Kumbe bao nyingi zina gundu Kombe la Dunia

DOHA, QATAR. HISPANIA imeichapa Costa Rica mabao 7-0 katika mechi ya kwanza ya Kundi E kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar juzi Jumatano.
Ni ushindi mzito wa kwanza kwenye fainali hizi, lakini je, wenyewe ni namba moja kwenye historia ya fainali hizo?
Hispania ilivyojipigia Costa Rica. Kwanza imefunga mabao kwenye vipindi vyote viwili, cha kwanza ikifunga mabao matatu na cha pili ikipachika manne.
Dani Olmo alifungua akaunti ya mabao hayo, kisha Marco Asensio na Ferran Torres wakafunga kabla ya mchezo huo kufika mapumziko.
Torres alifunga tena kwenye kipindi cha pili na kufuatia bao matata kabisa la Gavi lililofanya ubao usomeke mabao 5-0.
Wakati mechi ikikaribia dakika ya 90, Hispania iliongeza mabao mengine mawili kupitia kwa Carlos Soler na Alvaro Morata – ushindi uliowafanya La Roja kuongoza Kundi E kwa kujinafasi zaidi.
Kitu cha kushangaza, ushindi huo wa Hispania si mkubwa kwenye historia ya fainali za Kombe la Dunia, kwa sababu kuna timu nyingine nne zilishawahi kufunga idadi kama hiyo tangu michuano hiyo ilipoanza mwaka 1930.
Majirani zao Hispania, Ureno wao walishinda 7-0 dhidi ya Korea Kaskazini kwenye Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini, ambapo mabao yalifungwa na wachezaji sita tofauti.
Uturuki nao waliichapa Korea Kusini Saba Bila mwaka 1954 kama ambavyo ilifanya Uruguay dhidi ya Scotland katika fainali hizo hizo za Kombe la Dunia 1954.
Mechi ya mwisho kushuhudia ushindi wa mabao 7-0 kwenye fainali za Kombe la Dunia ni ile ya Poland ilipoichakaza Haiti mwaka 1974. Na hapo 7-0 bado si ushindi mkubwa Kombe la Dunia.
Ni hivi, Ujerumani wao waliichapa Saudi Arabia 8-0 kwenye Kombe la Dunia 2002, kama ambavyo Uruguay ilifanya dhidi ya Bolivia Kombe la 1950, wakati Sweden iliishushia kipigo cha mabao Nane Bila Cuba kwenye Kombe la Dunia 1938 – ikiwa ni moja ya ushindi mnono kabisa kwenye rekodi za Kombe la Dunia.
Hata hivyo, Hungary ndiyo timu iliyowahi kushinda mabao mengi zaidi kwenye mechi moja ya Kombe la Dunia, ilipofunga mara kumi dhidi ya El Salvador kwenye Kombe la Dunia 1982. Katika mechi hiyo, Hungary iliruhusu bao moja, hivyo wakaibuka na ushindi wa mabao 10-1, ushindi ambao upo juu ya ule wa 9-0 iliichapa Korea Kusini 1954 na Yugoslavia ilipoikamua 9-0 Zaire kwenye Kombe la Dunia mwaka Juni, 18, 1974.
Hata hivyo, timu hizo zilizowahi kuibuka na ushindi mnono kwenye mechi za Kombe la Dunia, hakuna hata moja ambayo ilimaliza ikiwa bingwa kwa mwaka husika.
Je, Hispania itaondoa hilo gundu na kuibuka na ubingwa Desemba 18 baada ya kuichapa Costa Rica mabao 7-0? Tusubiri tuone. Mchawi muda.