SIMULIZI YA HADITHI: Jana dume - 4

Muktasari:

  • Enjo alipompata mwanamme huyo alihisi kuwa alikuwa ameukata. Si muda mrefu akagundua ameingia choo sicho. Juhudi za kumkimbia zikagonga mwamba, kwani jamaa hakuwa mwanaume bali Janadume…!

ILIPOISHIA...
Nikahisi alikuwa mzungu mwenyeji kwani alikuwa akiifahamu vyema lugha ya Kiswahili.
“Bila samahani, niombe tu.” Nikamjibu.
“Lakini natanguliza samahani, sijui kama utaridhika.”
Aliponiambia hivyo nilishituka kidogo.
“Kwani unataka kuniomba nini?”


SASA ENDELEA...

“NAOMBA namba yako.”
“Namba yangu ya….?”
“Nilikuwa na maana namba yako ya simu.”
“Kama ni hilo tu hakuna tatizo.” Nikamwambia.
 Nikampa namba yangu. Nilimpa ili anipigie na kunieleza kile alichokuwa nacho moyoni mwake.
Nilipomtajia namba yangu aliiandika kwenye simu yake kisha akanipigia hapo hapo.
Simu yangu ilipoita aliniambia.
“Namba  yangu ndiyo hiyo, ahsante sana”
Hakurudi tena kwenye meza akatoka. Kwa vile mtu aliyefanya niamue kuondoka alishatangulia kutoka nikaona niendelee kukaa kidogo.
Nikawa namuwazi Yule mzungu aliyechukua namba yangu. Nilijiuliza alikuwa nani. Alikuwa ananifahamu au ndiyo tumekutana hapa hapa?
Baada ya kama nusu saa hivi nikainuka na kumfuata Flora na kumwambia twende zetu.
Flora hakunipinga tukatoka na kuchukua teksi tukarudi nyumbani.
Wakati niko kitandani, simu yangu ikaita. Nilipoichukua na kutazama kwenye sikrini ya simu niliona namba ya yule mzungu. Nikaipokea simu yake.
“Hello!” Nikasema kwenye simu.
“Hello! Mambo vipi?” Sauti ya yule mzungu ikasikika kwenye simu. Nilifurahi alivyoniuliza “Mambo vipi?” Niliona alikuwa mzungu aliyebobea katika lugha ya Kiswahili kiasi cha kutambua semi za mitaani.
“Poa.” Na mimi nikamjibu kwa kutumia lugha ile ile ya mitaani.
“Uko poa kabisa?” Akaniuliza.
“Mimi niko poa, sijui wewe?”
“Mimi pia niko poa. Umesharudi nyumbani?”
Mara moja nikagundua kuwa mzungu huyo alikuwa anataka kurefusha mazungumzo.
“Nimesharudi. Hapa niko kitandani.” Nikamjibu.
“Samahani sana. Mimi naitwa Mr Dachi, mimi ni Mjerumani ninayeishi huku Afrika.  Sijui mwenzangu unaitwa nani?”
“Naitwa Enjo”
“Okey. Jina lako zuri sana. Unaishi wapi?”
“Naishi Sinza.”
“Unafanya kazi?”
“Hapana. Kwa sasa niko nyumbani tu.”
“Okey. Mimi hupendelea sana kutembelea Afrika Mashariki. Huwa ninafikia kwenye mahoteli.”
“Nimefurahi kukufahamu.”
“Mimi pia nimefurahi kukufahamu na ninapenda uwe rafiki yangu.”
“Kuna aina nyingi za urafiki, wewe umependelea urafiki wa aina gani?”
“Urafiki wowote tu lakini tutazungumza zaidi tutakapokutana. Enjo una mchumba?”
“Sina mchumba.”
“Vizuri. Unadhani tunaweza kukutana wapi kwa ajili ya mazungumzo zaidi?”
“Sema wewe.”
“Mimi si mwenyeji sana hapa Dar.”
“Umefikia katika hoteli gani?”
“Hoteli ya Lux hapa Masaki. Niko chumba namba 35. Unaweza kufika?”
Mzungu huyo kanitajia hadi namba  ya chumba chake akidhani ningeweza kwenda kwake.
“Kwanini tusikutane mahali pengine?” Nikamuuliza.
“Tunaweza. Sasa sema wewe ni mahali gani?”
“Ngoja, kesho nitakupigia kukufahamisha.”
“Kesho saa ngapi?”
Nikafikiri kidogo kisha nikamjibu.
“Kesho mchana.”
“Ningefurahi zaidi kama utanitajia saa ili nisubiri simu yako.”
“Tuweke saa tano.”

“Sawa. Nipige mimi au utanipigia wewe?”
“Nitakupigia mimi.”
“Sawa. Nitasubiri simu yako saa tano.”
“Nashukuru. Usiku mwema.”
“Na kwako.”
Nikatangulia mimi kukata simu kisha nikaiweka kwenye kimeza cha mchagoni. Baadaye niliona niizime kabisa kwani sikupenda nikatishwe usingizi wangu kwa milio ya simu.
Usingizi haukuchelewa kunipitia, nikalala. Wakati niko usingizini nikaota niko kwenye ufukwe wa bahari mimi na yule mzungu tukikimbizana huku tukirushiana michanga. Sote wawli tulikuwa tumevaa mavazi hafifu ya kuogelea.
Mimi nilivaa chupi na sidiria yake na mzungu huyo alivaa chupi peke yake. Lakini rangi ya chupi yake na yangu zilikuwa zikifanana.
Baada ya kufukuzana na kuangushana kwa dakika kadhaa tuliingia kwenye maji na kuanza kuogelea kwa pamoja. Tuliogelea hadi tukafika maji mengi.
Mimi nilikuwa nyuma, yule mzungu alikuwa mbele yangu. Ghafla tukajikuta tuko katikati ya bahari. Ule ufukwe wa bahari hatukuuona tena.
Yule mzungu likuwa akiendelea kuogelea tu na mimi nikimfuatia nyuma. Ghafla nikaona tumetokea kwenye kisiwa kizuri kilichokuwa na minazi mingi ya kisasa.  Nikisemaminazi ya kisasa ninamaanisha ni ile minazi isiyo mirefu.
Tulipofika kwenye ufukwe wa kisiwa hicho tuliona jumba kubwa likiwa mbele yetu. Lilikuwa jumba zuri lililokuwa likimeremeta!
Yule mzungu akaniambia pale ndio nyumbani kwake. Akanikaribisha, tukaingia ndani.
Humo ndani tulitokea kwenye chumba kipana kilichokuwa na kitanda na kabati. Kitu ambacho kilinishangaza ni kuwa godoro la kitanda hicho pamoja na mto wake zilikuwa ni noti tupu!
Yule mzungu akajilaza kwenye lile godoro la noti. Mimi nikawa nazishangaa zile noti jinsi zilivyokuwa nyingi.
Nikashikwa na tamaa ya kutaka kuchukua zile noti. Hapo hapo nikaona kama kivuli cha mtu kwenye dirisha. Nilipotazama vizuri nikamuona marehemu mama yangu amesimama nje ya dirisha akinifanyia ishara nitoke mle chumbani.
Lakini alinifanyia ishara hiyo kwa siri na kwa hadhari ili yule mzungu asimuone.
Sasa mimi sikuelewa kwamba mama alinifanyia ishara ile ili nimkimbie yule mzungu au alitaka nitoke nionane naye kwa vile hatukuwa tumeonana kwa miaka mingi.
Kwa akili zangu nikachukulia kwamba mama alitaka nitoke nikasalimiane naye. Kwa vile duku duku la kumuona mama yangu lilikuwa limeshanishika nikageuka haraka ili nitoke mle chumbani.
Yule mzungu akamuona mama akichungulia kwenye dirisha, akauliza.
“Nani yule?”
Wakati anauliza hivyo alikuwa akishuka kwenye kitanda ili aende pale kwenye dirisha.
Na mimi nikapata nafasi ya kuchukua burungutu la noti kutoka kwenye godoro na kutoka nalo mbio. Huku nyuma nikasikia mzungu huyo akiniita.
“Wewe Enjo hebu rudi hapa!”
Ile sauti ya yule mzungu ndio iliyoniamsha usingizini. Nikafumbua macho. Kwa vile niliamka wakati natoka mbio nilijikuta nikihema huku moyo ukinienda mbio.
Mkono wangu wa kulia ulikuwa kama ulioshika lile birungutu nililokuwa nakimbia nalo. Nikahisi niliamka nikiwa na noti hizo mokononi. Kwa haraka nikayapeleka macho yangu kuutazama mkono wangu.
Sikuona chochote. Mkono huo ulikuwa mtupu!
Nikajiinua na kuketi kitandani huku nikijiuliza kwanini niliota ndoto ile.
Nikawasha taa ya mchagoni mwa kitanda nikatulia hapo kitandani na kuwaza.
“Kuna uwezekano mkubwa yule mzungu akawa ni tajiri, Ndio maana nimemuota amelalia godoro la noti.” Nikajiambia.
Niliendelea kujiambia kuwa kama nitashikamana naye anaweza kunitajirisha. Wazungu hawana tabia  ya ugumu wa pesa.
Asubuhi kulipokucha niliamkia kufua nguo zangu nilizozitumia kwa wiki ile. Nilipomaliza niliinjika chai. Kwa kawaida hupendelea kunywa chai ya rangi. Halafu hunywa maziwa peke yake.
Nilikuwa sipendelei kunywa chai ya maziwa. Baada ya chai kuwa tayari niliimimina kwenye chupa nikaenda kuoga. Baada ya kuoga na kuvaa nilikwenda mezani, nikapaka siagi slesi za mkate na kujinywea chai yangu.
Wakati nakunywa chai, simu yangu ikaita. Nilikuwa nimemsahau yule mzungu. Alipoona saa tano ilikuwa imefika alisubiri zipite dakika mbili ndipo akanipigia.
Nilipotazama simu, nikaona ni yeye aliyekuwa akinipigia. Ule msemo wa kuwa na ahadi ya kizungu ndipo nilipouthibitisha.
Kabla ya kuipokea simu hiyo nilijiuliza nitamwambia nini mzungu huyo kwa kutotimiza ahadi yangu ya kumpigia simu ikifika saa tano. Sikupata jibu. Nikaacha ile simu iite hadi ikakata yenyewe. Ndipo na mimi nikapiga.
Mzungu huyo akaipokea mara moja.
“Hello Enjo!” Akaniita.
“Hello Mr Dachi, mambo vipi?”
“Kama kawa kama dawa!” Mzungu akanijibu.
Nikaangua kicheko. Kilichonichekesha hasa si vile alivyotumia maneno hayo ya mitaani bali alikuwa akitamka maneno hayo  kwa lafudhi ya Kijerumani.
“Unacheka nini?” Akaniuliza.
“Nimefurahi kwa jinsi ulivyonijibu.”
“Nimekosea?”
 “Hapana, umepatia sana”
 “Nimeona kimya mpaka nimepiga mimi.”
“Ndiyo. Nilikuwa bafuni wakati unanipigia.” Nikatoa uongo.
“Nilifikiri umesahau.”
“Hapana, sikusahau. Nilikuwa nikupigie nikitoka bafuni.”
Mzungu huyo akanyamaza kimya kidogo. Pakapita ukimya wa sekunde kadhaa kabla ya sauti yake kusikika tena.
“Umeshafikiria tukutane wapi?” Akaniuliza.
Nikamtajia hoteli moja ya pale pale Sinza lakini ilikuwa mbali kidogo na nyumba ninayoishi.
“Unaweza kufika?” Nikamuuliza.
“Ninaweza.” akaniambia.
Akanyamaza kidogo kisha akaniuliza.
“Tukutane saa ngapi?”
“Kama saa kumi jioni hivi.”
Ningeweza kukutana naye wakati wowote lakini niliona nimtajie tu muda huo ili aone nilikuwa mtu wa mipango.