18 waula kwa wamiliki wa Southampton
KILIO cha wadau wa soka kinaelekea mwisho sasa hii ni baada ya wachezaji wa ndani kuanza kuonekana na kutoka kwenda kujaribu soka la kulipwa nje ya Tanzania.
Wazawa walikuwa hawana nafasi ya kutoka kwenda kujaribu soka la kulipwa nje na Tanzania ikiendelea kupanda kwa kukusanya mataifa mbalimbali kuja kucheza soka la kulipwa.
Sasa ni wakati wa Watanzania, hii ni baada ya vijana wa Kitanzania 18 walichaguliwa na kampuni ya Sports Republic, ambao ndio wamiliki wa klabu ya Southampton ya Uingereza, kwenda kuendelezwa kimasomo na kielimu kwanye kituo chao cha ABM Sport Republic kilichopo Bamako, Mali.
Baada ya Kelvin John ambaye pia aliondoka akiwa na umri mdogo sasa ni zamu ya vijana hao ambao pia wanandoto ya kufika mbali kisoka.
Wachezaji walioondoka ni Michael Aloys Michael, Edward John Jengerya, Rajabu Joseph Matimba, Mussa Mpemu Rajabu, Evastus Jali Lukanima, James Octavian Mtenga, Juma Yusuph Mwamsongo, Jafarri Mohamed Mwanyemba, Rahimu Salehe Omari, Jamlat Anuary Mwinyimkuu, Mohamed Hassan Hotalo, Hussein Hamid Mpagama, Diclass Mgeme.
Huku vijana wengine watatu wakiwa katika harakati za kuhitimu elimu yao ya kidato cha nne kwahio watasafiri mara baada ya kumaliza mitihani yao mwezi wa 11, 2023.
Vijana hao ni Machumu Shuba Biseko, Innocent Shija Lyangalu na William John Charles.
Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na Mkurugenzi wa kituo cha Football House, Mbaki Mutahaba ambaye amefunguka mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna walivyofanikiwa kuwapata wachezaji hao.
“Kama wenyeji wa Sport Republic hapa Tanzania, The Football House ikishirikiana na wadau wa mpira wa miguu wa mkoa/nchi husika tuliandaa zoezi la scouting kwa vijana wa umri ya chini ya miaka 17 na kwa vijana walio na umri wa chini ya miaka 22 na kumpeleka mgeni wetu katika mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam halafu tukampeleka Zanzibar;
“Zoezi lilifanyika kuanzia Aprili 24, 2023 mpaka Mei 1, 2023 kwa vijana wa umri kati ya 17-22 alichaguliwa mchezaji mmoja, Elias Lawi, anayechezea Coastal Union na alipata mwaliko wa kwenda Senegal mwezi wa sita, kwenye talent exhibition ambayo viongozi wa Southampton na wadau wake walikuwepo kutafuta vipaji vilivyo tayari kusaini professional contract,” alisema.
Mutahaba alisema kwa wale wa chini ya miaka 17, walipatikana kwanza 21 lakini baada ya mchujo wa pili ambao ulifanywa baada ya Sport Republic kutembelea nchi zingine barani Afrika kwa zoezi hilo hilo, walichujwa wakabaki 15.
“Taasisi yetu ya Football House ilishiriki kivyake kwenye kufanya zoezi la scouting katika mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ya mwaka huu mkoani Tabora na tulifanikiwa kujenga hoja kwa Sport Republic wawaongeze vijana wengine watatu na tunashukuru kwamba hoja yetu ilikubalika kwa hiyo hao watatu wataungana na wale 15;
“Hawa wote sasa wamepokea barua rasmi ya mwaliko wa kuendelezwa kielimu na kimpira kwenye kituo kipya cha ABM Foot Academy kilichopo Mali, ambacho kinaendeshwa na Sport Republic na tunatumaini watang’ara na hatimaye kupatiwa mikataba kama wachezaji wa kulipwa pale watapofikia umri sahihi kutokana na taratibu na sheria za FIFA,” alisema.