Al Ahly, Mamelodi karibuni, hii ndo Dar es Salaam!

SASA mambo yote ni hadharani. Baada ya kutangazwa ratiba ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika (CAFCL), sasa ni dhahiri bingwa mtetezi wa kombe hilo Al Ahly ya Misri na bingwa wa Ligi ya Afrika (AFL) Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini watakuwa jijini Dar es Salaam kwenye wikiendi mwishoni mwa Machi kwa ajili ya kupepetana na wenyeji Simba na Yanga.

Ni mapambano ya kihistoria kuwahi kutokea kwa pamoja kwenye jiji hili la Pwani ya Bahari ya Hindi. Haijawahi kutokea.

Wapenzi wa soka na hasa wafuasi wa klabu za Yanga na Simba walikuwa wameelekeza masikio yao katika jiji la Cairo ambako droo ya mashindano hayo ilikuwa ikifanyika.

Wanasema usiyemtaka kaja, ndivyo unaweza kuchukulia hisia za wapenzi hao wa soka mara ratiba ilipotoka na kuonyesha kuwa mafahali wanaolitawala soka la Afrika kwa sasa watakuwa ndani ya nyumba, Kwa Mkapa.

Kwa tunaoufahamu mpira, hili ni jambo la kufurahisha na wala si la kuogofya. Hayo ndio yalikuwa maombi ya Watanzania wengi kwa miaka mingi, yaani kuziona timu za nyumbani zinapambana na vigogo kama Al Ahly na Mamelodi.

Umahiri katika taaluma yoyote hupatikana kwa kupambana na walio mahiri. Bila kujali matokeo, mipambano hii itawaaacha Yanga na Simba wakiwa imara kama sio kiuchezaji basi ni katika mipango ya kufanya vizuri huko mbele.

Katika upande wa pili wa matukio, usiku wa baada ya droo ya robo fainali, Al Ahly anafungwa mabao 4-3 na National Bank of Egypt kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Misri.

Huko Afrika ya Kusini, Mamelodi wanatoka sare ya 1-1 na SuperSport kwenye Ligi Kuu ya DSTV. Katika usiku huo wa Jumanne, mnyama Simba aliifunga Singida Fountain Gate kwa mabao 3-1, hivyo kupunguza pengo la alama kati yake na Azam aliye nafasi ya 2 lakini Azam wakiwa wamecheza michezo miwili zaidi.

Al Ahly iko kwenye nafasi ya 10 ikiwa imecheza michezo minane katika Ligi Kuu ya Misri ikiwa nyuma kwa michezo 6 kulinganisha na Al Masri inayoongoza ligi ikiwa na michezo 14.

Mamelodi katika usiku huo wa Jumanne ilitoka sare ya 1-1 na SuperSport United katika Ligi Kuu ya DSTV. Ikumbukwe, Mamelodi au Masandawana kama inavyoitwa nyumbani, haijapoteza hata mchezo mmoja wa ligi kwa msimu huu inapofukuzia ubingwa wake wa saba mfululizo. Siku moja kabla ya kutangazwa kwa droo, Yanga iliifunga Ihefu kwa mabao 5-0. Ihefu ni timu pekee iliyoifunga Yanga kwenye msimu huu wa ligi.

Nimejaribu kuangaza matokeo ya hivi karibuni katika ligi za nyumbani za klabu hizo nne kuonyesha ubora na pia ukawaida wa Ahly na Mamelodi kama ilivyo kwa Simba na Yanga. Klabu hizo zinazotembelea Dar ni nzuri, lakini zinaweza kubanwa. Zinaweza kubanwa kwa sababu hata huko kwao kuna wakati zinakumbana na mazingira magumu mbele ya timu zinazodhaniwa kuwa ni za kawaida.

Kimataifa, Al Ahly ni mabingwa wa kihistoria kwani wamechukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa mara 43 na kwao ni kama wana hati ya ushiriki wa mashindano haya kuanzia robo fainali. Wapinzani wao si wageni katika mashindano haya kwani wameingia robo fainali mara nne katika miaka sita na sasa wanaisaka nafasi ya kuingia nusu fainali kwa mara ya kwanza. Simba vilevile si wageni wa kukutana na Ahly kwani timu hizo zimekutana mara kadhaa na matokeo mara nyingi yakimbeba mwenyeji jambo linaloufanya mchezo kuwa mgumu kwa Ahly pia.

Mamelodi wameingia robo fainali mara sita mfululizo na kumbuka pia ni mabingwa wa mwaka 2016. Msimu uliopita walitolewa katika ngazi ya nusu fainali na Wydad Casablanca ya Morocco. Hata hivyo, Mamelodi wanayo kazi ya ziada katika vita yao na Yanga. Yanga wanaweza wasiwe na wasifu kama wa Mamelodi, lakini kwa siku za hivi karibuni wamekuwa moja ya timu tishio barani Afrika hasa baada ya kutinga fainali za Kombe la Shirikisho (CAFCC) na kulikosa kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger. Yanga walichaguliwa kama moja ya timu 5 bora za msimu wa CAF 2023.

Katika miaka ya hivi karibuni, Uwanja wa Benjamin Mkapa umekuwa ngome kwa klabu za Tanzania na machinjio ya wageni. Mara nyingi timu za Yanga na Simba zimekuwa zikipata ushindi kwa njia na kiwango kinachohitajika.

Baadhi ya vipigo hivyo ni Simba 7-0 Horoya FC na hivi karibuni wakiichakaza Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa mabao 6-0.

Kama ilivyo kwa Simba, Yanga imekuwa ikitoa vipigo kwa kila timu iliyokuja Dar es Salaam. Ni Al Ahly pekee waliobahatika kutoka sare ya 1-1 na Yanga Kwa Mkapa katika msimu huu wa Ligi ya Mabingwa.

Simba wana uzoefu wa muda mrefu na wa karibuni pia wa kucheza na Ahly. Mechi ya karibuni ilikuwa kwenye Ligi ya Afrika ambako walitoka 2-2 Dar es Salaam na 1-1 Cairo, hivyo Ahly kusonga mbele kwa faida ya mabao mengi ya ugenini. Kwa jinsi hiyo Simba wana faida ambayo wanayo Ahly, pia faida ya kujuana.

Upande wa Yanga na Mamelodi hawajawa na bahati ya kujuana. Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amewahi kuifundisha Mamelodi lakini ni muda mrefu umepita na mambo mengi yamebadilika. Mbinu za makocha na uwezo wa wachezaji ndio utakaoshinda mechi. Kwenye uwezo wa kifedha Mamelodi wako mbali sana lakini matokeo ya karibuni yanaonyesha mpira wa Afrika unabadilika, hivyo pesa kutokuwa kete pekee ya kushinda mchezo.

Ni dhahiri kwamba mashabiki wengi wa Tanzania walitamani labda Simba akutane na Petro Atletico na Yanga akutane na Asec au hata Esperance. Kwa mtazamo wa kawaida na kwa viwango vya CAF hizi ndizo timu walidhani wanazimudu. Yawezekana hata Ahly na Sundowns walitamani kukutana na timu za Tanzania kuliko kukutana na timu zenye rekodi kubwa zaidi.

Pamoja na kupigania heshima, Ahly na Mamelodi wanakuja Dar es Salaam kusaka kibunda cha dola 2,500,000 sawa na Sh6.4 bilioni za Kitanzania iwapo wataingia nusu fainali na dola 4 milioni (Zaidi ya Sh10 bilioni 10) ya ubingwa.

Ikumbukwe timu 4 zitakazoishia robo fainali zitapata kiasi cha dola 1.3 milioni (Zaidi ya Sh3 bilioni).

Msukumo huo pia wanao Yanga na Simba. Fedha za zawadi zilizoongezwa na CAF zinakuwa kichocheo zaidi cha ushindani katika hatua hii. Yawezekana fedha hizi zikapindua meza na kuziinua timu zinazochechemea kiuchumi kama Yanga na Simba zinapolinganishwa na bajeti za Ahly na Mamelodi.

Al Ahly na Mamelodi Sundown wakaribishwe Dar. Waje Dar wakijua kwamba ni wachache wametoka salama katika miaka ya hivi karibuni. Wanaweza kuuliza uzoefu wa Jwaneng Galaxy na CR Belouzidad ilikuwaje katika michezo yao ya Dar es Salaam. Nani anajua, yaweza kuwa karibu mgeni mwenyeji apone.



Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.