima kabla ya kila pambano.

Mfano, Shirikisho la Kimataifa la Ngumi (IBA), lililokuwa likijulikana awali kama AIBA katika kanuni zake zilizoboreshwa MRI/CT Scan inapendekezwa kabla ya kushiriki mashindano makubwa kama mashindano ya dunia. Pia bondia akipigwa KO au TKO vipimo hivyo vitahitajika.

Makamu Mwenyekiti wa TPBRC, Jacob Mbuya, anasema wameingia udhamini na Hospitali ya Hitech Sai iliyopo Upanga mkoani Dar es Salaam na kwamba, mabondia wanne wameshapatiwa huduma ya vipimo hivyo baada ya ushauri wa daktari.


Umuhimu wa vipimo

Vipimo vya afya, vikiwamo MRI na CT Scan vina umuhimu mkubwa kwa mabondia kwa sababu ngumi ni miongoni mwa michezo yenye hatari kubwa ya majeraha ya kichwa na ubongo.

Kupitia vipimo hivyo wanaweza kugundua majeraha ya ubongo, uvujaji damu, uvimbe au nyufa za fuvu ambazo haziwezi kuonekana kwa uchunguzi wa kawaida.

Mbali ya hayo, bondia mwenye jeraha la zamani anaweza kuonekana mzima, lakini akipokea pigo jingine linaweza kuzidi na kusababisha ulemavu wa kudumu au kifo.

Ni kupitia vipimo daktari anaweza kuamua kama bondia yuko salama kupanda ulingoni ama anahitaji matibabu au mapumziko zaidi. Pia badala ya kutibu dalili kwa dawa za maumivu pekee, vipimo vinaonyesha chanzo halisi cha tatizo ili matibabu yafanyike kwa usahihi.

Daktari Gilbert Kigadye wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), ambaye pia hutoa tiba kwa watu wengine wakiwamo mabondia anasema michezo inayohushisha vishindo lazima wahusika wapimwe kabla ya msimu wa kazi kuanza ili kuhakikisha afya zao zipo sawa.

"Wanamichezo wa aina hiyo lazima wapimwe mwili mzima kuhakikisha wanakuwa salama na kuwaepusha na maambukizi na vifo. Ninachoshauri kwa mabondia, waweke mfumo wa kupimwa na madaktari zaidi ya mmoja, hilo litaondoa udanganyifu maana hawawezi kudanganya wala kutoa pesa kwa kila daktari," anasema.

Dk Shita Samwel, ambaye ni mtaalamu wa afya na mazoezi anasema vipimo hivyo vinatazama hali ya ubongo endapo kuna uvimbe au kuna shida ya mishipa ya damu, akisisitiza kwa ujumla vinabaini kama kuna tatizo linaloweza kuwa tishio.

"Ngumi zinahusisha majeraha ya kichwa pamoja ubongo wenyewe, hivyo nashauri wapewe elimu ya afya ili kuwapa ufahamu kuhusu matatizo yanayojitokeza upande wa majeraha ya ubongo. Pia wawe na madaktari binafsi wa kuwasimamia afya zao," anasema Dk Shita na kuongeza:

"Muhimu wajue kuwa kabla ya kushiriki pambano kufanya uchunguzi wa kiafya ni lazima. Kuzingatia mwongozo wa upimaji afya ule wa shirikisho la ndondi duniani, ikiwamo kabla ya pambano kuchunguza afya na kufanya pambano mara moja kwa miezi sita.”