Akpan injinia msomi anayeitaka nafasi yake Simba

UKARIMU, ucheshi na usikivu vimetawala maisha ya kiungo wa Simba, Victor Akpan anayecheza kwa mkopo Ihefu, ambaye anaamini furaha ya moyo ni tiba kwa afya ya binadamu.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Akpan sura yake ilijaa tabasamu na alijibu maswali kiustaarabu huku yale ambayo hakuwa tayari kuyajibu alitafuta namna nzuri ya kuyakwepa.

Kulingana na fani yake, Akpan anasema anahitaji zaidi utulivu wa akili na amani ya moyo ili kumsaidia kufanya kazi kwa wepesi, jambo linalomfanya chuki isiwe sehemu ya maisha yake.

“Naheshimu kila mtu, kwasababu kucheza mpira hakuwezi kunitofautisha na binadamu mwingine, siamini katika dharau ingawa sipendi kudharauliwa pia, ukiachana na hilo maisha ni mafupi yanahitaji furaha unapopata muda wa kufanya hivyo,” anasema.

Tangu ajiunge Ihefu, Akpan alitawaliwa na ukimya, hivyo amefunguka mambo mengi wakati anafanya makala na Mwanaspoti.


MAISHA YAKE SIMBA

Haikuwa rahisi kwake kucheza kwa kiwango cha juu, anafichua alikumbwa na majeraha yaliyomfanya asiwe fiti na baada ya kuona maneno yamezidi kwenye mitandao ya kijamii alilazimisha kucheza.

“Japokuwa sikuwahi kuulizwa nina shida gani iliyonifanya nisicheze mara kwa mara na hata nikipewa nafasi sikuonyesha ufiti unaotakiwa, nilishangaa kuona taarifa zangu kwenye mitandao ya kijamii, kila mmoja alikuwa anaandika anachokijua;

“Niliona taarifa ni nyingi na zilichangia kuivuruga akili yangu, ndio maana niliomba kutoka kwa mkopo ili nikapate nafasi ya kucheza na utulivu, ndio maana nipo Ihefu kwa miezi sita ambako napata nafasi ya kucheza na narudi kwenye kiwango kikubwa.”

Kitu kingine kilichompa changamoto, anaeleza alijiunga na Simba ikiwa kwenye presha kubwa ya kuhitaji matokeo mazuri, hivyo kutokana na majeraha ikawa ngumu kwake kuaminiwa moja kwa moja katika kikosi cha kwanza.

“Nakumbuka kocha Juma Mgunda alikuwa ananiambia kijana wangu punguza presha, uguza kwanza mguu upone usijilazimishe ukapata majeraha makubwa yatakayozaa tatizo juu ya tatizo.

“Kilichokuwa kinaniuma ni kuona nimesajiliwa tu nikapata majeraha na kama unavyojua Simba ina mashabiki wengi, lazima watahitaji kukuona unacheza vizuri.”

Licha ya kutopata nafasi ya kuonyesha uwezo wake, anakiri Simba imemfanya ajulikane zaidi tofauti na alivyokuwa Coastal Union ya Tanga.

“Kwa sasa nipo fiti, miguu yangu itaonyesha burudani waliyokuwa wanaitaka kutoka kwangu hata kama nipo Ihefu.”

Anamtaja Erasto Nyoni na Gadiel Michael kwamba ndio waliomsaidia katika nyakati ngumu kwake na walimuelekeza namna ya kuzikabili kuhakikisha hakati tamaa kutetea ndoto zake.


BAADA YA KUTUA IHEFU

Alipokutana na Yacouba Songne na Nelson Okwa walikaa chini na kupanga mikakati ya namna ya kufanya kazi zitakazowarejesha kwenye ubora baada ya kutoka kwenye klabu kongwe ambako walikosa nafasi.

“Tulikubaliana kupiga kazi itakayoonyesha thamani yetu, kwanza tulijiunga na Ihefu katika dirisha dogo ambalo kwa kawaida linahitaji watu wa kuongeza nguvu, tunapambana tuwezavyo kuhakikisha huduma zetu zinaibeba timu.

“Ihefu imepanda kutoka mkiani hadi nafasi za juu, jambo linalotupa faraja na nguvu ya kuhakikisha tunamaliza kwenye tano bora, tunaishi kwenye mazingira mazuri, kila kitu tunakipata.”


SOKA LA TANZANIA

Anasema soka la Tanzania lipo juu na linafuatiliwa na nchi mbalimbali kama Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda na kwingineko na amegundua vyombo vya habari vina nguvu kubwa ya ushawishi.

“Ukitaja ligi bora Afrika huwezi kukosa kuitaja Tanzania, vyombo vya habari vina mchango mkubwa wa kuwashawishi watu kuufuatilia mchezo huo, tofauti na nchi nyingine zinachukulia kawaida,” anasema.

Katika Ligi Kuu Bara anawakubali Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Yanga) na Abdul Suleiman ‘Sopu’ (Azam FC) na anawaelezea wana vipaji vikubwa na anaona wanaweza kucheza popote Afrika.

“Kuhusu Fei Toto, kama mchezaji ninayejua mchezo wa mpira ni wa muda mfupi naelewa anachopitia, wanaomshangilia leo akiwa staa watamcheka akistaafu kama hatajiwekeza kimaisha.

“Huenda kweli kakosea kuvunja mkataba, lakini Yanga wanaionaje thamani ya Fei Toto maana kwa sasa yupo kwenye kiwango cha juu asipopewa anachokitaka atapewa nyakati zipi, soka lina mambo mengi sana.”


ANAJUA KISWAHILI

“Tanzania bila Kiswahili unaweza kupata shida kubwa, nakumbuka wakati najiunga kwa mara ya kwanza Coastal Union, nilisemwa na wachezaji wenzangu, wakasema mchezaji gani kaja kapaka ‘bleach’ kichwani huyo atakuwa hamna kitu uwanjani.

“Niliumia sana na maneno yao, baada ya kufika uwanjani mazoezi ya asubuhi nilikwenda kumsalimia mmoja baada ya mwingine kwa Kiswahili, wakaanza ‘eh! kumbe mshikaji katusikia jana tukimsema’... iko hivyo, hata wakikufundisha lugha yao wanakufundisha matusi kwanza, ila mimi nilijifunzia Zanzibar,” anasema.


INJINIA AKPAN

Jamaa ni msomi. Akpan ana Shahada ya Injinia (Degree), lakini kwa sababu anapenda soka akaamua kujikita katika hilo, ingawa anakiri haikuwa rahisi wazazi wake kukubaliana naye.

“Nimetoka katika familia ya kisomi wazazi wangu hawakuniunga mkono kabisa kwenye soka kwani walihitaji niendelee na shule, hivyo ikitokea nikastaafu nitakwenda kufanyia kazi taaluma yangu,” anasema.