ZeKICK: Kibu rekodi zake zashtua Simba

Pablo atuma salamu.. aanza na dozi ya tatu huko

UNAPOZUNGUMZIA usajili uliotikisa msimu huu hutaacha kutaja jina la mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis wakati anatoka Mbeya City.

Sababu kubwa ya usajili huo kuwa gumzo ni kutokana na suala lililokuwa linahusu uraia wake ambapo awali alidaiwa kuwa na uraia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kabla ya Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene kumpa uraia Septemba 30, mwaka jana.

Katika kikosi cha Simba, Kibu ni mmoja wa washambuliaji ambao wameweza kuandika rekodi ya kipekee kwa msimu wa 2021/22, tangu alipofunga bao lake la kwanza kwani baada ya hapo amekuwa kwenye kiwango bora.

Mwanaspoti linakuletea takwimu zake tangu alipoanza kutupia bao la kwanza kwenye Ligi Kuu Bara akiwa na mabingwa hao watetezi.


KACHEZA DAKIKA 665

Katika michezo 10 ambayo Simba imecheza mpaka sasa nyota huyo amecheza minane akikosekana michezo miwili tu dhidi ya Biashara United Septemba 28 na Dodoma Jiji Oktoba Mosi, mwaka jana.

Michezo aliyotumia dakika zote 90 ni mitano dhidi ya Coastal Union, Namungo FC, Ruvu Shooting, Yanga na Azam FC, mitatu iliyobaki ni Tanzania Prisons dakika 45, Geita Gold (88), KMC (82) hivyo kuwa jumla ya dakika 665 alizocheza.


KACHANGIA MABAO MATANO

Kibu alianza kupata bao la kwanza akiwa na Simba kwenye mchezo na Ruvu Shooting Novemba 19, 2021, hivyo kuisaidia kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, huku mabao mawili yakifungwa na Meddie Kagere.

Baada ya kutupia ndipo moto wake uliendelea kuwaka kufuatia Desemba Mosi 2021 kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold kutoa asisti ya bao kwa winga Peter Banda dakika ya tisa kabla ya Mzamiru Yassin kutupia la pili na Simba kushinda mabao 2-1.

Desemba 24, 2021 aliweza kufunga mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya KMC uliopigwa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na kusababisha Simba kuondoka na pointi zote tatu muhimu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1, mabao mengine yakiwekwa kimiani na mabeki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Joash Onyango.

Januari Mosi, 2022 - ya Mwaka mpya aliuanza kwa neema baada ya kutoa asisti ya bao kwa Pape Ousmane Sakho wakati timu hiyo iliposhinda mabao 2-1 dhidi ya Azam FC huku bao lingine likifungwa na Sadio Kanoute.


BAHATI NA GUU LA KUSHOTO

Kawaida nyota huyu hutegemea sana mguu wake wa kulia katika uchezaji ila mabao yote matano aliyohusika nayo ni mawili tu aliyofunga kwa kutumia mguu wa kulia huku matatu akitumia kushoto.


WASIKIE WADAU

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Abdallah ‘King’ Kibadeni anasema kuwa Kibu ni mchezaji mzuri na kadri anavyozidi kufunga ndipo anatengeneza kujiamini zaidi.

“Kuendelea kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza ni jambo jema kwake maana inaonyesha ana kitu cha ziada ambacho kocha anakiona kutoka kwake,” anasema Kibadeni.

Kwa upande wake beki wa zamani wa kikosi hicho, Boniface Pawasa anasema kuwa mchezaji huyo akiendelea kujituma atakuwa bora zaidi ya hapa alipo kwa sasa.

“Anazidi kuimarika siku baada ya siku na ukimwangalia jinsi anavyopambana uwanjani unaona ni mchezaji mwenye njaa na kiu ya mafanikio,” anasema Pawasa.