Bolly Collins bondia aliyepofuka macho kwa ngumi, akaamua kujiua

New Content Item (1)
New Content Item (1)

ILIKUWA Juni 16, 1983 katika ukumbi wa Madison Square Garden jijini New York, Marekani, Billy Collins Jr akiwa na baba yake aliyekuwa bondia wa zamani, Collins Sr walikuwa ukumbini tayari kwa ajili ya pambano la utangulizi kabla ya miamba Roberto Duran na Davey Moore kuzichapa.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Wakati anaingia katika pambano hilo Collis Jr alikuwa ameshapigana mara 14 na kushinda mapambano yote huku 11 kati ya hayo ikiwa ni kwa KO.

Watu wengi walikuwa wakimpa nafasi ya kushinda tofauti na mpinzani wake, Luis Resto ambaye licha ya kuwa hatari umri nao ulikuwa unakwenda kumtupa mkono.

Pembeni ya Collis Jr kulikuwa na kocha wake ambaye pia ndiye aliyekuwa baba yake. Wakati huo Collins Jr ndio kwanza alikuwa na umri wa miaka 21.
Kwa upande wa Resto alikuwa na kocha wake, Panama Lewis.
Kengele ilipigwa na raundi ya kwanza ikaanza. Licha ya watu kufahamu kwamba Resto hakuwa na ngumi nzito, lakini kadri muda ulivyozidi kwenda ngumi zake zilionekana kumuathiri.

Mabondia hao walipigana katika raundi zote 10 na hadi pambano linamalizika Collins Jr alikuwa ameshachakazwa vya kutosha.


New Content Item (1)
New Content Item (1)

Macho yake yalionekana kuvimba vya kutosha na hata akaonekana kama ameng’atwa na nyuki au dondora.
Baada ya hapo mwamuzi aliwasogeza mabondia hao wawili katikati ya ulingo na akanyanyua mkono wa Resto kuashiria kwamba ndiye mshindi kwa mujibu wa pointi za majaji.

Mshindi alipotangazwa baba yake Collins Sr alikwenda kumpa mkono Resto ikiwa ni ishara ya kukubali kushindwa na kumpongeza kwa ushindi wake.

Lakini, baada ya kumshika mkononi wakati ambao Resto bado akiwa na glovu zake, baba wa Collins aling’amua kitu.
Aligundua kwama glovu za Resto zilikuwa ni laini sana kwenye eneo  la kupigia na ni kama hakuwa amevaa glovu.

Wakati mzee Collins Sr anang’amua hilo, Resto naye alishaona kuwa ameshtukiwa na akawa anang’ang’ana mzee huyo asije akamgusa mkono wake.


New Content Item (1)
New Content Item (1)

Vurugu zikavuka ukumbini na watu wote kutolewa ndani. Kesho yake kamisheni ya mchezo wa ngumi New York ilianza kufanya uchunguzi.

Baada ya hapo mazito yakaibuka. Uchunguzi huo ulibaini kwamba kocha wa  Resto aitwaye Panama alikuwa amefanya mchezo mchafu kwa kutoa baadhi ya sponji katika glovu za bondia huyo na kuzifanya ziwe laini, na iwe ngumu kwa Collins Jr kuweza kuzivumilia na kumsababishia madhara makubwa.

Jambo la kwanza lililofanyika baada ya matokeo ya uchunguzi huo ilikuwa ni kumfutia ushindi Resto na kufuta pambano lenyewe.

Wakati uchunguzi huo unaendelea, Collins alikuwa hospitali ambako madaktari walifanya kila waliloweza kuhakikisha anapona, lakini ilishindikana.


New Content Item (1)
New Content Item (1)

Macho yake yaliharibiwa vibaya na ngumi za Resto, hususani eneo la kiini na baada ya matibabu ya muda madaktari wakaweka wazi kwamba bondia huyo hataweza kuona tena, hivyo  itakuwa ndio mwisho wake wa kupanda ulingoni.

Kamisheni ya ngumi jijini New York iliwafungia maisha Resto na Panama kushiriki mchezo wa ngumi na wakati hilo linafanyika mwezi mmoja baada ya pambano familia ya Collins iliishtaki kamisheni hiyo, mwamuzi wa pambano, kampuni iliyoandaa pambano na ile iliyotengeneza glovu za Resto sambamba na wakaguzi waliozikagua kabla ya mechi.

Lengo la kufungua kesi hiyo lilikuwa ni kutaka fidia kwa kilichotokea, lakini mahakama ilitupilia mbali mashtaka yote.
Mwaka mmoja baada ya tukio hili, Collins Jr akiwa kwenye upofu wa milelele taarifa ya kushtusha ikaibuka. Ilikuwa ni siku ya Jumanne ambapo dunia ilitangaziwa kifo chake.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali ni kwamba bondia huyo alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea karibu na nyumba aliyokuwa akiishi. Gari hiyo alikuwa ikiendeshwa na rafiki yake ilitumbukia kwenye daraja akakutwa akiwa amefariki akiwa kwenye gari.


New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kwa mujibu wa taarifa kutoka jarida la Sports Illustrated, pamoja na maneno ya baba yake,ajali haikutokea kwa bahati mbaya bali ilikuwa imepangwa na Collins mwenyewe ambaye aliamini ni bora apoteze maisha kuliko kuendelea kuishia maisha ya tabu akiwa kipofu.

Miaka mitatu tangu pambano hilo lilipofanyika, yaani 1986, Resto na Panama walishtakiwa kwa kupanga na kutumia silaha kwa ajili ya kumshambulia mtu, ambapo Resto alifungwa jela miaka miwili ingawa kuna ripoti zinadai alifungwa kwa mwaka mmoja na nusu, kisha Panama akafungwa mwaka mmoja.

Awali, Resto alikataa kabisa kuhusika katika mpango wa kuzifanya glovu ziwe laini wakati anakwenda kupambana na Panama ndio alikiri kwamba alifanya hivyo bila ya bondia wake kujua, lakini mambo yalikuja kufichuka baada ya miaka mingi kupita.


New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ilikuwa mwaka 2009 wakati Resto alipokuwa katika mahojiano na makala ya ‘Assault in the ring’, alipofichua kwamba ni kweli alifahamu juu ya ujanja uliofanywa katika glovu zake na pia akaongeza kwamba alipewa na dawa zilizomsaidia pumzi isikate haraka wakati anapambana.

Resto alikuwa akizungumza haya huku machozi yakimtoka akijutia kwa kile alichokifanya.
Kocha wake Panama alifariki dunia mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 74, lakini hadi leo jina lake halitasahaulika katika mchezo wa ngumi juu ya ukatili na kitendo cha kinyama alichowahi kukifanya.

Miezi kadhaa baada ya pambano, kamisheni za ngumi duniani kote ziliziongeza umakini katika ukaguzi wa vifaa vyote vya mchezo wa ngumi na zikaundwa sheria zaidi zinazomlinda bondia wakati wa pambano.