SIMULIZI YA HADITHI: Jana dume -5

Muktasari:

  • Enjo alipompata mwanamme huyo alihisi kuwa alikuwa ameukata. Si muda mrefu akagundua ameingia choo sicho. Juhudi za kumkimbia zikagonga mwamba, kwani jamaa hakuwa mwanaume bali Janadume…!

LIPOISHIA...
Akanyamaza kidogo kisha akaniuliza.
“Tukutane saa ngapi?”
“Kama saa kumi jioni hivi.”
Ningeweza kukutana naye wakati wowote lakini niliona nimtajie tu muda huo ili aone nilikuwa mtu wa mipango.


SASA ENDELEA...

“SAA kumi nikukute mimi au utanikuta wewe?” Akaniuliza baada ya kimya kifupi.
“Vyovyote itakavyokuwa. Kama utawahi wewe kufika utanisubiri. Kama nitawahi mimi nitakusubiri.”
“Ahadi za kizungu nitaziweza wapi?” Nilikuwa nikijisemea kimoyomoyo baada ya kuniuliza. “Nikukute mimi au utanikuta wewe?’
“Okey, hiyo ni ahadi nyingine itimize tafadhali.”
“Usijali Mr Dachi.”
Nilipotaja jina hilo akafurahi.
“Nitajali kama hutatimiza ahadi yako.” Akaniambia huku akionyesha furaha aliyokuwa nayo.
“Ondoa wasiwasi, nitafika.”
“Okey, asante sana.”
“Asante.”
Nikakata simu.
Nikaendelea kunywa chai yangu huku nikimfikiria mzungu huyo. Kwa jinsi nilivyokuwa nikizifahamu tabia za wanaume nilishatambua kuwa yule mzungu alikuwa akinitaka kimapenzi lakini alishindwa kuniambia wazi. Badala yake aliamua kuzungusha maneno kwa kuniambia anataka tuwe marafiki bila kufafanua urafiki huo ni wa aina gani.
Nilikuwa nimeshaweka msimamo kuwa endapo ataweka pesa mbele, nitakuwa tayari kuwa naye mradi tu tutumie kinga kwani sikuwa tayari kuzaa mtoto wa kizungu.
Nikakumbuka kwamba aliwahi kuniuliza kama nilikuwa na mchumba. Nikajiambia kama atataka kuwa na uchumba na mimi itabidi kwanza nimchunguze tabia zake kabla ya kumkubalia.
Baada ya kumaliza kunywa chai niliondoa vyombo nikaenda kuviosha kisha nikarudi sebuleni kwangu na kupumzika kidogo huku nikichezea simu yangu.
Saa saba mchana nikawa kwenye saluni moja kutengeza nywele zangu. Nilitaka nikikutana na yule mzungu anione niko moto!
Ilikuwa saa tisa nilipotoka saluni nikakodi bodaboda iliyonirudisha nyumbani. Nilibadili nguo nyingine kisha nikatoka. Wakati bodaboda inanishusha pale hotelini ilikuwa saa kumi kasoro dakika mbili hivi. Nilitaka niwahi ili yule mzungu aone nina ahadi.
Wakati naingia kwenye lango la hoteli, kwa pembeni mwa macho yangu nilimuona mzungu huyo amesimama kando ya mti uliokuwa pembeni mwa ile hoteli.
Sikugeuza uso wangu kumtazama. Nilijifanya kama sikumuona. Nilihisi kwamba alifika mapema  akisubiri saa kumi ya ahadi yetu aingie ndani.
Hata baada ya mimi kuingia  humo hotelini na kuketi, yule mzungu hakunifuata japokuwa alishaniona wakati ninashushwa na wakati ninaingia humo hotelini.
Alisubiri mpaka ilipofika saa kumi kamili ndipo nilipomuona akiingia. Tabia yake ile ikanishangaza. Nikajiuliza ndio tabia za wazungu au….?
Wakati nawaza hivyo yule mzungu alikuwa akitupa tupa macho kwenye ukumbi ule wa hoteli, akaniona.
Akatembea taratibu kuelekea katika meza niliyokuwa nimeketi.
“Oh karibu.” Nikamwambia mara tu alipofika karibu na meza yangu.

“Asante.”
Alivuta kiti akaketi.
“Habari ya kutoka muda ule?” Akaniuliza.
“Nzuri. Ndio unafika?” Nikajidai kumuuliza.
“Ndiyo ninafika.” Akanijibu. Nikajua anasema uongo kwani nilishajua kuwa alifika mapema.
“Asante kwa kutimiza ahadi yako.” Akaniambia.
Mhudumu naye alikuwa ameshafika.
“Naweza kuwahudumia.” Akatuambia.
Nikamtazama yule mzungu.
“Utakunywa nini?” Akaniuliza.
“Nitakunywa soda tu.”
“Hapana. Utakunywa bia. Sema unataka bia gani?”
Nikacheka kidogo kabla ya kumuuliza.
“Wewe unataka ninywe bia?”
“Ndiyo.”
“Nitakunywa Kilimanjaro.”
Mzungu naye akaagiza mzinga wa konyagi.
Mhudumu alipoondoka, mzungu huyo aliniambia alikuwa amefurahi kuwa na mimi siku ile. Alinitajia sehemu mbalimbali ambazo alisema aliwahi kuniona kabla ya siku ile na akanipenda.
Sehemu alizonitajia ilikuwa ni kweli niliwahi kufika. Hapo nikajua kuwa kukutana kwetu hakukuwa kwa bahati tu bali alikuwa akinifuatilia.
Mazungumzo yetu hayo yalikatizwa wakati yule mhudumu alipotuletea vileo tulivyoagiza.
Wakati tunaendelea  kunywa, Dachi alinitamkia kuwa alikuwa amenipenda sana. Bila shaka ile pombe aliyokuwa anakunywa ndio iliyompa ujasiri wa kunitamkia maneno hayo kwa uwazi.
Kwa upande wangu nilikuwa nikimchekea tu. Nikagundua kuwa mzungu huyo anapolewa anakuwa na maneno mengi sana na hana aibu ya kuzungumza.
Akataka na mimi nimtamkie kuwa nimempenda. Nikamwambia kuwa nimempenda.
Nilipomwambia hivyo akaanza kung’ang’ania aende na mimi nyumbani kwake akimaanisha kule hotelini alikokuwa akiishi.
“Tutakwenda siku nyingine si leo.” Nikamwambia.
“Kwanini isiwe leo?” Akaniuliza huku akinitolea tabasamu.
“Leo sikupanga kuja kwako, nilipanga nije hapa tuzungumze.”
“Sasa utakuja lini?”
“Kwani wewe huna mke?” Nikamuuliza.

Dachi akatikisa kichwa.
“Mke wangu utakuwa wewe.”
“Huko kwenu Ujerumani huna mke?”
“Sina.”
“Una maana hujaoa bado?”
“Bado.”
“Kwanini?”
“Mimi nataka mke wa Kiafrika kama wewe.”
“Na hapa Dar huna msichana mwingine?”
Dachi akatikisa kichwa.
“Bado sijampenda yeyote zaidi yako.”
Wakati tunazungumza nilikuwa ninakunywa ile bia  taratibu huku nikimtazama mzungu huyo na kupima maneno yake.
Ingawa nilimtamkia kuwa nampenda lakini sikuwa nimeshafanya uamuzi wa kuwa naye kwa haraka haraka vile.
“Utakuja lini nyumbani kwangu?” Akaniuliza tena baada ya kupita ukimya mfupi.
“Nitakwambia.”
Jibu langu hilo likaufanya uso wake ufadhaike.
“Sikiliza. Naona bado hujaniamini lakini mimi ni mtu wa ukweli. Nitahakikisha kuwa maisha yako yanakuwa ya furaha utakapokuwa na mimi. Nitakununulia nyumba, nitakununulia gari na kama utanizalia mtoto nitakupeleka kwetu ukaishi huko na utakuwa kama malkia wangu.”
Maneno yake yalianza kunitia tamaa. Nikaanza kufikiria kuachana na mpenzi wangu Eddie, Mzanzibari ambaye alikuwa akisoma huko Uingereza ambaye tulipanga kuja kuoana atakapomaliza masomo yake.
Wakati namuwazia mzungu huyo niliona akitia mkono kwenye mfuko wa suruali yake akatoa bahasha iliyonona. Akaniambia.
“Chukua.”
Nikanyoosha mkono wangu na kuichukua ile bahasha.
“Ni milioni kumi.” Akaniambia huku akinikabidhi bahasha yenye noti za Dola 4,000, na kuongeza:
“Utakwenda kuzihesabu nyumbani. Tia kwenye mkoba wako.”
Sikupenda kudhihirisha usoni kwangu ni kwa jinsi gani nilifurahi. Nikafungua mkoba wangu na kuitia bahasha hiyo ya pesa.
“Okey. Nenda kafikirie, ni siku gani utakuja kwangu kisha utaniambia.”
“Sawa. Nitakwambia kwenye simu.” Nikamwambia haraka.
Nilikunywa bia moja tu, sikutaka kuongeza nyingine. Nilihisi mazungumzo yangu na yule mzungu yalikuwa yamefikia tamati. Baada ya kupata zile pesa sikutaka kuendelea kukaa tena pale. Nikamwammbia. “Mimi nakwenda zangu.”
“Hutaki kuongeza bia?” Dachi akaniuliza huku akitoa tabasamu laini. Tabasamu lake lilikuwa kama la kunicheka mimi nilivyotaharuki baada ya kunipa zile pesa.
“Basi imetosha. Mimi silewi sana. Nakunywa bia moja tu.”
Dachi hakusema kitu akabaki kunitazama huku akiendelea kutabasamu.
Nikainuka kwenye kiti na kuchukua mkoba wangu ambao niliutundika begani.
Dachi naye naye akainuka.
“Sikiliza nikuambie kitu,” akaniambia. Alinyamaza kidogo kisha akaendelea.
”Ukija kwangu nitakupa zawadi nzuri sana na hutaisahau maishani mwako.”
“Nimekusikia. Usijali Mr Dachi, tutakuwa pamoja. Kwa sasa acha niende kwanza. Lakini tutaongea mengi kwenye simu.”
“Sawa. Hakuna tatizo lakini nakuomba uzingatie niliyokwambia.”
“Nimeshayazingatia. Usijali.”
Nikaondoka. Dachi akarudi kwenye kiti na kuendelea kunywa pombe yake.
Nilikodi teksi iliyonirudisha nyumbani. Wakati wote nikiwa kwenye teksi hadi nafika nyumbani, yule mzungu alikuwa ametawala akili yangu.
Zile milioni kumi alizonipa pamoja na maelezo yake mengine yakiwemo yale aliyonieleza kuwa nikienda huko hotelini anakokaa atanipa zawadi ambayo sitaisahau maishani mwangu, yalikuwa yamenihamasisha.
Nilipofika nyumbani niliketi sebuleni na kufungua mkoba wangu nikaitoa ile bahasha yenye pesa. Niliziweka kwenye kochi kisha nikaanza kuzihesabu.
Zilikuwa ni noti 40 za Dola 100 kila moja (sawa na Sh10.3 milioni). Nikapanga kesho yake niende nikaziweke benki. Nikazirudisha pesa hizo kwenye mkoba kisha nikaendelea kumuwaza yule mzungu.
Niseme ukweli kuwa sikuwa nimewahi kushika shilingi milioni kumi mkononi mwangu tena zikiwa katika Dola Dola nyingi vile. Ile ilikuwa ni mara yangu ya kwanza.
Kwa pesa hizo na kwa ahadi nyingine alizoniahidi yule mzungu nikawa nimepata tamaa ya kuwa naye kwa kuamini kwamba angeweza kuyabadili maisha yangu.
Binafsi nilikuwa nikitamani kupata gari langu mwenyewe lakini sikujua ningeanzia wapi hadi niweze kulipata. Pia nilitaka kumiliki nyumba yangu niachane na nyumba za kupangisha lakini sikuwa na uwezo.