Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arsenal, Manchester City kazi inaendelea EPL

EPL Pict

Muktasari:

  • Lakini, Arsenal inafahamu wazi, nyuma yao kuna vigogo Manchester City, ambao wanaweza kuwang’oa kwenye kilele hicho cha msimamo wa Ligi Kuu England endapo kama watapoteza mchezo wao ujao, kisha wapinzani wao hao kwenye mbio za ubingwa, watafanya kweli kwenye mchezo wa Villa Park.

LONDON, ENGLAND: KWENYE msimamo wa Ligi Kuu England unavyosoma, Arsenal imeketi kileleni kwa tofauti ya pointi tatu baada ya kukusanya pointi 19 katika mechi nane, ambapo imeshinda sita, sare moja na kuchapwa moja. Imefunga mabao 15 na kufungwa matatu, hivyo ina tofauti ya mabao 12.

Lakini, Arsenal inafahamu wazi, nyuma yao kuna vigogo Manchester City, ambao wanaweza kuwang’oa kwenye kilele hicho cha msimamo wa Ligi Kuu England endapo kama watapoteza mchezo wao ujao, kisha wapinzani wao hao kwenye mbio za ubingwa, watafanya kweli kwenye mchezo wa Villa Park.

Uzuri ni kwamba Arsenal na Man City zote zitecheza Jumapili, ambapo Washika Bunduki wa Mikel Arteta watakuwa Emirates kuwakabili wapinzani wenzao wa kutoka kwenye jiji la London, Crystal Palace.

Utamu wa mechi hiyo itamshuhudia, Eberechi Eze akikabiliana na waajiri wake wa zamani, Palace baada ya kutua Arsenal kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Rekodi zinaonyesha Arsenal na Palace zimekutana mara 32 kwenye mechi za Ligi Kuu England na The Gunners imeshinda 19, mara tisa ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, wakati Palace imeshinda nne, mara mbili ilikuwa ugenini.

Man City itakuwa Villa Park kuwakabili Aston Villa katika moja ya mechi ngumu kabisa kwenye wikiendi hii. Kocha Pep Guardiola wa Man City, tumaini lake kubwa lipo kwa straika Erling Haaland, ambaye amekuwa moto kwelikweli kwenye ligi, akiwa ameshafunga mabao 11 hadi sasa.

Rekodi zinasoma, Man City na Aston Villa zimekutana mara 50 kwenye Ligi Kuu England, ambapo sare ni 10, huku Villa ikishinda tisa, saba nyumbani na Man City imeshinda 31, mara 10 ilipokwenda kucheza ugenini. Balaa hilo.

Mechi nyingine za Jumapili ni pamoja na Bournemouth ikiwa nyumbani kucheza na Nottingham Forest inayojitafuta, Wolves na Burnley, wakati Everton itakuwa na kibarua kizito nyumbani kukabiliana na Tottenham Hotspur. Everton imekuwa moto kwelikweli msimu huu ikichagizwa na uhodari wa kiungo mshambuliaji matata, Jack Grealish, huku Spurs ikitamba na huduma ya Mbrazili, Richarlison, ambaye amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu.

Lakini, kasheshe la Ligi Kuu England lilianzia Ijumaa kwenye mechi baina ya Leeds United na West Ham United, kabla ya Jumamosi, ambako kuna mechi nyingi za kibabe, zikianzia huko Stamford Bridge kwa wenyeji Chelsea kukipiga na Sunderland.

Kwenye Ligi Kuu England, Jumamosi ni ya moto, ambapo Newcastle United watakuwa na shughuli pevu ya kuikabili Fulham, huku Manchester United ikiwa na mtihani wa kuwakabili wababe wanaowatesa mara nyingi, Brighton kwa miaka ya karibuni. Hata hivyo, wakati timu hizo mbili zikikutana huko Old Trafford, rekodi zao zinasoma hakuna mbabe kwenye mechi walizokutana, ambapo mara 16 kwenye ligi, kila moja imeshinda mara nane. Mara tano nyumbani na tatu ugenini, ikiwa ni rekodi kwa pande zote mbili. Je, nani ataweka pengo la kushinda mara nyingi? Kitu kizuri katika mechi za Man United na Brighton, hazijawahi kutoka sare kwenye mechi ya Ligi Kuu England, huku mchezo wa mwisho uliofanyika uwanjani Old Trafford, Man United ilikubali kichapo cha mabao 3-1. Je, Ruben Amorim atakuwa na maajabu na Man United yake baada ya kupata mzuko wa kutoka kuichapa Liverpool wikiendi iliyopita?

Mechi ya usiku zaidi kwa Jumamosi itazikutanisha Brentford na Liverpool huko uwanjani

Gtech Community. Liverpool ya kocha Arne Slot itakwenda kwenye mechi hiyo ikiwa na jambo moja kichwani kugomea rekodi mbaya ya kupoteza mechi ya nne mfululizo kwenye ligi baada ya kuchapwa tatu zilizopita dhidi ya Crystal Palace, Chelsea na Man United.

Kwenye ubao wa rekodi, Liverpool imekuwa mtemi kwenye mechi zake dhidi ya Brentford, ambapo mara nane ilizokutana, sare ni moja na wakali hao wa Anfield wameshinda sita, ikiwamo mbili za ugenini, wakati Brentford imeshinda moja tu, ilipocheza nyumbani.

Lakini, hali ya sasa ndicho kitu kinachofanya mechi hiyo kuwa na mvuto mkubwa. Itakuwaje?