SIMULIZI YA HADITHI: Jana dume -3

Muktasari:

  • Enjo alipompata mwanamme huyo alihisi kuwa alikuwa ameukata. Si muda mrefu akagundua ameingia choo sicho. Juhudi za kumkimbia zikagonga mwamba, kwani jamaa hakuwa mwanaume bali Janadume…!

ILIPOISHIA...

JIONI tulipokuwa tunataka kutoka kazini Flora akampigia mwenye nyumba wake.
“Ningekuomba uje nyumbani jioni hii kama utaweza.”
“Una ishu muhimu?”
“Ni kuhusu nyumba. Kuna dada yangu anataka kupangisha ule upande wa pili.”
“Anayo kodi ya mwaka mzima.”
“Ndiyo anayo.”
“Kwa hiyo nije na mkataba wa pango?”
“Ikiwezekana njoo nao.”
“Sawa. Nitakuja saa kumi na mbili jioni. Si utakuwa umesharudi kutoka kazini?”
“Kazini ndio tunataka kutoka sasa hivi.”…! SASA ENDELEA...


“BASI nitakuja muda huo.”
“Utatukuta.”
Flora akakata simu na kuniambia.
“Sasa itabidi twende kule nyumbani tukamsubiri huyu mzee.”
“Amekwambia atakuja saa ngapi?”
“Saa kumi na mbili jioni.”
“Si uache nirudi nyumbani kwanza halafu nitakuja kabla ya saa kumi na mbili.”
“Si utakuwaunajizungusha burw Enjo kwani huko nyumbani una kazi gani?”
Nikafikiri kidogo kisha nikasema. “Okey,,,basi acha twende tu.”
Tulipotoka kazini ikabidi twende Sinza alikokuwa akiishi Flora. Yule mpangaji aliyekuwa upande wa pili wa Flora alikuwa ameshahama. Upande huo ulikuwa mtupu.
Tulisubiri hadi saa kumi na moja na nusu mwenye nyumba alipompigia simu Flora.
“Upo nyumbani?”
“Tupo tunakusubiri wewe.”
“Haya nakuja.”
“Usisahau huo mkataba wa pango.”
“Mkataba upo kwenye mkoba wangu.”
“Sawa.”
Saa kumi na mbili kasoro robo mzee mwenye nyumba akawasili. Alikuwa mtu mzima aliyekaribia umri wa miaka sitini. Flora alinitambulisha kwake. Mzee akanifungulia mlango wa upande uliokuwa unapangishwa tukaingia ndani.
Mzee alituonesha maeneo yote ya nyumba hiyo. Ilikuwa na vyumba viwili  vya kulala, kimoja kikiwa na choo cha ndani. Chumba cha sebule, jiko na stoo. Hakukuwa na marekebisho yoyote yaliyohitajika.
“Vipi mama, nyumba imekuridhisha?” Mzee akaniuliza baada ya kututembeza kwenye nyumba hiyo.
“Imeniridhisha.” Nikamjibu.
“Kodi yangu ni shilingi milioni mbili  na laki nne kwa mwaka. Maji na umeme unalipa mwenyewe.”
“Sawa.”
Tukarudi upande wa pili kwa Flora ambako Flora alimlipa kodi yake tukasaini mkataba wa pango. Nakala moja nikabaki nayo. Wakati huo ndipo Frank aliponipigia simu.
“Habari ya jioni?”
“Nzuri kaka. Uliniambia utanipigia ndiyo unanipigia?”
“Ndiyo nimepata nafasi ya kutulia. Unajua mpaka sasa bado niko ofisini.”
“Kumbe hujatoka ofisini?”
“Bado nipo. Uliniambia ulipata ule mzigo kutoka kwa Flora?”
“Ndiyo nilipata. Asante sana.”
“Na mmeshauwakilisha kwa mwenye nyumba?”
“Tuko naye hapa. Hapa niko nyumbani kwa Flora. Ameshamlipa mwenye nyumba pesa zake na tumeshaandikishiana mkataba wa pango.
“Ni kwamba wewe sasa ni mpangaji wa hapo nyumbani?”
“Tayari mimi ni mpangaji.”
“Sawa. Ukiwa na tatizo lolote usisite kuniambia. Hatukuanza kujuana leo Enjo.”
“Ni kweli kaka. Kukiwa na tatizo nitakwambia tu.”
“Basi acha niendelee na kazi. Tutaonana hapo kesho asubuhi.”
“Sawa. Jioni njema.”
“Na kwako pia.”
Frank akakata simu.
Nilianza kuingiza vitu kidogo dogo hapo nyumbani. Vingine nilitoka navyo nilikokuwa nikiishi na vingine vilitoka madukani. Baada ya mwezi mmoja tu nyumba yangu ikawa imechangamka.
Nilimshukuru sana Frank kwanza kwa kunitafutia kazi na pili kunilipia pango kwa mwaka mzima. Taratibu nilianza kugundua kuwa msaada wa Frank ulikuwa na lengo lilillojificha. Haukuwa wa bure kwani alikuwa akinifuatafuata sana hapo nyumbani.
Baadaye alinibainishia kwamba alikuwa akinitaka kimapenzi. Sikumkatalia na wala sikumkubalia. Sikumkatalia kwa sababu kutokana na wema alionifanyia kisingekuwa kitendo kizuri kumkatalia na sikumkubalia kwa sabbau kwa upande wangu sikuwa tayari kuwa naye kimapenzi. Nilikuwa nikimuona kama kaka.
Kwanza kile kitendo cha kunitaka mimi kilinishitua. Na aliniambia kwa kutumia nguvu za ziada. Tulikuwa tumekwenda kwenye hoteli moja kule kule Sinza akanunua ulevi mwingi. Siku hiyo alikunywa sana na mimi nikanywa sana.
Wakati tumelewa ndipo alipoanza kunisumbua kwa maneno na kunishika shika.
“Enjo hakika wewe ni mzuri sana…kama ningekuwa sijaoa ningekuoa wewe.”
“Asante.” Nilikuwa nikimjibu.
“Unajua Enjo ninakupenda sana. Naomba unipatie nafasi katika moyo wako.” Frank alikuwa akiendelea huku mkono wake ukiwa kwenye kiuno change nikauondoa.
“Frank, wewe ni kaka yangu. Inatupasa sasa turudi.”
“Subiri kwanza tuzungumze. Tunaweza kulala hata hapa hoteli.”
“Hapana. Kwanini ulale hoteli wakati una nyumba yako na wifi yuko nyumbani anakusubiri. Na mimi pia nina nyumba yangu. Kwanini tulale hoteli?”
“Sasa wewe unasemaje?”
“Kesho tutaongea vizuri zaidi.”
Tuliondoka hapo hoteli karibu saa nane usiku. Akanirudisha nyumbani huku akiendelea kunibembeleza na kuniahidi kunifanyia vitu vizuri zaidi. Kutoka siku ile nikajifunza kwamba sitatoka na Frank kwenda mahali popote pa starehe.
Na ndivyo nilivyofanya. Kila alipojaribu kuniambia twende sehemu nilikuwa nikimpa sababu za kumkatalia. Lakini Frank hakuchoka kunipigia simu na kunifuata nyumbani mpaka akawa ni kero kwangu. Mara kadhaa sikupokea simu zake na alipokuja nyumbani kwangu sikuwa na furaha naye.
Frank aliniandama kwa miaka miwili bila kukata tamaa. Na siku zote nilikuwa namdanganya.
Frank alipochoka akaanza kunichukia. Sikujua kilichokuwa kinaendelea upande wa pili lakini nilikuja kushitukia tu nikipewa barua ya kuachishwa kazi. Nikashukuru Mungu.
Nilikwenda kumueleza dada na kumuonesha ile barua ya kuachishwa kazi.
“Kwani kumetokea nini?”
“Sijui. Nimeona tu nikipewa hii barua leo.”
“Frank amekwambiaje?”
“Sijakutana naye na hajaniambia kitu.”
“Kwani uhusiano wenu ukoje siku hizi?”
“Kwa kweli uhusiano wetu si mzuri. Tangu alipoanza kunitaka amekosa subira, yaani hata salamu tunapeana mara moja moja sana. Tena si ile salamu ya kuchangamka.”
“Labda ni yeye aliyekufanyia fitina uachishwe kazi.”
“Kama aliweza kunifanya niajiriwe hawezi kushindwa kufanya niondolewe.”
“Kama angekuwa na nia njema angekwisha kupigia na kukueleza tatizo.”
“Yule ni kama kaka yangu. Kwa vyovyote nisingeweza kufanya naye chochote.”
“Utatafuta mahali pengine. Achana naye.”
Ili kuonesha kwamba Frank hakuwa na nia njema na mimi na alihusika mimi niachishwe kazi, hakunipigia simukunieleza chochote. Nikajua Frank alikuwa ndiye mbaya wangu.
Baada ya kumueleza Flora habari ya Frank alisikitika.
“Hakutumia uamuzi mzuri.” Akaniambia na kuongeza.
“Lakini mimi hajanieleza chochote.”
“Hawezi kukueleza hivyo lakini ameamua kunikomoa.”
“Kama milikuwa mnaishi kama dada na kaka mngeendelea hivyo tu.”
“Mwenzangu moyo wake ulibadilika akatokwa na utu akawa kama hayawani.”
“Pole shoga yangu.”
“Nimeshamuachia Mungu. Kama ni riziki nitaipata mahali pengine.”
Licha ya uhusiano wangu na Frank kwisha, uhusiano wangu na Flora uliendelea. Kwa vile tulikuwa tunaishi nyumba moja urafiki wetu haukukoma. Kulikuwa na siku ambayo alialikwa kwenye tafrija ya harusi ya mdogo wa rafiki yake. Kwa vile alikuwa peke yake akanichukua na mimi.
Tulifika katika tafrija hiyo saa mbili usiku. Na ilikuwa ikifanyika kwenye hoteli ya Mlimani iliyokuwa Kinondoni.
Tulikula na kunywa. Mwenzangu alikuwa mpenda muziki. Mara kwa mara alikuwa akiinuka kwenda kucheza. Katika meza tuliyokuwa tumekaa akaja mzungu mmoja naye akakaa. Labda aliamua kuja kukaa na mimi baada ya kuona nilikuwa nimekaa peke yangu.
Kama mwenyewe alivyokuwa mweupe alikuwa amevaa suti nyeupe. Ingawa kifungo cha shati alikifunga hadi cha mwisho hakuwa amefunga tai.
Ungeweza kudhani kwamba alikuwaja kukaa na mimi baada ya kuona nilikuwa peke yangu na pengine alitaka kusemeshana na mimi lakini jambo la ajabu ni kuwa alipokaa kwenye kiti alibaki kunitazama tu bila kunisemesha kitu chochote.
Nilikuwa nikitazama kando lakini nikimuona kwa jicho la pembeni jinsi alivyokuwa akinitazama. Nikajiuliza mtu huyu hanielewi au ananifananisha na mtu Fulani. Kama alikuwa akinifananisha kwanini alikuwa haniulizi? Jinsi alivyokuwa akinitazama nilikuwa nikiona aibu.
Kusema kweli alinikosesha raha. “Kama amenipenda angeniambia tu kuliko kunitazama vile.” Nikajiambia kimoyo moyo nikiwa nimekasirika.
Kwa vile muda ulikuwa umepita sana niliona bora nimfuate Flora nimwambie turudi nyumbani. Lakini kama aliyekuwa amesoma mawazo yangu mzungu huyo aliinuka haraka na kunifuata kabla sijapiga hatua.
“Samahani dada, kuna kitu nataka kukuomba.” Akanimabia kwa kiswahili fasaha.
Nikahisi alikuwa mzungu mwenyeji kwani alikuwa akiifahamu vyema lugha ya Kiswahili.
“Bila samahani, niombe tu.” Nikamjibu.
“Lakini natanguliza samahani, sijui kama utaridhika.”
Aliponiambia hivyo nilishituka kidogo.
“Kwani unataka kuniomba nini?”