Miaka 22 ya unyonge kwa makocha wazawa!

Miaka 22 ya unyonge kwa makocha wazawa!

SIO ajabu, huko mitaani mara nyingi mmewahi kukutana na mabango hayo. Mabango yanayotundikwa na kubandikwa katika maeneo tofauti, lakini vyote vikitangaza biashara ya aina moja. Ni kama vile wenye matangazo hayo wameambizana waandike nini. Nazungumzia yale mabango na vibao vya matangazo ya waganga wa kienyeji. Mengi hubandikwa katika nguzo za umeme ama juu ya miti na yote yakitangaza biashara za waganga hao.

‘Je unataka kujiunga na freemason? Unataka kupandishwa cheo kazini...Umekimbiwa na mume au mke? Muone mtaalamu...!’

Lingine katika kunogesha litasomeka; ‘Mganga kutoka Nigeria au Ufipa...una tatizo la nguvu za kiume, unaandamwa na mikosi? Mtaalam ana dawa ya mafanikio na mvuto kazini, dawa ya kuongeza akili, mwanao atafaulu mitihani bila kusoma...’ Wizi mtupu!

Bango lingine lenye kujaa vitisho linaweza kusomeka hivi; ‘Kiboko ya Majini, mwenye pete za mvuto na bahati...hashindwi na chochote...ndani ya nusu saa tu, mume au mkealiyekukimbia atarudi...anatoa dawa ya utajiri....piga simu...’

Hao wanaojita wataalamu wamekuwa wakivuna fedha, kwani kuna baadhi ya watu wanawaamini matapeli hao. Wamekuwa wakijipeleka wenyewe na kuliwa fedha zao sana tu. Hii ni kwa sababu ndani ya watu hawafanani. Watu lazima watofautiane hata kama ni watu wa tumbo moja na hata kama ni mapacha wa toka nitoke!

Ni kama vile katika soka letu, japo wote wanaupenda mchezo huo, lakini kila mmoja ana ushabiki wake. Hapa nchini kama shabiki fulani wa soka sio mnazi wa Jangwani, basi lazima atakuwa wa Msimbazi...!

Lakini hiyo yote ni kutaka kunogesha tu, ile burudani ya soka, wakifurahia kuziona timu zao zikipata mafanikio.

Bahati mbaya ni kwamba mashabiki hao wa soka na wadau wengine huko, mitaani hawajawahi kukutana na mabango au matangazo ya hao waganga wakitangaza kuwa na dawa za kuwawezesha makocha wazawa kunyakua UBINGWA wa Ligi Kuu Bara.

Kama atajitokeza tapeli mmoja, akaliweka bango la tangazo lake mitaani au kutupia kwenye mitandao ya kijamii, huenda jamaa huyo atavuna fedha nyingi. Kila shabiki angependa kuona unyonge wa makocha wazawa mbele ya wageni unafutika kama sio kufa kabisa. Wangependa kuona taji hilo la Ligi Kuu Bara likianza kubebwa na Kocha Mzawa kwani kwa sasa ni miaka 22 HAWAJASHUHUDIA.

Ndio, huu ni msimu wa 22 tangu John Simkoko aliponyakua taji hilo akiiongoza Mtibwa Sugar kuzima ubabe wa vigogo Simba na Yanga. Alizima ubabe wa makocha wa kigeni.

Kocha Simkoko alitwaa taji hilo mara mbili mfululizo akianza msimu wa mwaka 1999 na kulitetea tena 2000 na kuwa mzawa wa mwanzo na mwisho kuligusa taji hilo hadi leo hii.

Tangu Simkoko afanye hivyo mara ya mwisho taji hilo limekuwa likipita mikononi mwa makocha wa kigeni, wengi wao wakiwa Wazungu, huku makocha wazawa wakiwa wasindikizaji ama kuwa wasaidizi wa wageni hao. Aibu iliyoje hii?!


REKODI HII HAPA!

Kocha Mkenya, Marehemu James Siangía alimpokea Simkoko taji hilo msimu wa 2001 na 2003 akiifundisha Simba. Mwaka 2002 Siang’a alizidiwa akili na Mmalawi aliyekuwa Yanga Jacky Chamangwana, ambaye alirejea tena kubeba taji hilo la Ligi Kuu misimu miwili mfululizo ya 2005 na 2006. Chamangwana kwa sasa ni marehemu.

Mwaka wa 2004, Mzambia Patrick Phiri aliipa Simba taji hilo kabla ya kurejea kufanya hivyo tena msimu wa 2009-2010 kwa rekodi ya kutopoteza mchezo hata mmoja msimu huo.


TWALIB? HAPANA!

Ingawa katika Ligi Ndogo mwaka 2007 Twalib Hilal nyota wa zamani wa Tanzania aliyeng’ara na Simba alikuja kuipa klabu yake hiyo ya Simba taji ndani ya muda mfupi, lakini ni ngumu kumhesabia kama mzawa kwa vile alishakuwa na uraia wa Oman. Yaani alikuja Simba akiwa sio Twalib yule Mtanzania alikuja kama M-Oman.

Baada ya mfumo wa Ligi kubadilishwa na kuwa na msimu wa kuunganisha miaka miwili, kocha mjanja mjanja kutoka Serbia, Dusan Kondic alitwaa taji hilo mara mbili akiinoa Yanga 2007-2008 na 2008-2009.

Naye Mganda, Sam Timbe aliingia kwenye rekodi ya makocha wageni kubeba ubingwa wa Bara akiinoa Yanga msimu wa 2010-2011, kabla ya Kocha mwingine Mserbia, Milovan Cirkovic kuipa Simba taji la mwisho la Ligi Kuu msimu wa 2011-2012. Milovan aliyewahi kuinoa Simba mara mbili, alikabidhiwa taji lake kwa kishindo baada ya Simba kuifumua Yanga mabao 5-0 katika mechi iliyotumika kukabidhiwa taji lao Mei 6, 2012. Ilikuwa bab’kubwa!


MOTO ZAIDI

Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi, Ernie Brandts alikuja kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutoka nchi kubwa barani Ulaya kubeba taji nchini.

Kocha huyo aliisaidia Yanga kushinda taji msimu wa 2012-2013 kabla ya Mcameroon aliyetimuliwa katikati ya msimu wa 2017-2018 ndani ya Simba, Joseph Omog naye aliandikisha rekodi yake.

Omog, alinyakua ubingwa akiwa na Azam msimu wa 2013-2014 akiwa amekipokea kikosi kasi kutoka mikononi mwa Stewart Hall na msimu uliofuata wa 2014-2015 Mholanzi mwingine, Hans Van Pluijm akalinyakua taji hilo kabla ya kulitetea tena 2015-2016.

Msimu wa 2016-2017 Mzambia, George Lwandamina aliipa Yanga taji lao la 27, likiwa ni la tatu mfululizo akitoka kumpokea kazi Babu Pluijm.


MATAJI YA SIMBA

Kwa misimu minne mfululizo, imeshuhudiwa makocha wa kigeni ndani ya Simba wakibeba mataji kibabe.

Alianza Mfaransa Pierre Lechantre aliyewazidi akili Lwandamina aliyekuwa Yanga kabla ya kutimka na kumuachia kibarua Mwinyi Zahera sambamba na Aristica Cioaba wa Azam FC aliyechemsha mapema kwenye mbio za ubingwa za 2017-2018.

Msimu uliofuata baada ya Lechantre kutimka, kazi ikaachwa kwa Mbelgiji, Patrick Aussems aliyelitwaa taji la 2018-2019 na 2019-2020 ilikuwa zamu ya Sven Vanderbroeck pia kutoka Ubelgiji na msimu uliopita, taji likabebwa na Mfaransa Didier Gomes.


HATA MSIMU HUU

Hata msimu huu ligi ikiwa imesaliwa na michezo ya raundi nane kabla ya kukamilika Juni 29, kuna kila dalili ya wazi ya kocha wa kigeni kulibeba tena taji hilo la Ligi Kuu Bara, kwani kama sio Nasreddine Nabi wa Yanga basi ni Pablo Franco wa Simba.

Nasreddine ni Mbelgiji mwenye asili ya Tunisia na Pablo ni kocha kutoka Hispania. Wazawa wanasubiri nini? Tusubiri pengine msimu ujao, lakini kwa sasa imebaki historia tu!

Kwa unyonge huu kwanini shabiki wa soka nchini asitamani kwenda kwa mtaalumu kama wataliona bango linalotangaza kuwa, ipo dawa ya kuwawezesha makocha wazawa kubeba taji la TPL? Maana sio kwa msoto huu!

Bila ya shaka umefika muda wa makocha hao kutupa mashuka ya unyonge waliojifunika katika usingizi wa pono ili warejesha heshima yao katika Ligi Kuu Bara.