Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afrika inavyosaka rekodi fainali za Kombe la Dunia 2026

Muktasari:

  • Kuongezeka kwa nafasi za Afrika kuliambatana na mjadala mkubwa. Wapo waliodai FIFA imeongeza idadi ya timu bila kuzingatia ubora wa ushindani, huku wengine wakiamini huu ndio ulikuwa wakati sahihi kwa bara hili kuonyesha uwezo mkubwa ambao kwa miaka mingi ulikuwa unakosa fursa ya kutosha kuonekana.

TORONTO, CANADA: FAINALI za Kombe la Dunia 2026 huko Amerika Kaskazini zimeanza kwa kishindo ambapo kwa mara ya kwanza katika historia Afrika inawakilishwa na timu 10, idadi kubwa zaidi ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 1930.

Kuongezeka kwa nafasi za Afrika kuliambatana na mjadala mkubwa. Wapo waliodai FIFA imeongeza idadi ya timu bila kuzingatia ubora wa ushindani, huku wengine wakiamini huu ndio ulikuwa wakati sahihi kwa bara hili kuonyesha uwezo mkubwa ambao kwa miaka mingi ulikuwa unakosa fursa ya kutosha kuonekana.

Baada ya kukamilika kwa raundi ya kwanza ya hatua ya makundi, bado ni mapema kutoa hitimisho la mwisho, lakini picha ya awali inaonyesha jambo moja muhimu; Afrika imeingia katika Kombe la Dunia hili ikiwa na ujasiri mkubwa kuliko wakati wowote ule katika historia.

Ni kweli kwamba sio kila timu imeanza vizuri. Zipo zilizopata ushindi, sare na nyingine zimepoteza. Lakini ukiweka pembeni matokeo na kuangalia namna timu hizo zilivyocheza, utaona wazi kuwa Afrika imepiga hatua kubwa katika ubora wa kiufundi, nidhamu ya mchezo na uwezo wa kushindana na mataifa makubwa ya soka duniani.

Katika miaka ya nyuma, timu nyingi za Afrika zilikuwa zinaingia Kombe la Dunia zikiwa na vipaji vikubwa lakini zikiandamwa na matatizo ya maandalizi, ukosefu wa utulivu wa kiutawala au kushindwa kukabiliana na presha ya mashindano makubwa. Safari hii hali inaonekana kuwa tofauti.


MOROCCO SIO KINYONGE

Kama kuna timu moja ya Afrika ambayo imeingia Kombe la Dunia 2026 ikiwa imebeba matumaini makubwa, basi ni Morocco, waliwasili katika mashindano hayo wakiwa na heshima kubwa baada ya kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.

Kutokana na historia hiyo, macho mengi yalikuwa kwenye mchezo wao wa kwanza wa Kundi C dhidi ya Brazil. Swali kubwa lilikuwa kama Morocco ingeweza kuthibitisha kuwa mafanikio ya Qatar hayakuwa bahati au ilikuwa imefikia kilele chake miaka minne iliyopita. Dakika 90 za kwanza zimeonyesha kuwa bado ni timu inayostahili kuheshimiwa.


Dhidi ya Brazil, Morocco ilipata sare ya bao 1-1 katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa. Licha ya kukutana na moja ya mataifa yenye historia kubwa zaidi ya soka duniani, Wamorocco walicheza kwa kujiamini, wakionyesha utulivu mkubwa wanapokuwa na mpira na nidhamu wanapolazimika kujilinda.

Kilichovutia zaidi ni kwamba Morocco haikuonekana kama timu inayotafuta kuzuia madhara dhidi ya Brazil badala yake, ilicheza kwa mpangilio, ikitengeneza nafasi na kuonyesha kwamba inaweza kushindana na timu yoyote katika mashindano haya. Sare hiyo imeongeza kujiamini ndani ya kikosi na kuifanya kuwa moja ya timu za Afrika zilizoanza vizuri zaidi.

Matokeo hayo yameiweka Morocco katika nafasi nzuri kuelekea mchezo wake wa pili dhidi ya Scotland ambao utapigwa usiku wa kuamkia Jumamosi. Mchezo huo unatarajiwa kuwa muhimu sana kwa sababu ushindi utaipeleka karibu zaidi na hatua ya mtoano. Scotland nayo inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na morali baada ya kuifunga Haiti bao 1-0 katika mchezo wake wa kwanza.


GHANA YAONYESHA NJAA YA MAFANIKIO

Kwa muda mrefu Ghana imekuwa miongoni mwa mataifa yenye historia kubwa na ya heshima katika Kombe la Dunia barani Afrika. Black Stars wamewahi kufika hatua za juu na kuacha alama kubwa, hasa kizazi cha mwaka 2010 kilichokaribia kufika nusu fainali kabla ya kuondolewa katika mazingira yaliyoacha maumivu makubwa kwa mashabiki wengi wa Afrika.

Miaka 16 baadaye, Ghana imeingia Kombe la Dunia 2026 ikiwa na dhamira mpya na kizazi kipya kinachotafuta kuandika historia yake. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakipewa presha kubwa ya matarajio, safari hii wameanza kwa utulivu zaidi na nidhamu kubwa.

Mchezo wao wa kwanza wa Kundi L dhidi ya Panama ulitoa jibu la mwanzo. Ghana ilipata ushindi muhimu wa bao 1-0, matokeo ambayo yamewaweka kwenye nafasi nzuri mapema katika mbio za kufuzu hatua ya mtoano.

Kilichovutia zaidi si ushindi pekee, bali namna Black Stars walivyocheza. Walionekana kuwa na mpango wa wazi, wakidhibiti mchezo kwa vipindi muhimu na kuonyesha ukomavu ambao mara nyingi hukosekana kwenye timu za Afrika katika mechi za aina hii.

Sasa Ghana inajikuta katika nafasi nzuri ya kupigania tiketi ya hatua ya mtoano, ikiwa na msingi imara kabla ya kukutana na wapinzani wake wakubwa zaidi katika kundi. Muhimu zaidi, ushindi huo umeongeza imani ndani ya kikosi kwamba wanaweza kushindana kwa kiwango cha juu zaidi katika mashindano haya. Mchezo ujao watacheza dhidi ya England, Juni 23.


IVORY COAST INAENDELEA KUKUA

Ivory Coast, imeingia Kombe la Dunia 2026 ikiwa na matarajio makubwa baada ya mafanikio yao ya AFCON 2024 ambapo walionyesha kwamba bado wana nafasi ya kurejesha heshima ya soka la Afrika katika ngazi ya kimataifa.

Katika mchezo wao wa kwanza wa Kundi E dhidi ya Ecuador, Ivory Coast ilipata ushindi muhimu ambao umeendelea kuthibitisha ukuaji wa kikosi hicho. Huo ulikuwa mchezo uliowahitaji uvumilivu, umakini na kutumia vizuri nafasi chache zilizojitokeza na walifanya hivyo kwa ufanisi.

Katika mechi yao ya kwanza, walionekana kuwa na utulivu mkubwa, wakidhibiti presha ya mashindano makubwa na kuonyesha ukomavu wa kikosi kilichojaa wachezaji wanaocheza katika ligi kubwa za Ulaya.

Ushindi dhidi ya Ecuador umeiweka Ivory Coast katika nafasi nzuri kuelekea hatua inayofuata lakini changamoto halisi bado ipo mbele yao. Mchezo dhidi ya Ujerumani utakuwa kipimo muhimu zaidi cha kuelewa kama kweli wanaweza kushindana na vigogo wa dunia au bado wanajijenga kuelekea kiwango hicho.


DR CONGO ILIVYOTIKISA

Miongoni mwa matokeo yaliyotikisa raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia 2026 ni sare ya bao 1-1 kati ya DR Congo na Ureno, moja ya timu zenye nyota wengi na historia kubwa katika soka la Ulaya na dunia.

DR Congo waliingia kwenye mashindano haya bila kelele nyingi lakini mchezo wao wa kwanza umebadilisha mtazamo wa wengi kuhusu uwezo wao. Wameonyesha kuwa hawapo Amerika kama washiriki wa kuongeza idadi, bali kama timu inayoweza kushindana na vigogo wa dunia.

Katika mchezo huo, Wakongo walionyesha ujasiri mkubwa, nidhamu ya mchezo na uwezo wa kustahimili presha ya muda mrefu dhidi ya timu iliyojaa vipaji vya kiwango cha juu. Hatua yao ya kupata sare dhidi ya Ureno imekuwa moja ya matokeo ya kushangaza zaidi katika hatua ya awali ya makundi.

Kilichoonekana wazi ni kwamba DR Congo imeingia mashindanoni ikiwa na mabadiliko makubwa ya kiuchezaji. Hawakuogopa jina la mpinzani wao, badala yake walicheza kwa mpango na kuonyesha kuwa wanaweza kusimama dhidi ya timu yoyote.

Matokeo hayo yameongeza imani ndani ya kikosi na pia yamewapa ujumbe wapinzani wao katika kundi kwamba safari yao haitakuwa rahisi. Kila pointi sasa ina thamani kubwa na sare hiyo inaweza kuwa msingi muhimu kuelekea hatua inayofuata.


Iwapo DR Congo itaendeleza kiwango hicho katika mechi zijazo dhidi ya Colombia na Uzbekistan, basi inaweza kuwa miongoni mwa timu zitakazoshangaza wengi katika Kombe la Dunia 2026 na kuandika historia mpya kwa soka la Afrika.


MISRI INATAKA HESHIMA YAKE

Kwa miaka mingi Misri imekuwa miongoni mwa mataifa makubwa zaidi ya soka barani Afrika, ikiwa na historia ndefu ya mafanikio katika mashindano ya Afrika na wachezaji waliowahi kutamba katika ngazi ya juu.

Hata hivyo, mafanikio hayo ya Afrika hayajawahi kuonekana ipasavyo katika fainali za Kombe la Dunia, jambo ambalo limekuwa chanzo cha presha na matarajio makubwa kila wanapoingia mashindanoni.

Katika mchezo wao wa kwanza wa Kundi G dhidi ya Ubelgiji, Misri ilionyesha dalili za timu inayotaka kubadilisha historia hiyo. Sare ya bao 1-1 imekuwa matokeo muhimu dhidi ya moja ya timu zenye wachezaji wengi wanaocheza katika ligi kubwa za Ulaya na imewapa Wafarao nafasi ya kuamini kwamba wanaweza kushindana katika kiwango cha juu.

Kilichoonekana zaidi ni utulivu wa Misri katika vipindi muhimu vya mchezo. Licha ya presha ya Ubelgiji na ubora wa wachezaji wake, Misri haikurudi nyuma kwa hofu, bali ilijibu kwa nidhamu na mpangilio mzuri wa kiuchezaji.

Hata hivyo, changamoto kubwa inayoonekana kwa kikosi hicho ni uwezo wa kumalizia nafasi wanazozitengeneza. Wamekuwa wakifika kwenye maeneo hatari, lakini kukosa makali mbele ya lango kumewagharimu kupata ushindi katika mechi za aina hii.

Kama Misri itaweza kuongeza ufanisi katika eneo la mwisho la uwanja katika michezo yake ijayo dhidi ya New Zealand na Iran, basi ina uwezo wa kuwa miongoni mwa timu zitakazofanya vizuri zaidi katika kundi lao. 


SENEGAL INA SABABU YA KUAMINI

Kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Ufaransa kinaweza kuonekana kama mwanzo mbaya kwa Senegal katika Kombe la Dunia 2026. Hata hivyo, ukitazama mwenendo wa mchezo huo ndani ya dakika 90, picha inakuwa tofauti kabisa na matokeo yanavyoonyesha.

Senegal ilianza mchezo kwa ujasiri mkubwa dhidi ya moja ya mataifa yenye ubora wa juu zaidi duniani. Ufaransa ilijulikana kwa ubora wa kikosi chake, kasi ya mashambulizi na uzoefu wa mashindano makubwa lakini Senegal haikuingia uwanjani ikiwa na hofu. Badala yake, ilionyesha nguvu, kasi na nidhamu ya kimchezo inayowafanya wawe miongoni mwa timu hatari kutoka Afrika.

Katika kipindi kikubwa cha mchezo, Senegal ilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga na hata kulazimisha Ufaransa kujilinda katika baadhi ya nyakati. Hii inaonyesha kwamba tofauti ya ubora kati ya timu hizi mbili haikuwa kubwa kama matokeo yalivyokuwa.

Hata hivyo, kilichoigharimu Senegal ni makosa machache ya kiulinzi pamoja na kushindwa kutumia nafasi muhimu walizozipata. Katika mashindano kama Kombe la Dunia, makosa madogo huweza kuamua matokeo na hilo ndilo lililowagharimu katika mchezo huu.

Licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, bado kuna sababu kubwa ya kuamini kwa upande wa Senegal. Kikosi chao kina uzoefu wa kutosha katika mashindano ya kimataifa na wachezaji wao wengi wanacheza katika ligi kubwa za Ulaya, jambo linalowapa uwezo wa kurejea wakiwa bora zaidi wakati ambao watakuwa wakikabiliana na Norway, Jumanne ya Juni 23.


CAPE VERDE YAANDIKA HISTORIA

Sare ya bila kufungana dhidi ya Hispania inaweza kuonekana kama matokeo ya kawaida lakini kwa Cape Verde ni moja ya siku muhimu zaidi katika historia yao ya Kombe la Dunia 2026.

Timu hiyo imeingia kwenye mashindano haya ikiwa na presha ndogo ukilinganisha na mataifa makubwa ya Afrika lakini hilo ndilo limewapa nafasi ya kucheza kwa uhuru na nidhamu dhidi ya moja ya vigogo wa soka duniani.

Hispania ilitarajiwa kutawala mchezo kwa umiliki wa mpira na kutengeneza nafasi nyingi za mabao lakini Cape Verde ilisimama imara, ikijilinda kwa umakini mkubwa na kudhibiti maeneo hatari ya uwanja.

Kilichofanya matokeo hayo kuwa ya kipekee ni kwamba Cape Verde haikufungwa hata bao moja dhidi ya timu yenye ubora wa kiufundi na uzoefu mkubwa wa mashindano makubwa. Hii inaonyesha ukuaji mkubwa wa kiufundi na kimbinu wa kikosi hicho.

Matokeo haya yameongeza heshima ya Cape Verde ndani ya kundi lao (H) na pia yamefanya wapinzani wao kuanza kuwachukulia kwa tahadhari zaidi. Baada ya kumalizana na Hispania, usiku wa kuamkia Jumatatu ya Juni 22 watacheza dhidi ya Uruguay saa 7:00 kwa Afrika Mashariki.


TUNISIA YAPATA ONYO

Ikiwa kuna timu ambayo imeanza Kombe la Dunia 2026 kwa changamoto zaidi miongoni mwa wawakilishi wa Afrika, basi ni Tunisia. Matokeo ya mchezo wao wa kwanza yameacha maswali mengi kuliko majibu huku presha ikiongezeka mapema katika hatua ya makundi.

Kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Sweden kimekuwa pigo kubwa kwa timu hiyo, Tunisia ilionekana kushindwa kudhibiti kasi ya mchezo, kupoteza umiliki katika maeneo muhimu na kushindwa kukabiliana na mashambulizi ya wapinzani wao.

Tatizo kubwa halikuwa mabao pekee yaliyofungwa, bali ni namna timu ilivyopoteza umbo lake la kiuchezaji ndani ya dakika 90. Hii imeibua maswali ya kiufundi na kimbinu kuhusu maandalizi yao kabla ya mashindano haya makubwa.

Kwa miaka mingi, Tunisia imekuwa ikipewa heshima kama moja ya timu zenye nidhamu nzuri ya kiuchezaji barani Afrika lakini mchezo huu wa kwanza umeonyesha mapungufu makubwa ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi haraka ili kubadili mwenendo wa kundi lao.

Sasa kikosi hicho kinakabiliwa na wakati mgumu. Mechi zinazofuata dhidi ya Japan na Uholanzi zitakuwa kama fainali, kwani matokeo mabaya zaidi yanaweza kumaanisha safari yao imeishia hapo.


ALGERIA YAKUMBANA NA UKWELI

Katika mchezo dhidi ya Argentina, moja ya mataifa yenye historia kubwa zaidi duniani, Algeria ilipata kipigo cha mabao 3-0. Matokeo hayo yanaonyesha wazi tofauti ya ubora, uzoefu na ukomavu wa kiuchezaji kati ya timu hizo mbili katika fainali za Kombe la Dunia.

Licha ya matokeo hayo kuwa mazito, Algeria ilionyesha kuhitaji kufanya kitu tofauti. Kulikuwa na vipindi ambavyo walijaribu kukataa unyonge na kutafuta nafasi za kushambulia lakini walikosa umakini katika eneo la mwisho na pia walipoteza mwelekeo walipobanwa na kasi ya Argentina.

Hata hivyo, bado Algeria inaonekana kuwa na nafasi, wakati mwingine fainali za Kombe la Dunia mara nyingi yamekuwa mashindano ya mabadiliko ya haraka na historia inaonyesha kuwa timu nyingi zimeanza vibaya lakini zikarejea na kufuzu hatua ya mtoano baada ya kurekebisha makosa yao.

Mechi zilizobaki dhidi ya Austria na Jordan zitakuwa kipimo halisi cha uwezo wao wa kujinasua. Kila mchezo unaosalia una uzito mkubwa na makosa madogo yanaweza kuwa na athari kubwa kwa safari yao kwenye mashindano haya.


AFRIKA KUSINI IPO KWENYE PRESHA

Bafana Bafana wamejikuta katika hali ngumu mapema kwenye Kombe la Dunia 2026, baada ya kupoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Mexico kwa mabao 2-0 na kisha kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wao wa pili dhidi ya Czechia.

Kwa sasa Afrika Kusini itahitajika kushinda katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Korea Kusini huku wakisikilizia matokeo ya timu nyingine  ili kuona kama wanaweza kutinga mtoano.


AFRIKA IMEPIGA HATUA GANI?

Kuna mabadiliko makubwa matatu ambayo yameanza kujidhihirisha wazi katika soka la Afrika.Kwanza, timu za Afrika sasa zimepunguza hofu walizokuwa nazo dhidi ya vigogo wa soka la dunia. Zamani, timu nyingi ziliingia uwanjani zikiwa tayari zimekubali ubora wa wapinzani wao kabla hata ya mpira kuanza.

Safari hii hali hiyo imeanza kubadilika huku ushindani ukiwa mkubwa zaidi hata dhidi ya majina makubwa.Pili, kiwango cha makocha kimeongezeka kwa kiasi kikubwa. Sasa timu nyingi za Afrika zinaonekana kuwa na mipango madhubuti ya kiufundi, mbinu zilizo wazi za mchezo na si kutegemea vipaji vya wachezaji pekee kama ilivyokuwa awali.

Tatu, wachezaji wa Afrika wamepata uzoefu mkubwa zaidi wa kucheza soka la kiwango cha juu. Idadi kubwa ya wachezaji sasa wanashiriki katika ligi kubwa barani Ulaya na kwingineko, jambo linalowasaidia kuhimili presha na kasi ya mashindano makubwa ya kimataifa.


JE, AFRIKA INAWEZA KUFIKA FAINALI?

Hili ndilo swali linaloanza kuzungumzwa kwa sas miongoni mwa wadau wa soka la Afrika kwa miaka mingi, ndoto kubwa ya Afrika imekuwa kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia. Historia inaonyesha jinsi ilivyokuwa ngumu kuvuka hatua hiyo, licha ya juhudi kubwa zilizowekwa na mataifa mbalimbali.

Cameroon mwaka 1990, Senegal mwaka 2002 na Ghana mwaka 2010 zote ziliishia hatua moja kabla ya kufikia ndoto ya fainali. Hata hivyo, Morocco ilivunja ukuta huo mwaka 2022 kwa kufika nusu fainali, jambo lililobadilisha mtazamo wa dunia kuhusu uwezo wa soka la Afrika.

Sasa mjadala umehamia hatua nyingine kubwa zaidi kufika fainali ya Kombe la Dunia. Je, inawezekana? jibu ni ndiyo, lakini si rahisi.