Bado wapo sana...
IMEELEZWA hakuna makocha ama viongozi wanaoweza kuvumilia kukaa na wachezaji kwa muda mrefu wasio na faida kwenye timu, vinginevyo kitakachowafanya wadumu ni uwezo wao.
Hilo linathibitishwa na baadhi ya mastaa ambao Mwanaspoti limebaini wamekaa kwa muda mrefu kwenye timu kwa sababu huduma zao ni muhimu na kuvibeba vikosi vyao katika michuano mbalimbali.
SURE BOY - YANGA
Salum Abukar ‘Sure Boy’ alijiunga na Yanga msimu wa 2021/2022 akitokea Azam FC ambako alikaa zaidi ya miaka 10 tangu alipopanda nayo 2008/09 na ndio ilianza kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.
Sure Boy alikuwa kati ya wachezaji walioisaidia Azam FC, kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 2014, Kombe la Kagame 2015, 2018 na Kombe la Mapinduzi 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.
Kiungo mshambuliaji huyo, alitua Yanga na mguu mzuri kwani aliisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na Ngao ya Jamii na wa ASFC.
AISHI MANULA - SIMBA
Huwezi kumweka kwenye kundi la chipukizi, kwani ana miaka 10 kucheza Ligi Kuu Bara, tangu alipopandishwa Azam B kwenda timu ya wakubwa mwaka 2012.
Azam FC amecheza misimu mitano kuanzia 2012-17 kisha akajiunga na Simba ambako nako mwaka huu anafikisha msimu wa tano baada ya kujiunga nao mwaka 2017.
JOHN BOCCO - SIMBA
Straika anayeongoza kwa rekodi ya mabao 145 kwa wachezaji wa sasa Ligi Kuu Bara, pamoja na umaarufu wake amecheza timu mbili tu Azam FC aliyopanda nayo 2008-17, kisha akahamia Simba 2017 hadi sasa.
Bocco ameacha rekodi za kusisimua na kukumbukwa Azam FC, aliisadia kunyakua taji la Ligi Kuu mwaka 2014, Kombe la Kagame 2015, 2018, Kombe la Mapinduzi 2012,2013, 2017 na aliacha akiwa ameifungia jumla ya mabao 88.
Mabao hayo aliyafunga msimu wa 2008/09 (1), 2009/10 (14), 2010/11 (15), 2011/12 (19),2012/13(7), 2013/14 (7), 2014/15 (3), 2015/16 (12) na 2016/17 (10), baada ya kuhamia Simba 2017/18 (14), 2018/19 (15), 2019/20 (9), 2020/21 (16), 2021/ 22 (3) na huu wa 2022/23 bado hajaanza kucheka na nyavu.
Hivyo Simba akiwa nahodha amechukua mataji manne ya Ligi Kuu, la Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), taji la Kombe la Mapinduzi na amefunga mabao 57 kwenye ligi.
JONAS MkUDE - SIMBA
Ana historia ya aina yake, tangu alipopandishwa kutoka Simba B mwaka 2012 hajawahi kuhama timu na ndiye mkongwe kwenye kikosi hicho, hilo linampa thamani kubwa mbele ya viongozi na mashabiki wake, pia ameisaidia timu hiyo kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu mara tano, 2012, 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21.
AGREY MORIS - AZAM
Aliichezea Mafunzo ya Zanzibar 2003-2009, kisha akajiunga na Azam 2009-2022. Ndiye mchezaji mkongwe ndani ya kikosi hicho na ni kati ya mabeki bora wa kati.
Ndani ya muda aliocheza Azam FC amenyakua mataji mawili ya Kagame mwaka 2015 na 2018, moja la Ligi Kuu 2014 na Kombe la Mapinduzi matano, 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.
SHABAN NDITI - MTIBWA SUGAR
Tangu alipojiunga na Mtibwa Sugar kwa mara ya kwanza 2022-2006 alihamia Simba mwaka 2006-2008, kisha akarejea tena Mtibwa Sugar mwaka 2008-2022 na kwa sasa mara nyingi anaonekana kwenye benchi la ufundi, aliisaidia timu hiyo kunyakua taji 1999/2000.
WACHEZAJI WA MIAKA 2000
SHADRACK NSAJIGWA - KOCHA
Beki wa zamani wa Tanzania Prisons (2004/05), Yanga (2006-2012) na Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa licha ya kucheza kwa mafanikio makubwa hakuwa mchezaji aliyekuwa anahamahama. Kwa muda alioichezea Yanga aliisaidia kunyakua mataji ya Ligi Kuu mwaka 2006, 2008/09, 2011/12 akiwa nahodha.
“Ukiona unadumu kwa timu kama Yanga ujue kiwango chako ni muhimu, pia inajenga uaminifu mbele ya mashabiki na kujitengenezea koneksheni na watu wengi,” anasema.
NADIR HAROUB - MENEJA
Beki wa zamani wa Yanga na Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye kwa sasa ni meneja wa Taifa Stars, hakuwa mchezaji wa kuhamahama timu.
Alijiunga na Wanajangwani (2000-2003), Malindi FC (2003-2005), Yanga (2006-2018).
Anazungumzia hilo, “Kukaa muda mrefu na timu unajenga urafiki na uaminifu mbele ya mashabiki na viongozi hata ukitundika daruga bado utakumbukwa pengine kupewa nafasi ya cheo chochote, ila hasara ni pale hupati nafasi ya kucheza hapo thamani yako inakuwa ndogo na ukiona hilo bora kuondoka ukapate changamoto sehemu nyingine.”
GEORGE KAVILA - KOCHA
Japokuwa amepitia Coastal Union, Twiga, Villa Squad, George Kavila alikaa kwa muda mrefu Kagera Sugar, miaka 11, tangu alipojiunga nayo (2007-2018) alipoamua kustaafu.
“Nina liseni D nakwenda kusoma C, faida za kukaa na timu kwa muda mrefu unajijengea uaminifu, pia kiwango chako kikiwa juu lazima mkataba unapoisha utasajiliwa kwa pesa ndefu na kuongezewa mshahara, shida ni kwa wale ambao hawapati nafasi, hao thamani yao inakuwa ndogo sana na biashara yao kisoka haiwi nzuri,” anasema.
FREDY MBUNA - KOCHA
Miaka 11 aliyokuwa ameichezea Yanga, tangu alipojiunga nayo (2000–2011), anasema mchezaji anayedumu kwenye kikosi ni yule ambaye huduma yake ni muhimu.
Baada ya kuondoka Jangwani alijiunga Moro United (2011-2013) na Majimaji (2013–2017), anasema timu hizo zilimwomba akazisaidie.
“Faida ya kudumu na timu mfano mimi nikaitwa Yanga kuwa ‘Kit Manager’ na sasa ni kocha ninayesimamia timu za vijana, nina leseni B naisaka A, hiyo inatokana na kuitumikia kwa uaminifu wakati nacheza uwanjani,” anasema.
Kutokana na hilo, kocha wa zamani wa Pan African, Godian Mapango anasema kama mchezaji anadumu kwenye timu, basi benchi la ufundi na viongozi wameona huduma yake inafaa kuendelea kuwepo.
“Hakuna kocha anayeweza akadumu na mchezaji asiye na faida na timu, ukiona mchezaji anakaa zaidi ya miaka mitano basi anastahili kuwepo kutokana na anachokifanya uwanjani,” anasema.