Abbas Magongo Zidane wa Tanzania aliyegeuka mali ya Kenya

INASIKITISHA sana. Watanzania walio wengi hawakuwahi kumuona mmoja kati ya wchezaji waliokuwa na kipaji kikubwa ambacho kilizaliwa katika kitongoji cha Rufiji na kukulia Kirumba jijini Mwanza. Si mwingine ni Abbas Khamis Magongo.

Jamaa alikuwa mwamba kwelikweli kwenye dimba la kati. Huyu unaweza kusema ni namba nane (kiungo) ambaye hakuwahi kutokea tangu nchi hii imeumbwa.


ALIMPIGA KIBAO KAKA’KE?

Baada ya kucheza cha ndimu, Abbas Magongo alijiunga na Toto Africans ya Mwanza kati ya mwaka 1976 hadi 1977. Timu hii ilikuwa chini ya uwenyekiti wa baba yake mzazi, Khamis Magongo. Mara baada ya kuachana na Toto Africans, Magongo aliibukia Pamba United ya Shinyanga ambapo alionyesha uwezo mkubwa sana.

Watu wengi wanalizungumzia hili, kwamba Magongo aliwahi kumpiga kibao kaka’ake, beki wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Toto Africans, Ibrahim Magongo (naye ni marehemu) aliyekuwa beki walipokutana kati ya Pamba United na Toto Africans lakini Mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Simba na Taifa Stars, Khalfan Abdallah Ngassa ‘Babu’ anafafanua.

“Hapana hakuwahi kumpiga, isipokuwa katika michezo ya Kanda, akiwa na Pamba United ya Shinyanga, mchezo mmoja kabla ya kukutana na Toto, alifanya tendo la makusudi ili asicheze dhidi ya timu yake hiyo ya zamani,” anasema Ngassa, baba mzazi wa nyota wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga, Simba, Azam na Taifa Stars, Mrisho Ngassa ‘Uncle’ na kuongeza;

“Sijui kama alilipa fadhila kwa sababu aliwahi kuichezea Toto au hakutaka kukutana na ndugu yake, ambaye alikuwa beki.”

   

MAGONGO ATUA KOGAL’O

Akiwa Pamba United pale Shinyanga, Abbas Magongo alishawishiwa na baharia mmoja aitwaye Juma Sentala kwenda Kenya. Safari yao ya kwanza ilikuwa Mombasa.

Babu Ngassa ndiye aliyerudi na mabegi mengine ya nguo ya baba yake mdogo kutoka Shinyanga hadi Mwanza.

Baada ya Magongo kucheza Mombasa kwa muda mfupi, alionekana na Gor Mahia ambao walimchukua. Kwa mara ya kwanza aliitumikia Gor Mahia ‘K’Ogalo’, Januari 1984. Ilikuwa ni katika mchezo wa kirafiki kabla ya kuanza kwa msimu ‘Pre-seasson’ na kuvutia mioyo mingi ya mashabiki wa timu hiyo.

Ni mara chache sana mchezaji kuwavutia mashabiki wake kama vile ilivyokuwa kwa  Magongo mashabiki wa K’Ogalo walimchagua kuwa mchezaji bora wa muda wote wa klabu hiyo na wakamtaja kwa furaha kwa jina la ‘Zamalek’.

Wakati anaitumikia K’Ogalo, Magongo alikuwa na ushirikiano mkubwa na Charles Otieno ‘Injinia’ ambaye baadaye alichukuliwa na Kenya Breweries na kumfanya kubaki na John Okello ‘Zangi’ na George Onyango ‘Fundi’


AITWA HARAMBEE

Mwaka 1986, Abass Magongo aliitwa timu ya taifa ya Kenya, ‘Harambee Stars’ kwa mara ya kwanza. Lakini kabla ya hapo, ndani ya miaka miwili kulikuwa na kelele za mashabiki wakihoji kwanini mwamba huyo haitwi kuitumikia timu hiyo.

Kitu ambacho wengi hawakukifahamu ni kwamba  Magongo hakuwa akimiliki hati ya kusafiria ya Kenya.

Baada ya kushawishiwa kubadilisha uraia, Magongo aliwasiliana na baba yake, mzee Khamis Magongo ambaye alimkubalia kwa sababu aliamini mwanawe alishashakuwa mkubwa na kumtaka atazame maslahi yake.


AWEKA ALAMA HARAMBEE STARS

Alikuwa mchezaji muhimu wa Harambee Stars kati ya miaka ya 1986 hadi 1991 chini ya Kocha Mohammed Kheri ambaye alimwona  Magongo kama mchezaji wake wa thamani zaidi mwaka 1987,  Magongo  alikuwa tegemeo la ushindi katika Kombe la Washindi Afrika mwaka 1987 akiwa na Gor Mahia.

Katika mashindano hayo, raundi ya mwisho Gor Mahia ilicheza  na Esperance ya Tunisia jijini Tunis, Magongo alifunga bao la kwanza kwa juhudi zake baada ya kuwazidi akili mabeki kadhaa wa Esparance kabla kumfunga kipa.

Katika mchezo wa marudiano Nairobi, Magongo alipiga kona iliyotua kichwani kwa Peter Dawo na kuwa bao.

Anatajwa kuwa na hasira sana. Mwaka wa 1988 hasira zake zilionekana wakati Harambee Stars ilipozuru Brazil, Kocha wa Harambee Stars, Chris Mokhoha na Meneja Joel Kadenge walimshutumu Magongo kwa kuwa kiongozi la wachezaji wenye utovu wa nidhamu. Magongo hakuwahi kuwa nyuma katika kupigania haki za wachezaji.


KWANINI ZIZOU?

Magongo alipokuwa uwanjani ilikuwa ni raha kumtazama akicheza pamoja na kwamba nyuma ya tabasamu zuri  na nywele zake za afro alikuwa na hasira kali ambayo mara nyingi hushindwa kuzizua pindi alipochukizwa.

Uwanjani Magongo aliwazidi ujanja wapinzani na miguso ya aina yake ya mpira. Alikuwa Zinedine Zidane wa Kenya. Pasi zake zilipendeza. Lakini tofauti na Zidane, Magongo alikuwa mfanyakazi chafu na ngumu zaidi uwanjani na pengine alikuwa fiti zaidi.

Alifunika kila majani ya uwanjani, akicheza kwa kujitoa na kuonyesha uwezo katika kushambulia, huku akirudi nyuma kusaidia safu ya ulinzi. Watangazaji wa Redio ya KBC mara kwa mara walikuwa wakisikkika wakisema ‘Abass Magongo anatawala uwanja mzima.’


ALICHEZA AFCON 1990

Kutokana na hali hiyo, Magongo alitemwa kwenye kikosi Harambee  Stars kilichokuwa kinaenda kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 1988 zilizofanyika Morocco.

Hata  hivyo, alifanikiwa kucheza mechi tatu za Afcon za mwaka 1990 zilizofanyika Algiers, Algeria.

Mashabiki wa Kenya, hususan wale wa Harambee Stars  walimtaja ndiye kiungo bora zaidi kuwahi kucheza Kenya. Maoni haya yalithibitishwa na kura zilizopigwa mtandaoni zikimbeba kiungo huyo aliyepata elimu yake katika Shule za Makongoro na Kitangili za Mwanza.


AASILI WATOTO

Khalifan Ngassa anamwita Abbas Magongo baba mdogo, anasema Magongo kule Nairobi kabla ya kufariki aliacha watoto wawili, mmoja wa kiume ambaye kwa sasa ni marehemu na mwingine wa kike aitwaye Pili.

Ngassa ambaye alihudhuria harusi ya Abbas kule Kenya, anasema mtoto huyo aliwahi kufika Tanzania akiwa mdogo pamoja na wazazi wake.

Hata hivyo, kuna taarifa  Magongo ambaye kwa baba na mama yake walizaliwa watatu tu na dada yake Zuwena na Ibrahim aliasili watoto 10 alioishi nao.  Akiwa Nairobi mara nyingi alikuwa akipendelea kuagiza samaki kutoka Mwanza na kuingia jikoni  na kuipikia familia yake.

Unajua mwisho wa enzi wa Magongo ulikuwaje? Je, Mrisho Ngassa nyota wa zamani wa Tanzania anayeshikilia rekodi ya mfungaji wa muda wote akiwa na mabao 25, aliwahi kumuona? Utapata majibu Jumapili ijayo...Itaendelea!