‘First Eleven’ Simba, Yanga

Muktasari:

JANA Jumamosi pale Kwa Mkapa ilikuwa ipigwe mechi ya Karikoo Derby. Hii ni mechi ambayo ilikuwa inazungumzwa kila kona ya nchi, kwani ilikuwa inakutanisha miamba ya soka nchini kwenye Ligi Kuu Bara.

JANA Jumamosi pale Kwa Mkapa ilikuwa ipigwe mechi ya Karikoo Derby. Hii ni mechi ambayo ilikuwa inazungumzwa kila kona ya nchi, kwani ilikuwa inakutanisha miamba ya soka nchini kwenye Ligi Kuu Bara.

Ni Simba ambao walikuwa waikaribisha Yanga katika mechi ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo, baada ya mzunguko wa kwanza Yanga kuwa wenyeji wa watani zao na kutoka sare ya kufungana bao 1-1.

Ingekuwa mechi ya mambo mawili; ushindi na heshima. Kila timu ilikuwa inasaka pointi tatu huku kila moja ikisaka kuweka heshima ya kutofungwa na mtani wake ambapo yaliyojitokeza ndiyo kama mlivyosikia. Kutokana na ubora wa vikosi vya timu hizo msimu huu, Mwanaspoti linakuletea ‘first eleven’ ya mechi ambayo inaundwa na nyota wa timu hizo.

MANULA - SIMBA

Vikosi vya timu zote mbili vina makipa sita, lakini Aishi Manula anapewa nafasi ya kuwa katika kikosi cha kwanza kutokana na kiwango chake bora alichoonyesha msimu huu.

Manula katika Ligi Kuu ndiye kipa aliyecheza mechi nyingi bila kuruhusu bao, vilevile ameendeleza ubora hata katika mashindano ya kimataifa ambayo amedaka mechi tano na kuruhusu bao moja.

Katika ligi kipa huyo amecheza mechi 14 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

KAPOMBE-SIMBA

Beki wa kulia, Shomary Kapombe ataanza kwenye kikosi hicho na hakuna ubishi katika ubora wake anamzidi Kibwana Shomary wa Yanga.

Kapombe ni bora katika kuzuia mawinga wasumbufu kama Tuisila Kisinda, Deus Kaseke na mwingine yoyote ambaye huwa anakutana naye.

Miongoni mwa silaha za Simba katika kushambulia ni Kapombe ambaye huwa anapiga krosi na pasi za maana kwa washambuliaji na kufunga mabao, lakini muda mwingine hufunga mwenyewe.

ZIMBWE - SIMBA

Katika nafasi ya beki wa kushoto pale Yanga inaonekana kusuasua sio Yassin Mustapha ambaye ni majeruhi wala Adeyun Saleh.

Mabeki hao wawili wote hawapo katika viwango bora na kuna muda hufanya makosa ambayo yanaigharimu timu.

Hivyo kwenye kikosi hicho moja kwa moja Mohammed Hussein ‘Zimbwe’ ataanza. Ana uwezo wa kukaba ingawa kuna wakati anazidiwa, lakini ni mzuri zaidi timu inapokuwa inashambulia mara kwa mara.Huenda ubora huo wa Zimbwe Jr uliwavutia mpaka Yanga ambao siku chache zilizopita walikuwa wakihusishwa kumsajili.

NINJA - YANGA

Abdallah Shaibu ‘Ninja’ beki wa kati wa Yanga hakuanza vizuri msimu huu kwani alikuwa mchezaji ambaye anaishia benchi na wakati mwingine kutokuwepo kwenye orodha ya wachezaji 18.

Nafasi ya beki wa kati walikuwa wakicheza Lamine Moro na Bakari Mwamnyeto, lakini wakati huu mambo yamebadilika kwenye kikosi hicho.

Ninja amekuwa ni mchezaji wa kikosi cha kwanza na kucheza mara kwa mara tangu amepewa nafasi na aliyekuwa kaimu kocha mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi.

Moja ya nguzo ya ulinzi ya Yanga ni Ninja ambaye amekuwa akicheza kwa nguvu na kujitolea hata katika makosa ambayo wachezaji wenzake hushindwa kufanya vizuri.

ONYANGO - SIMBA

Tangu amesajiliwa Simba mwanzoni mwa msimu huu, beki wa kati, Joash Onyango ameingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na ukweli ni kwamba amekuwa bora.

Ndani ya Simba amekuwa ngome imara akicheza na Paschal Wawa au Kennedy Juma kwa nyakati tofauti, jambo linalomfanya aingie kwenye kikosi hiki cha kombaini.

LWANGA - SIMBA

Taddeo Lwanga anaingia nafasi ya kiungo mkabaji kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukaba na kuzuia mashambulizi ya timu pinzani kabla ya kuwafikia mabeki wao.

Lwanga ni mmoja wa wachezaji walio katika kiwango bora tangu amesajiliwa Simba wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea nchini Misri. Kutokana na uwezo wake huo wa kuzuia viungo washambuliaji bora wa timu nyingine kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ umempa nafasi hiyo.

KISINDA - YANGA

Pindi Yanga wanaposhambuliwa Tuisila Kisinda amekuwa akishuka chini kumsaidia kukaba beki wa kulia au kushoto wa timu yake na kuifanya timu hiyo kuwa salama.

Kisinda, ubora mwingine mkubwa ambao ameuonyesha ni uwezo wake wa kukimbia kwa kasi anapokuwa na mpira na kuwafanya mabeki wa timu pinzani kuwa na wakati mgumu kumzuia.

Katika ubora huo wa kukimbia anapokuwa na mpira alioonyesha Kisinda hata katika mechi ya kwanza na Simba alisababisha timu yake kupata penalti ambayo Michael Sarpong aliifungia bao la kuongoza.

MUKOKO - YANGA

Kwenye kikosi hicho nafasi ya viungo watacheza wawili; Lwanga na Tonombe Mukoko ambaye naye amekuwa bora na uwezo wa kuwazuia wapinzani.

Mukoko tangu amejiunga na Yanga msimu huu ameifanya timu hiyo kuwa imara katika safu ya kiungo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukaba mpaka mwisho.

Kiungo huyo Mkongomani sio katika kukaba tu, bali alionyesha uwezo mwingine hata kwenye kushambulia na mpaka sasa ameifungia timu hiyo mabao matatu katika Ligi Kuu Bara.

SOGNE - YANGA

Katika mechi nne za Yanga ambazo wamecheza tangu kurejea kwa ligi baada ya kusimama kutokana na msiba mkubwa ilioupata nchi wa kuondokewa na Rais wa tano, John Magufuli, Yacouba Sogne amefanya vizuri.

Katika mechi tano ambazo Yanga walicheza mshambuliaji huyo amefunga mabao matatu ikiwemo lile ambalo alifunga mechi ngumu ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Tanzania Prisons.

Washambuliaji wa Simba ambao wameonekana kuwa na idadi ya kufunga mabao mengi katika ligi, lakini tangu kurejea kwa ligi hawakuwa na makali zaidi kama aliyoonyesha Sogne.

CHAMA - SIMBA

Kiungo fundi wa Simba, Clatous Chama amefunga mabao saba kwenye ligi mpaka sasa, lakini pia ametoa pasi za mwisho 13 ambazo wachezaji wengine wamezitumia kufunga mabao.

Chama anaingia kwenye kikosi hicho kutokana na ubora wake hasa Simba wanapokuwa na mpira wakati wa kushambulia anahusika kwenye mambo mengi sahihi ikiwemo kutoa pasi za mwisho na kufunga mwenyewe.

Kiungo huo anaingia moja kwa moja kwani anapokuwa uwanjani hasa timu yake inaposhambulia ni mchezaji hatari.

MIQUISSONE - SIMBA

Hakuna ubishi kuwa moja ya mawinga hatari nchini ni Luis Miquissone. Huyu anawasaidia mabeki kukaba au kwenda kufanya mashambulizi mbele.

Ndani ya Simba, Luis ni mmoja wa wachezaji hatari ambao muda wote anatakiwa kuchungwa kwani anaweza kufunga, kutoa pasi za mwisho pamoja na kuwasumbua mabeki wa timu pinzani muda wote.

Luis ameonyesha ubora huo sio katika mashindano ya ndani ikiwemo ligi aliyofunga mabao manane, bali hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye hatua ya makundi amefunga mabao matatu.