Hadithi
HADITHI: Bomu Mkononi - 25

Muktasari:
Binti mrembo cheupe ambaye ukimwangalia unaweza kusema ni Mwarabu ameolewa na wanaume wawili na sasa amekutana na boifrendi wake wa zamani ambaye walipanga kuoana kabla ya jamaa kutimkia Afrika Kusini...
ASUBUHI ya siku iliyofuata, Sele akanipigia simu kunijulisha kuwa alikuwa ameshaondoka.
“Haya, safari njema,” nikamwambia.
“Nikifika nitakufahamisha.”
“Poa.”
Jua lilikuwa limeshakuchwa aliponipigia tena simu na kuniambia kuwa alikuwa ameshafika Arusha.
“Marerani nitakwenda kesho asubuhi,” akaniambia.
“Ukifika huko utanijulisha mambo yakoje.”
“Sawa. Nitakujulisha.”
Siku iliyofuata mida ya saa nne hivi Sele akanipigia simu na kuniambia alikuwa ameshafika Marerani na kukutana na mwenzake.
Kutoka siku ile akawa ananipigia simu kila siku kwa siku tatu ambazo alikaa Marerani. Siku ya nne yake alirudi akaniambia kuwa alikuwa anashughulikia kuhamia katika ile nyumba aliyopangisha.
Zikapita siku mbili ndipo aliponipigia tena na kuniambia kuwa alikuwa ameshahamia katika nyumba hiyo. Siku hiyo ndiyo niliyokwenda kukutana naye. Nilikwenda katika ile hoteli tunapokutana akanichukua hadi katika hiyo nyumba.
Niliiona, ilikua nyumba nzuri yenye hadhi. Tuliingia ndani nikaona alikuwa amenunua fanicha za thamani na nyumba ilipendeza sana kwa ndani.
Sele akaniambia kuwa ile nyumba ilikuwa ni maandalizi ya harusi yetu kwani yeye akiwa Marerani ataniacha mimi pale nyumbani.
Nikakubaliana naye. Siku ile Sele alitaka nilale pale kwake lakini nilikataa kwa kusingizia kuwa shangazi alikuwa anaumwa. Nikaondoka jioni lakini nikiwa nimepata tamaa.
Mbali ya ile nyumba, kulikuwa na magari mawili ya Sele ambayo aliniambia yatawasili hivi karibuni, gari moja likiwa ni langu.
Unaweza kuona kuwa nilikuwa ninajipalia makaa ya moto kutaka kumiliki wanaume watatu kwa wakati mmoja lakini huwezi amini jinsi nilivyokuwa nikijiamini na sikuwa na wasiwasi kabisa.
Nilikuwa nimeshapanga niolewe na Sele na nikiona mambo yake yanakuwa mazuri nitakorofisha kwa waume zangu wa kwanza ili niachike, nibaki na Sele kwa vile nilikuwa nampenda sana na isitoshe angenipa gari.
Siku iliyofuata Mustafa akarudi ghafla. Sikufurahi nilipoona amerudi kwani nyendo zangu na Sele zingeharibika. Lakini kwa vile mara nyingi akitoka nyumbani asubuhi anarudi jioni au usiku, nikaona ningeweza kuwasiliana na Sele.
Siku ile ambayo Musatafa aliwasili, Sele alinipigia akataka tukutane lakini nikamwambia nisingeweza kuondoka nyumbani kwa vile shangazi amezidiwa.
Nilimjibu hivyo kwa sababu sikuwa na namna yoyote ya kuondoka pale nyumbani siku ile.
Siku iliyofuata Mustafa akaniambia anakwenda Bagamoyo kumsalimia mama yake. Alipoondoka na mimi nikaondoka kwenda kwa Sele.
“Nimekuja mara moja tu kwa vile jana umeniita. Unajua shangazi hana hali nzuri na si vizuri kumuacha peke yake kwa muda mrefu.” nikamdanganya Sele ili nisikae kwake sana.
Alichoniitia Sele ilikuwa ni kuzungumzia mipango ya harusi yetu. Nilimwambia wazazi wangu walikuwa wameshakufa na mtu wangu wa karibu alikuwa shangazi yangu ambaye ni mzee na mgonjwa.
“Sasa itakuwaje?” Sele akaniuliza.
“Lakini bado hakuna tatizo. Kama nilivyokwambia nilikwishaolewa na kuachika. Mimi sasa ni mtu mkubwa ninaweza kujiamulia mwenyewe mambo yangu bila kumhusisha shangazi. Ingawa ndugu wengine wapo lakini sina ulazima wa kuwahusisha. Tutaoana mimi na wewe tu.”
“Yaani kwa upande wako hakutakuwa na mtu yeyote?” Sele akaniuliza.
“Wewe unanitaka mimi au watu? Kama unanitaka mimi huna sababu ya kuhitaji watu. Mimi nishakubali tuoane.”
“Sawa.”
Nilipoona Sele alikuwa akiendelea kuwaza nilimwambia.
“Ukitaka nyingi nasaba, utapata mwingi msiba.”
Ilikuwa ni methali ya Kiswahili ambayo niliona niitumie kumuonya Sele aachane na habari ya kutaka kuhusisha watu wa upande wangu katika harusi yetu.
“Nina ndugu zangu huko Tanga lakini hao tuwaache kwanza kwa sababu wako mbali. Iko siku tutakwenda kuwajulisha kuwa tumeona,” nikamwambia.
Maneno yangu yakamuingia Sele, swali lake la mwisho aliniuliza.
“Mahari yako nitampa nani?”
“Utanipa mwenyewe, kumbe ulitaka kumpa nani?”
“Mara nyingi naona anapewa mzazi wako au kaka yako mkubwa.”
“Sasa mzazi wangu yuko wapi?”
“Umeniambia kwamba wazazi wako wameshakufa.”
“Kaka ninaye lakini si kaka yangu tumbo moja wala baba mmoja na yuko Tanga.”
“Kwa hiyo?”
“Sihitaji umpe hizo pesa, hakunilea. Na pia sihitaji kumuhusisha katika harusi yetu.”
“Mimi nakusikiliza wewe, unavyoniambia ndivyo nitakavyotekeleza.”
“Hapo umesema maneno ya maana. Sasa sikiliza nikwambie.”
“Enhe…”
“Utanipa mwenyewe mahari yangu. Mimi nataka mahari ya shilingi milioni mbili.”
Nikamnyooshea mkono Sele na kumkunjulia kiganja changu kama vile nilikuwa nataka kupokea hizo pesa.
Kitendo hicho kilimchekesha Sele.
“Ndio unataka hizo pesa?” Akaniuliza.
“Ndiyo.”
“Mbona una haraka, si ndio tunapanga?”
“Tumeshapanga na tumeshakubaliana, sasa ni utekelezaji tu,” nikamwambia Sele.
“Unadhani ni busara tukioana bila kushirikisha upande wenu?’ Sele akaniuliza.
Nilitafakari jibu, sikulipata. Sikuweza kumjibu kuwa ni busara kwa sababu nilijua fika kuwa si busara na pia sikuweza kumwambia si busara kwa sababu wazo hilo nililitoa mimi ili kuficha siri yangu kuwa nimeolewa mara mbili.
“Wasiwasi wako ni kitu gani?” Nikamuuliza baada ya kukosa jibu sahihi.
“Mimi sina wasiwasi wowote, nilikuuliza tu.”
“Tatizo lingekuwepo kama ningekuwa mwana mwari ambaye sijaolewa, idhini ya wazazi au wakubwa wangu ilikuwa inahitajika ili niolewe. Lakini mimi nimeshaolewa. Ninahesabiwa kuwa ni mtu mzima mwenye uamuzi wangu, isitoshe wazazi wangu ambao ni lazima wajue kuhusu ndoa yangu wameshafariki. Sasa sioni kama kuna tatizo kwa uamuzi huo.”
“Sawa, nimekuelewa.”
Sele aliponiambia hivyo alinyamaza kimya kwa muda kisha akaniuliza.
“Kitu muhimu ninachokiona kwa sasa ni kukubaliana kuwa sisi ni wachumba kutoka sasa. Hatuna utamaduni wa kuvalishana pete ila tunakuwa na makubaliano tu. Sasa baada ya hapo ndio ninalazimika kukulipia mahari yako. Umeniambia unataka shilingi milioni mbili?”
“Ndio nataka mahari ya shilingi milioni mbili,” nikamjibu. Uso wangu ulikuwa mkavu usio na chembe ya aibu.
“Kwa vile uamuzi ni wako wewe mwenyewe kwanini usiweke milioni moja?”
“Wewe unataka unipe shilingi milioni moja?’
“Ndio.”
“Unaweza kunipa hiyo milioni moja lakini milioni moja iliyobaki nitakudai.”
Sele akacheka.
“Kwanini usiisamehe kabisa?” Akaniuliza.
“Hapana, siwezi kusamehe kwa sababu ni haki yangu.”
“Sawa, nitaweka deni.”
“Sasa utanipa lini?”
“Kwa vile nahitaji tuoane kwa haraka nitakupatia kesho.”
“Halafu ndoa itakuwa lini?”
“Tutapanga siku baada ya kukupa nusu ya mahari yako.”
“Sawa. Basi mimi naenda zangu, sikai leo.”
Tukaagana na Sele, nikaondoka.
Nilifika Mbezi, Mustafa alikuwa hajarudi. Ili kujua kama anarudi nikampigia simu.
“Baba Rama vipi, unarudi?” Nikamuuliza alipopokea simu.
“Nimemkuta mama ni mgonjwa. Nilimpeleka hospitalini, ndio nataka kumuaga hivi nirudi.”
“Anaumwa nini?”
“Ni malaria tu.”
“Lakini ameshapata dawa?”
“Amepata dawa, anaendelea vizuri.”
“Mpe salamu zangu, mwambia nampa pole na namtakia kupona haraka.” Nilijifanya nina imani kweli, kumbe ni nyoka wa ndumba kuwili.
“Sawa, nitampa salamu zako.”
“Basi nakusubiri.”
“Sawa.”
Baada ya kuzungumza na Mustafa nikakata simu. Nilikuwa nimeketi sebuleni nikaanza kumuwaza Sele ambaye aliniahidi kuwa angenipa nusu ya mahari ya shilingi milioni moja kesho yake. Nilijiambia mara tu nitakapozitia mikononi shilingi milioni moja nitakwenda kuziweka benki niongeze akiba yangu ambayo ilikuwa imeshafikia shilingi milioni kumi na tisa. Nikiongeza shilingi milioni moja nitakuwa na shilingi milioni ishirini taslim.
Mawazo yangu pia yalikwenda kwenye gari ambalo Sele aliniahidi kuwa angenipa. Nikajiambia nikipata gari nitakuwa nimemshinda Amina na pia litarahisisha nyendo zangu.
Asubuhi ya siku iliyofuata mara tu Mustafa alipoondoka nyumbani nikampigia simu Sele.
“Unakuja?” Sele akaniuliza.
“Sijui kama nitaweza. Shangazi amezidiwa sana,” nikamdanganya.
“Sasa itakuwaje?”
“Lakini naweza kuja mara moja, sitakaa sana.”
“Basi uje, nimeshakwenda kuchukua pesa benki.”
“Okey, ninakuja.”
Nilikuwa chumbani nikavaa nguo za kutokea haraka haraka kisha nikatoka sebuleni.
Nilimuita mtumishi wetu nikampa shilingi elfu kumi.
“Chukua hii, utanunua soda. Mimi natoka kidogo lakini sitachelewa sana.”
“Baba akija nimwambieje?’
“Ndio nilikuwa nataka kukuagiza. Kama baba yake Rama atatokea mwambie nimekwenda kumsalimia jirani yangu anaumwa.”
“Jirani yupi?”
“Sasa wewe usimwambie jirani yupi, mwambie niko kwa jirani tu.
Inaendelea...