AKILI ZA KIJIWENI: Siri ya Hakim na mama yake

MIEZI kadhaa iliyopita, Achraf Hakimi alikuwa gumzo duniani baada ya kumzidi akili mke wake ambaye alitaka kuvuna utajiri wake kirahisi.

Mwanamke alifungua kesi mahakamani ya kudai talaka kwa Hakimi na kisha akaomba mali za nyota huyo wa PSG zipigwe pasu na kila mtu aondoke na chake jambo ambalo lingekuwa na hasara zaidi kwa beki huyo wa Morocco.

Hata hivyo, mwanamke huyo alijikuta kwenye mshtuko baada ya kubainika kuwa mali alizokuwa anazitegemea kwa Hakimi, hazikuwa chini ya umiliki wake na badala yake zilikuwa zikimilikiwa na mama wa mchezaji huyo.

Wengi waliona hilo kama jambo la ajabu lakini kumbe beki huyo ameonyesha uhalisia wa vijana wa kiume wa Morocco wa kuwa karibu zaidi na wazazi wao wa kike kwa maana ya mama zao kuliko baba zao.

Ndani ya miji tofauti ya Morocco, vijana wengi wa kiume wameonekana wapo kando ya mama zao iwe katika matembezi, sehemu za kupumzikia, migahawani na kwingine.

Rafiki yangu mmoja kule Rabat, Khalil Houssam alinifichulia kuwa jamii yao inampa thamani kubwa mwanamke na ndio maana watoto wengi wa kiume wanakuwa karibu na mama zao.

“Kwenye dini yetu, tunafundishwa kuwa mwanamke ana daraja kubwa na kwa mtoto anapomthamini mama yake kidini anakuwa amefanya jambo kubwa. Lakini sisi tunaheshimu wazazi wote ingawa mama ndio tunampa upendeleo zaidi kwa sababu yeye ndio mlezi wa familia,” alisema Houssam.

Nimefichuliwa kuwa kutokana na wazazi wa kiume kutokuwepo nyumbani mara kwa mara kutokana na harakati za kimaisha, watoto wanatumia muda mwingi kuwa na wazazi wao wa kike jambo linalotengeneza urafiki mkubwa baina yao.