Ajali ya Jonas Mkude, kweli mambo yamekwisha hivi hivi tu!

Muktasari:

  • Ilikuwa ajali kama zilivyokuwa nyingine zinazotokea kila siku nchini, lakini hilo haliwezi kuwa kikwazo cha kuacha suala hilo lipite hivi hivi.

 TANGU kiungo wa Simba, Jonas Mkude apate ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja, suala hilo linaonekana kutaka kupita hivi hivi, kiasi kwamba hakuna anayelizungumzia.

Ilikuwa ajali kama zilivyokuwa nyingine zinazotokea kila siku nchini, lakini hilo haliwezi kuwa kikwazo cha kuacha suala hilo lipite hivi hivi.

Nimeendelea kujiuliza maswali mengi, kwamba baada ya fainali ya Kombe la FA mjini Dodoma, ina maana wachezaji wa Simba waliachwa hivi hivi, waliachwa kila mtu aende na njia yake.

Je, wachezaji waliokuwa wamechaguliwa kujiunga Taifa Stars nao waliachwa kila mtu aende kivyake, bila kujali aina ya usafiri wanaotumia.

Wachezaji wengi waliochaguliwa Taifa Stars na inawezekana hata wale ambao hawakuwa katika kikosi hicho, walirudi Dar es Salaam wakitokea Dodoma kwa usafiri wa kudandia au kwa lugha nyepesi unaweza kusema walipata ‘lifti’.

Na hapo ndio kuna shida, kama mchezaji wa klabu kongwe kama ya Simba anaweza kudandia lifti ya gari yoyote bila kuzingatia ubora wa gari hilo, basi tuna safari ndefu sana.

Nieleweke vizuri, silaumu ajali hata kidogo kwa sababu najua kila siku nchi hii kuna ajali, nyingine ni bahati mbaya na kuna nyingine ambazo zinatokana na uzembe.

Lakini tujiulize maswali machache, hivi Simba walikuwa na mpango gani kuhusu wachezaji waliochaguliwa kujiunga Taifa Stars, waliwasusia TFF ili washughulikie usafiri wao?

Je, TFF ilikuwa na mpango gani kuhusu wachezaji hao? Kama ilikuwa inajua wachezaji zaidi ya saba wapo Dodoma, ilifanya mpango wowote wa kuandaa usafiri maalumu wa uhakika ili warudi salama.

Leo hakuna mtu ambaye anazungumzia suala hilo, kwa sababu aliyefariki ni shabiki, lakini kama ingekuwa amefariki mchezaji sidhani kama suala hilo lingebaki kimya kiasi hiki.

Ambacho kinasahaulika ni kuwa katika kila jambo, lazima kuwe kuna jambo la kujifunza, lakini kwa ninavyojua soka letu, sidhani kama Simba, TFF au wachezaji wenyewe wamejifunza lolote. Jambo hili litarudia tena na tena.

Sidhani kama tunahitaji miujiza kujua umuhimu wa wachezaji wetu wa klabu na Taifa Stars. Tatizo wanachukuliwa kama watu wa kawaida wakati walitakiwa kuchukuliwa kama ‘watu maarufu’.

Hawa ni watu maarufu na ndio maana hata sehemu wanazoishi inabidi ziwe na hadhi kubwa, waishi maisha maalumu, wawe na ratiba maalumu ya chakula, wawe na bima ya afya. Anayesimamia haya yote huwa ni mchezaji mwenyewe na klabu yake huwa inahusika.

Huwezi kumuacha mchezaji wako unayemtegemea tena nahodha wa timu, aombe lifti kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam. Kama ingekuwa ni nchi za watu walioendelea kuna watu walipaswa kuwajibika haraka kutokana na uzembe huo.

Sidhani kama uongozi wa klabu hapa nchini unajua nyumba wanazoishi wachezaji wao. Sidhani kama wanajua magari wanayoyatumia yana hadhi gani katika ubora na matengenezo.

Mkude amepata ajali, kwa bahati nzuri imemuacha hai, lakini sijui kama kuna aliyejifunza jambo lolote. Kama mambo yataendelea kubaki kama yalivyo basi kuna safari ndefu sana na mpira wetu huu utaendelea kudorora siku hadi siku.

Na kwa sababu mpira wetu umeendelea kudorora siku hadi siku, ndio maana hakuna maendeleo yoyote, mapenzi yamebaki kwa mechi moja tu; Simba na Yanga. Watu hawaendi uwanjani hata kuangalia Taifa Stars ikicheza.

Waliosababisha haya ni viongozi wa klabu na TFF ambao walipokuwa wakiomba kura waliahidi mambo mazuri na wakatuwekea mipango na vipaumbele vya kuvutia, walipoingia madarakani wakakutana na fedha isiyofanyiwa hesabu, wakachanganyikiwa. Wakasahau ahadi zao, nao wakageuka mchwa. Na hapo ndipo mpira wetu ulipofia.