HADITHI: Zindiko (sehemu ya 1)
Muktasari:
- Hii ni hadithi ya kusisimua yenye visa na mikasa ya kimaisha kutoka kwa mtunzi mahiri, Sultan Tamba. Twende naye...
SULTAN TAMBA
KIJIJI cha Mbwira, kilikuwa mbali na mjini. Inawezekana ndio sababu ya maendeleo yake kuchelewa ikilinganishwa na vijiji vingine vinavyopakana navyo ambayo sasa vimeshakuwa miji. kwa sababu hata wananchi waliokwenda kuishi au kufanya kazi huko, walikuwa wakisita kurudi mara kwa mara na kujenga nyumba zao na za wazazi wao, au kuanzisha hata biashara ndogondogo.
Kijuu juu, hiyo ndiyo unayoweza kuisemea kama sababu ya kwanza ya ufinyu wa kijiji chenyewe na mzunguko wa pesa kuwa mdogo. Na pengine ni sababu za kisiasa zaidi.
Lakini sababu ya msingi hasa siyo hiyo!
Ni kitu cha hatari.
Na hili lilikuwa wazi kwa sababu kijijini pale, palikuwa na mabango kadhaa yanayoonya kuhusu uwepo wa Joka la Zindiko.
Kuanzia machapisho ya karatasi hadi bango kubwa la barabarani.
Ni kwamba, kando kidogo ya kijiji hicho, kuna jengo la zamani, lisilokaliwa na mtu. Jengo hili, ndilo lililokuwa na zindiko. Zindiko la joka. Jengo lisilo na majirani. Lililotengwa na watu – likaachwa peke yake.
Mabango machache ya tahadhari yaliyobakia hapo kijijijini, yalikuwa yakiwaambia watu kwamba USISOGELEE JENGO HILI. KUNA JOKA LA ZINDIKO, LINAUA WATU.
Tangazo hilo, ndilo lililosababisha jengo hilo kuwa pweke, kujitenga na kuwa mbali na wananchi. Jengo liliogopwa. Historia ya miaka ishirini ya jengo hilo ilimtisha kila aliyesikia. Pia haikuwa hadithi za sungura na fisi, bali ilikuwa ni kitu cha kweli ambacho kipo na ushahidi kamili wa kila kilichotokea, likiwemo joka lenyewe.
Jengo hili chakavu na la miaka mingi, lilikuwa linalindwa kwa zindiko la Joka kubwa sana, refu na lenye nguvu ambalo lilikuwa linaishi kwenye mtungi ulioko mbele kwa upande mmoja wa jengo.
Watu walilipita mbali – mita kadhaa. Wengine hata kuliangalia hawakuangalia kwa sababu ya hofu na wasiwasi.
Kwa kipindi cha miaka 20, watu kadhaa walishapoteza maisha baada ya kujaribu kuingia ndani ya uzio mfupi wa jengo hilo.
Zama lilipomalizika kujengwa, jengo hili lilikuwa na mvuto wa aina yake, lilisisimua na kuwa jengo la kwanza la aina hiyo kijijini. Lakini wakati huo, lilikuwa lipo peke yake. Mwenye kiwanja chake, alituma watu wakafyeka msitu na kujenga jengo hilo. Kila aliyeliona, alikubali wazi kwamba lilikuwa ni jengo la thamani na fahari.
Lakini tangu zama hizo, hakujulikana mmiliki.
Uzio mfupi uliolizunguka, ulikuwa ni mpaka thabiti baina ya jengo hilo na watu wengine. Kiasi kwamba wote waliothubutu kuuvuka uzio huo, walivamiwa na kumezwa na joka hilo fasta. Joka ambalo licha ya nguvu na uwezo wake, lakini lilishangaza watu kutokana na urefu wake usio na mwisho. Kila lilipokuwa likitoka kwenye mtungi wake wenye mdomo mpana ambao ndio upana wa joka lenyewe, lilikuwa halimaziki na halijawahi kumalizika.
Kila lilipokuwa likitoka kwenye mtungi wake na kumshambulia mtu yoyote aliyevuka uzio wa jengo hilo, lilitoka kwenye mtungi kwa urefu wowote ule, ambapo baada ya kummeza mtu huyo, lilikuwa likirudi ndani ya mtungi – kinyumenyume kwa kasi sana.
Ni joka lililokuwa likilinda jengo hilo baada ya zindiko lililofanywa hapo kwa miaka mingi. Zindiko lililofanywa kwa nguvu ya jiwe jekundu. Jiwe adimu ambalo ni moja kati ya mawe matatu yaliyowahi kupigwa marufuku duniani.
Kwa miaka yote hiyo 20, hakuna mtu aliyefanikiwa kuvuka uzio huo na kunusurika. Wote walimezwa. Tena walimezwa kwa msemo wa ghafla! Yaani hata wenyewe wakiwa hawajaelewa, walishtukia joka limemfikia na kummeza. Kasoro mtu mmoja tu!
Mzee Zimataa.
Hata wakati huu ambapo alikuwa amefika kwenye jengo hilo, alikuwa amesimama akilitazama jengo hili.
Yeye ndiye binaadamu peke yake ambaye katika kipindi cha miaka 20 alikuwa akihudumu kwa kutunza mazingira na pia ni kuwa sehemu yake ya kupatia nguvu za dawa zake. Maana Zimataa, zaidi ya kuwa mhudumu mtiifu wa jengo hilo, pia ni mganga wa jadi mwenye nguvu na anayeaminika sana.
Zimataa alikuwa amesimama nje kidogo ya geti dogo la jengo la zamani lenye uzio mfupi na imara, mkononi akiwa amekumbatia mtungi mdogo, mtungi ambao ulikuwa na dawa alizokuwa amekuja kuzibariki kwenye mtungi wa Joka la Zindiko.
Zimataa aligeuka upande mmoja na kutazama bango lililo jirani naye lililoandikwa kwa maandishi makubwa: HATARI: USIVUKE UZIO KUINGIA KWENYE UWANJA WA JENGO HILI. NI ENEO LA KIFO.
Alitabasamu kimoyomoyo kwa sababu tangazo hilo yeye halikumhusu kwa sababu ni yeye pekee ambaye alikuwa na mhuri kwenye mkono wake unaomruhusu kuingia kwenye uzio huo na kufanya usafi wa mazingira na kutia nguvu dawa zake.
Yeye tu!
Ni yeye pekee kwa miaka 20.
Aliposimama hapo, alikuwa akilitazama jengo hilo lililochukua wastani wa robo ya maisha yake.
Tangu hapo alipokuwa mwanaume wa miaka 40 na sasa Mzee wa miaka 60 akiwa ni mhudumu wa jengo hilo – kazi ambayo alipewa bila hiyari. Alilazimishwa na alilazimika.
Lakini alikuwa amechoka. Maisha ya uhudumu wa pale, lawama kutoka kwa kila Mtendaji wa kijiji na viongozi wengine kuhusu nani hasa mmiliki wa jengo hilo ilimsumbua na sasa ilimchosha. Viongozi, wanakijiji na watu wengine walikuwa wakimwogopa kwa sababu mbili – kwanza ni uganga wake na pili walihisi ana siri zilizojificha kuhusu mmiliki na jengo zima.
Alisimama hapo akitazama jengo na kisha akaanza kutembea polepole akivuka geti na kuingia ndani yake.
Mita chache kutoka alipo Zimataa, Diwani wa eneo hilo, Mutwa Mamutwa na Mbunge Mheshimiwa Mizinga Tulo walikuwa wamesimama wakimtazama Zimataa.
Ilionekana kwamba walisimama mda mrefu kiasi na kwamba hata Zimataa alivyokwenda, ni kama walimtangulia na kumngoja afike. Pengine kutokana na ratiba ambayo imezoeleka, diwani huyu mpya mwenye ari na matazamio mapya alikuwa amemualika mbunge ajumuike naye katika kushuhudia kile ambacho alimsimulia.
Walikuwa wakimtazama tangu anafika na hadi anaanza kuingia kwenye uzio. Na sasa mbunge akatingisha kichwa kuonesha kuelewa kitu.
“Bila shaka yule ndiye Bw. Zimataa - mtu ambaye ulinambia ndiye pekee mwenye uwezo wa kuingia pale muda wowote bila kudhurika kwa miaka yote hii,” Mbunge alisema polepole.
Diwani alikubali kwa kutingisha kichwa na kukishusha.
‘Ndiyo Mheshimiwa. Nafikiri sasa unajionea mwenyewe. Yeye ni mtunza mazingira wa jengo hilo na pia ni mganga mwenye nguvu sana. Nakubalika na anaaminika sana. Sio mganga wasiwasi hata kidogo.
“Ni mganga ambaye hutumia mtungi wa Joka la Zindiko kuzipa nguvu dawa zake. Ndiyo maana hakuna ugonjwa au shida anayopelekewa inayomshinda.”
Mbunge akakubali! Akaonesha kuelewa kinachozungumzwa.
Zimataa akafika kwenye mtungi na kusimama kwa utulivu. Akauelekeza mtungi kwenye mdomo wa mtungi mkubwa kwa unyenyekevu.
“Kwa idhini yako Joka la Zindiko, na kwa nguvu za Jiwe jekundu zilizokuleta hapa, naleta dawa hizi za wagonjwa kumi na mbili waliokuja jana. Zipe nguvu dawa hizi, ziwe na nguvu ya uponyaji.”
Baada ya kusema hivyo, Zimataa akamwaga dawa ya mchanganyiko wa maji na majani kwenye mtungi ule.
Alipomaliza akarudi kinyumenyume hadi mbali kidogo, kisha akapiga magoti na kuinamisha kichwa chake chini.
Akatulia kidogo.
Kutoka kwenye mtungi, joka kubwa na refu, likatoka kwenye mtungi na kumfuata, likaanza kumzunguka.
Likamzunguka na kumzingira.
Kule aliko Mbunge aliliona tukio hilo akiwa amepigwa na ganzi ya fadhaa.
Katika historia ya maisha yake, hakuna siku ameshuhudia jambo la ajabu na la kutisha Zaidi ya hilo. Joka linaendelea kutoka mtungini bila kumalizika na kumzunguka Mzee Zimataa aliyetulia kimya.
Hili ndilo tukio ambalo lilikuwa limempa heshima kubwa kijiji kizima.
Kwamba lile joka ambalo limekuwa likiua kila anayekanyaga kwenye eneo hilo, Mzee Zimataa ni rafiki yake! Kwamba kila anapotaka, huenda kwenye mtungi na kufanya tambiko hilo dogo na kisha joka kutoka na kumzuka kama ishara ya kumsalimu.
Mzee Zimataa aliheshimika sana.
Mpaka kufikia hapo, kwa miaka yote hiyo, Mzee Zimataa amepitia mambo mengi makubwa kutoka kwa serikali na viongozi wengine waliokuwa wakitaka kuliondoa zindiko hilo au kulibomoa jumba lenyewe ili kukifanya kijiji kuwa salama.
Inaendelea kesho...