AKILI ZA KIJIWENI: Yanga iandae mzigo wa kumbakisha Aziz Ki

BAADA ya kuonyesha kiwango bora dhidi ya Mamelodi Sundowns, Stephane Aziz Ki alitoa kauli moja nzuri masikioni mwa mashabiki na wapenzi wa Yanga juu ya hatima yake klabuni hapo.

Aziz Ki ambaye ni raia wa Burkina Faso akiwa mzaliwa wa Ivory Coast alisema kuwa bado ataendelea kubaki ndani ya klabu hiyo kwa vile kuna jambo anahitaji kulitimiza akiwa na Yanga.

Kiungo huyo mshambuliaji ambaye anaongoza kwa kupachika mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na mabao 13 sawa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC ametoa kauli hiyo huku mkataba wake wa miaka miwili na Yanga ukikaribia kufikia tamati.

Ikumbukwe kwamba Aziz Ki mwenye umri wa miaka 28, alijiunga na Yanga, Julai 2022 hivyo mwishoni mwa msimu huu atakuwa anamaliza mkataba wake hivyo ili abakie hapo anapaswa kuongeza mkataba mpya au kujiunga kwingine akiwa mchezaji huru.

Klabu yoyote ya soka inapenda kusikia kauli kama ya Aziz Ki wakati mkataba wa mchezaji unapoelekea kumalizika huku akiwa muhimu kikosini lakini bado haipaswi kuifanya Yanga ione itakuwa na urahisi wa kumbakisha kiungo huyo.

Kwa sasa inatakiwa kuandaa kiasi kizuri cha fedha ambaho kitatosha kumfanya Aziz Ki atimize ahadi yake ya kubakia kikosini kwa vile mapenzi peke yake hayatoshi kumfanya mchezaji ajifunge klabuni.

Kuamini kwamba Aziz Ki anaweza kubaki kwa mshahara na dau lilelile la usajili kama ambavyo alipata katika mkataba uliopita ni kujiweka katika hatari ya kumpoteza kiungo huyo kwa vile wachezaji sio watu wa kuwaamini moja kwa moja.

Kama akipata fungu kubwa kwingine wala sio jambo la ajabu kuona akigeuka maneno yake na kuiacha Yanga kwenye mataa kwa vile anacheza soka kwa ajili ya fedha kwanza na ndio maana aliamua kuiacha Asec Mimosas iliyomlea na kumkuza na kujiunga na Yanga.