Bao 14 Simba Queens zakoleza ushindani

JUZI Simba Queens ilitoa kipigo kikali cha mabao 14-0 dhidi ya Kinondoni Queens katika mechi yao ya kirafiki lakini jambo kubwa ambalo kocha msaidizi wa timu hiyo ya Msimbazi, Mussa Hassan 'Mgosi' ameliona ni ushindani wa namba kikosini.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena kuanzia saa 10 jioni, mabao manane yalifungwa na wachezaji wanne waliofunga mawili-mawili kila mmoja ambao Jentrix Shikangwa, Danai Bhobho, Zainabu Mohamed na Shelda Boniface na mengine sita yalifungwa na wachezaji sita tofauti - Olaiya Baraka, Aisha Mnunka, Silvia Mwacha, Diakiese Isabella, Asha Djafari na Asha Rashid.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Mgosi alisema lengo la mechi hiyo lilikuwa ni kujiweka sawa na mzunguko wa pili lakini amegundua kuna ushindani mkubwa na mzuri kwa nyota wake baada ya wachezaji 10 tofauti kila mmoja kufunga angalau bao moja katika mechi hiyo.

Alisema kila mchezaji alijitoa na kufanya vizuri kwenye mchezo huo ili kulishawishi benchi la ufundi limpe nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza. 

"Wachezaji wapo kwenye ushindani wa kupigania nafasi ya kuwa kwenye kikosi cha kwanza na ndio maana umeona mabao yamefungwa na pia safu ya ulinzi haijakubali kuruhusu bao. Kila mmoja anajitahidi kuonyesha ubora wake ili kutushawishi makocha kumpatia nafasi ya kuwa katika kikosi cha kwanza," alisema Mgosi na kuongeza;

"Lengo ni kujiweka vizuri zaidi na kuhakikisha mzunguko wa pili tunaendelea kufanya vizuri zaidi ukizingatia mpaka sasa tunaongoza ligi hivyo tunatakiwa kujiandaa zaidi kwenye uwanja wa mazoezi ili tuje tofauti kwa kufuta makosa yote yaliyojitokeza na kuboresha zaidi."