Battle sita za kibabe Simba, Yanga

Muktasari:

MIONGONI mwa mambo yanayonogesha na kuipa mvuto mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga ni ushindani wa wachezaji wa upande mmoja na mwingine kutokana na ubora na sifa walizonazo ndani ya uwanja.

MIONGONI mwa mambo yanayonogesha na kuipa mvuto mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga ni ushindani wa wachezaji wa upande mmoja na mwingine kutokana na ubora na sifa walizonazo ndani ya uwanja.

Katika mechi za namna hii wale wa safu ya ulinzi hutafuta mbinu bora za kuhakikisha zinawadhibiti washambuliaji wasifunge mabao wakati huo washambuliaji wenyewe wakitafuta namna bora ya kuhakikisha wanapenya mabeki na makipa ili kuzifungia timu zao mabao.

Wakati huo wale wa safu ya kiungo hujitahidi kupambana ili waongoze umiliki wa mpira, waweze kujiweka katika nafasi nzuri ya kudhibiti upande wa pili na kutengeneza mazingira mazuri ya ushindi kwa timu zao.

Kuelekea mechi ya Simba na Yanga itakayochezwa kesho Jumamosi, Mwanaspoti linakuletea vita sita kali ambazo zinaweza kufanya mechi baina ya timu hizo mbili kubwa nchini kuwa na mvuto wa kipekee.


TSHABALALA vs KISINDA

Winga wa Yanga, Tuisila Kisinda amekuwa akionekana kama mchezaji mwenye kasi kubwa zaidi kuliko wengine katika Ligi Kuu Bara msimu huu na kasi yake mara kwa mara imekuwa ikiisadia Yanga katika kutengeneza mabao na kusaka faulo au kona ambazo huwa chanzo cha mabao cha timu hiyo.

Upande wa pili, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amekuwa akitajwa kama mlinzi bora wa kushoto hapa nchini kutokana na uwezo wake mkubwa katika kujilinda na kuzuia.

Wawili hawa bila shaka kila mmoja atataka kumuonyesha mwenzake nani zaidi katika mchezo huo.


NINJA vs MUGALU

Chris Mugalu amekuwa mshambuliaji chaguo la kwanza la Simba katika mechi ngumu za ndani na zile za Ligi ya Mabingwa Afrika na kiujumla amefunga mabao tisa.

Kesho bila shaka atakuwa katika vita nzito na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye sifa yake kubwa imekuwa ni kuwafanya washambuliaji hatari wasifurukute pindi anapokutana nao kama alivyofanya dhidi ya Meddie Kagere kwenye Kombe la Mapinduzi.


SAIDO vs TADDEO

Kiungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza ni fundi wa kufunga mabao na kupiga pasi za mwisho ambapo amefunga mabao matatu kwenye ligi na kupiga pasi tano zilizozaa mabao lakini wengi wanatamani kuona kama ataweza kufurukuta mbele ya kiungo mkabaji Lwanga Taddeo ambaye ameonyesha ubora na kiwango cha juu katika kutibua mashambulizi na mipango ya viungo na washambuliaji wa timu pinzani.


KAPOMBE vs YACOUBA

Kinara wa upachikaji mabao katika kikosi cha Yanga kwenye Ligi Kuu hadi sasa ni Songne Yacouba ambaye hadi sasa ameifungia timu hiyo mabao sita na kiuhalisia ndiye mchezaji aliye kwenye ubora wa hali ya juu kwa sasa.

Yacouba amekuwa akishambulia kutokea upande wa kushoto ambao katika mechi hiyo utamfanya acheze dhidi ya beki wa kulia wa Simba, Shomary Kapombe.

Kapombe amekuwa akitegemewa zaidi Simba katika kupandisha mashambulizi hivyo kiu ya wengi ni kuona kama Yacouba ataweza kumfanya Kapombe asipande mbele au yeye ndio atageuka beki?


ADEYOUM vs LUIS

Mchezo wa mwisho wa watani wa jadi ambao beki wa kushoto wa Yanga, Adeyoum Saleh alicheza ulikuwa ni ule wa Januari 4, 2020 ambao timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.

Adeyoum alionekana kupata wakati mgumu mbele ya winga Deo Kanda ambaye alifunga bao moja ingawa beki huyo wa kushoto ndiye alipiga krosi iliyozaa bao la kusawazisha la Yanga.

Beki huyo atakuwa kibaruani dhidi ya winga msumbufu, Luis Miquissone ambaye mbali ya kufunga mabao, ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho, kupiga chenga na kumiliki mpira.


MUKOKO vs CHAMA

Clatous Chama ndiye moyo wa Simba kwa sasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzalisha mabao iwe kwa kufunga au kupiga pasi ya mwisho ambapo hadi sasa amehusika na mabao 21 kwenye ligi, akifunga saba na kupika 14.

Katika mchezo uliopita wa ligi hiyo baina ya timu hizo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, Chama alishindwa kufurukuta mbele ya kiungo Mukoko Tonombe ambaye amekuwa uti wa mgongo wa Yanga katika mechi zake.