AKILI ZA KIJIWENI: CAF ingemfikiria na Rais Samia Hassan

New Content Item (1)

Nimesikia na kuona Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) likitoa tuzo maalum kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Mfalme Mohammed VI  wa Morocco kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kusapoti mchezo wa soka barani Afrika.

Paul Kagame kilichombeba ni sapoti yake kwa mashindano ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambayo yale ya klabu na timu za taifa za wakubwa kwa wanaume amekuwa akitoa fedha za uendeshaji wake kwa muda mrefu.

Lakini pia ndiye amesapoti ujenzi wa ofisi ya Kanda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) nchini Rwanda na hivi karibuni alitoa fedha za ukarabati wa Uwanja wa Nyamirambo ambao sasa unaitwa Pele kwa ajili ya kumuenzi gwiji wa soka duniani, Edinson Arantes dos Nascimento aliyefariki mwaka jana.

Kwa upande wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco, yeye alipewa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya soka ndani na nje ya Morocco, kusapoti programu za soka kwa vijana wadogo pamoja na uwekezaji mkubwa alioufanya kwa timu za taifa za nchi hiyo.

Wakati nikisikia habari za viongozi hao kupewa tuzo, nikamkumbuka ghafla Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan jinsi anavyoonyesha nia ya dhati ya kusapoti michezo kama kaka zake hao wawili waliopewa tuzo.

Rais Samia kwa sasa ndiye mdhamini wa mashindano ya kanda ya soka kwa wanawake ya Cecafa lakini pia amekuwa akisapoti timu zote za taifa za soka Tanzania.
Ni Rais Samia ambaye ametenga kiasi cha Sh 10bilioni kwa ajili ya kukarabati viwanja vya soka nchini na amepanga kujenga na kuziendeleza shule za soka hapa nchini.

Kwa vile ni Rais Mwanamke na ndani ya muda mfupi ameonyesha ana nia ya dhati ya kusaidia mchezo wa soka, Fifa na Caf wangefanya uandamizi tu kwa kumpa tuzo na yeye.