Abbas Magongo mwisho wa enzi

WIKI iliyopita tuliwaletea mchezaji wa zamani wa Tanzania, Abbas Khamisi Magongo ambaye baadaye alichukua uraia wa Kenya na kutamba na Gor Mahia na Timu ya Taifa ya Kenya, Harembee Stars.

Mwaka 1987 Magongo alibeba Kombe la Washindi Afrika akiwa na Gor Mahia ya Kenya na Mwaka 1990 alicheza fainali za Afcon zilizofanyika Algeria. Unataka kujua nini kilitokea zaidi? Sasa endelea.

Magongo aliitumikia Gor Mahia hadi mwaka 1991 alipoenda kujaribu bahati yake Uarabuni, Oman akiwa na wachezaji wengine kina Austin Oduo, Mickey Weche na Henry Motego.

Akiwa mchezaji, Magongo alikuwa rahisi kumpenda. Alikuwa na jicho la pasi za mauaji kwa ustadi wa kufunga mabao muhimu. Aliwahi kukokota mpira na kutoka katika ya mduara wa kati na kuwapita mabeki na kwenda kumfunga kipa mashuhuri wa AFC Leopards ‘Ingwe’,  Mahmoud Abbas wakati wa Mashemeji Derby ya 1984. Bao liingine kama hilo alilifunga dhidi ya Esperance katika mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Mandela.

Alirudi Kogalo kwa muda mfupi mwaka 1994 na alishiriki mchezo wa marudiano wa Kombe la CAF dhidi ya Zamalek.

Baada ya kustaafu soka, Magongo alichezea timu ya Wazee wa Kazi.


ALIKUWA MTU WA WATU

Huko Outering Estate alikokuwa akiishi karibu na Buruburu Estate jijini Nairobi, alikuwa ‘mtu wa watu’. Nyota ambaye alichanganyika kwa uhuru na wote na wengine bila ya kuwabagua.

“Kila alipokuwa akirudi kutoka safari ya nje ya nchi, marafiki zangu walikuwa wakikusanyika nyumbani kwetu. Kila mara alikuwa akituletea zawadi kama vile jezi, peremende na midoli kwa ajili ya watoto. Kila siku ilikuwa kama sherehe kwetu. marafiki wengi ambao waliendelea kututembelea kutoka kwa mashabiki hadi marafiki zake wa soka na pia majirani. Alipendwa na wengi,” alikaririwa Pillie Abbas Magongo, binti yake wa mwisho.

“Alitujali sote. Tulisherehekea siku zetu zote za kuzaliwa na alihakikisha kwamba sote tulienda shule. Tulikuwa kaka na dada. Alikuwa pia mtu wa dini ambaye alitufundisha kumcha Mungu,”  alisema Pillie babake alikuwa akiswali katika Msikiti wa Riyadh uliopo Majengo Nairobi na pia Msikiti wa Jamia katika Wilaya ya Biashara ya Nairobi.

“Kila ilipofika Desemba 31, watu wengi walipiga kambi nyumbani kwetu. Tulikuwa tukifyatua fataki kwenye nyumba yetu na majirani zetu wote walikuwa wakila na kunywa pamoja nasi tulipokuwa tukisherehekea Mwaka Mpya,” aliongeza.


KIFO CHAKE

Kifo chake kilitokea baada ya kupambana sana na Ugonjwa wa Nimonia kwa miaka kadhaaa, Magongo aliaga dunia katika Hospitali ya Mater jijini Nairobi Januari 29, 2001.

Haya yote yalikuja bila kutarajiwa na wengi baada ya mchezaji huyo kulazwa kwa wiki mbili katika hospitali hiyo Novemba 2000, Magongo aliruhusiwa na daktari akitoa dalili zote za kupona.

Hakika alionyesha maendeleo mazuri katika siku hiyo ya Jumatatu ya maafa.


ALIFUNGIWA NA CAF

Magongo alipata matatizo ya kupumua mapema asubuhi na mara moja alikimbizwa Hospitali ya Mater.

Kifo kililipokonya soka ya Kenya mchezaji mahiri ambaye alisimama katika safu ya kati ya K’Ogalo katika mchezo pekee wa kuwania ubingwa wa Kombe la Mandela mwaka 1987 mjini Cairo ambao ulimfanya afungiwe kucheza kwa miaka miwili -lakini kwa timu yake alikuwa mzalendo alimwachia kila mmoja tabasamu.

Mkewe Amina Ndindi Magongo alikuwa mtu wake mwaminifu na mwaminifu.

Magongo alimpenda Amina. Alikutana naye uwanjani, mwanamke huyo alikuwa shabiki wa mpira wa miguu na tangu walipoonana hakumruhusu kumtoroka. Alifunga naye ndoa na hakuwahi kupoteza nafasi ya kuthibitisha kwamba alikuwa na maana kubwa na alikuwa kila kitu katika maisha yake. Alimthamini kama mama wa watoto wake.

Amina naye alifariki dunia miezi 17 baadaye, Julai 4, 2002 na kupumzishwa katika makuburi ya Kiislamu ya Kariokor.

Mbali na kufanikiwa kupata watoto wawili na Amina, Magongo aliasili watoto wengine aliokuwa akiishi nao na kuwahudumia kama wanawe wa kuwazaa kati yao ni Ann Nduku, Swaleh Abbas Magongo, Alice Mulisya, Kevin Malive, Swaleh Mohammed, Brenda Mulisya, Dhahabu Swaleh, Rukia Ali na Irene Masiriana .


MRISHO NGASSA HAKUMUONA

Mrisho Ngassa kinasaba angemwita, Abbas Magongo babu yake lakini winga huyo hakuwahi kumuona mchezaji huyo. Ngassa alifanikiwa kumuona babu yake mwingine, Ibrahim Magongo ambaye alitumia muda mwingi kutananina naye kila walipoonana. Bahati mbaya babu yake huyo ambaye naye alikuwa beki mahiri wa Pamba FC alifariki dunia mwaka 2017.

Nawashukuru wote mliokuwa mkiifutilia safu hii ya Mjuaji, hasa wale ambao tuliokuwa tukiwasiliana kwa simu na kuzungumza mambo mengi ya zamani. Asanteni sana kwa maoni na ushauri wenu.