Simba ameingia katika mtego wa Panya Nigeria

Monday November 23 2020
edo pic

SIMBA ni mnyama mkubwa, lakini ni kama vile Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), imewawekea mtego mdogo wa panya. Ni katika pambano lao la kwanza la kufuzu michuano ya klabu ya Afrika dhidi ya Plateau United ya Nigeria.

Mtego wa panya kivipi? Kuna mambo mengi ndani yake. Kwa mfano, jina la Nigeria ni kubwa katika soka, lakini kwa miaka mingi sasa Wanigeria na watu wengine wa Afrika Magharibi hawatambi sana katika soka la ndani ya Afrika.

Timu ya mwisho kutoka Nigeria au tuseme kutoka Afrika Magharibi iliyofanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika ilikuwa Enyimba. Ilitwaa mara mbili mfululizo. Mwaka 2003 na 2004. Kuanzia hapo Wanigeria na rafiki zao wa Afrika Magharibi ubingwa wa Afrika wameishia kuutazama katika televisheni tu wakiwa wamekaa sebuleni.

Enyimba ilifanikiwa kutokana na uwekezaji wa tajiri mmoja wa mafuta aliyeamua kukusanya mastaa na kupiga kazi kama ambavyo tajiri wa Mamelodi Sundowns, Patrice Motsepe alivyoamua pale Afrika Kusini.

Kwanini watu wa Afrika Magharibi hawatwai taji hili? Majibu ni mawili rahisi. Kwanza hawafanyi uwekezaji wa kutosha katika klabu zao, lakini pili licha ya ukubwa wa soka katika nchi zao mastaa wao wengi wanacheza nje ya nchi. Wengi hawana muda na soka la nyumbani.

Haishangazi kuona katika ngazi ya klabu za Afrika Kaskazini huwa zinatamba lakini katika timu za taifa mara nyingi zile za Afrika Magharibi huwa zinatamba zaidi. Wanafanya kazi rahisi tu ya kuwakusanya kina, Sadio Mane na kuunda timu imara za taifa. Katika klabu zao za ndani hawana kina Mane.

Advertisement

Simba inaingia katika mtego huu dhidi ya Plateau. Kwanza tunatazamia kuiona timu ambayo haina uwezekaji mkubwa kuliko Simba, lakini ghafla inaweza kuiacha Simba ikiwa katika aibu kubwa kama wao watapita na kuiacha Simba katika mataa.

Hawa Wanigeria tunatazamia watakuwa na wachezaji wenye vipaji vizuri, lakini tunataka kuona kama wataiingiza Simba katika mtego wa Panya. Kwamba soka la Nigeria linaweza kusimama juu muda wote licha ya uwekezaji mkubwa unaoweza kufanyika katika klabu moja kubwa ya Tanzania.

Mwaka 2003 wakati Simba ilipokutana na Enyimba katika michuano hii hadithi ilikuwa tofauti. Enyimba ilikuwa katika uwekezaji mzuri wa kuwatoa Simba na pia kuvisumbua vigogo vingine vikubwa barani Afrika kama Zamalek, Al Ahly, Esperance, Etoile du Sahel na wengineo.

Kudhihirisha zilikuwa timu mbili tofauti, mwishoni mwa msimu huo Enyimba ilimuuza mshambuliaji wao, Steven Wrogu kwenda El Marreikh ya Sudan kwa dau la dola milioni moja. Jiulize ilifanyia nini hizo pesa. Jiulize namna ilivyokuwa inamiliki wachezaji wenye thamani kubwa.

Leo sitazamii kuiona Plateau ikiwa daraja moja na Enyimba lakini kama ikifanikiwa kuitoa Simba basi itaniachia maswali mengi. Uwekezaji wa Simba utanipa mashaka makubwa. Hiki ni kipimo tosha kwa kuanzia kuliko kucheza na timu za Comoro au Shelisheli ambazo mara nyingi tunapewa katika raundi ya kwanza.

Hapo hapo unakumbuka jinsi ambavyo mara ya mwisho Simba walitolewa na timu ndogo ya UD Songo kutoka kule kwa Wamakonde Msumbiji. Unajiuliza kama Simba ikitolewa katika hatua hii na timu kutoka Nigeria. Inaweza kuonekana kwamba labda walibahati tu kufika hatua ya makundi misimu miwili iliyopita.

Huu ni mtego wa Panya. Haiwezekani Simba itolewe mara mbili mfululizo katika hatua hii baada ya kufika makundi huku wakijinasibu wana timu ya kimataifa. Nadhani itapaswa kurudi nyuma na kujitazama na pia kuchunguza zaidi michuano hii inataka nini?

Simba imetoka kuwababua Coastal Union mabao 7-0 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha. Ni mwendelezo wa ubabe katika soka la ndani tangu pale walipoishia kwa mara ya mwisho katika michuano ya kimataifa baada ya kuondolewa na UD Songo.

Lakini kuna hili jambo jingine ambalo linasumbua akili kidogo. Kikosi cha Simba kinaonekana kama vile hakipangiki kwa namna ambavyo kimejaza mastaa. Kuna kina Clatous Chama, Bernard Morrison, Larry Bwalya, Chris Mugalu, Luis Miquissone na wengineo.

Wakati fulani huwa najiuliza. Kikosi hiki ambacho wengine ukiita Dream Team kimefikia uwezo wa kwenda moja kwa moja na kufika fainali za Afrika. ukikitazama ukiwa ndani unaona kama vile Simba haina mapungufu hata eneo moja. Tatizo linakuja katika mechi kama hizi unapogundua kuwa timu yao kumbe bado ina mapungufu na ni timu ya kawaida tu.

Mtego huu wa Panya utawaacha Simba ikibana meno na kugundua kwamba labda wanahitaji wachezaji zaidi ya Chama na wengineo waliopo kikosini. Ni mtego wa Panya ambao kama wakishindwa kujinasua utawaachia maswali mengi kuhusu safari yao ya kuwafikia wababe wa Afrika kina Raja Casablanca na wengineo.

Mtego huu wa Panya pia utaitafakarisha sana Simba kiasi cha kuamua kuanza mradi mwingine badala ya huu. Kwa sasa Simba wanaweza kujisamehe kwa kufungwa na akina Al Ahly, Wydad Casablanca na wengineo lakini hawatajisamehe kwa kufungwa na Plateau katika hatua ya mwanzo tu.

Advertisement