Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Bomu Mkononi - 24

Muktasari:

  • Binti mrembo cheupe ambaye ukimwangalia unaweza kusema ni Mwarabu ameolewa na wanaume wawili na sasa amekutana na boifrendi wake wa zamani ambaye walipanga kuoana kabla ya jamaa kutimkia Afrika Kusini...

TUKAINGIA katika lango la hoteli.

“Nilipokuwa Sauzi nilikuwa nikikuwaza sana,” akaniambia.

“Hata mimi nilikuwa nakuwaza,” nikamdanganya.

“Uliponiambia umeolewa kuna kitu kiligusa moyo wangu kwani dhamiri yangu ilikuwa ni kuja kufunga ndoa na wewe.”

“Lakini si nimeshaachana na yule mwanaume, una wasiwasi wa nini?”

Tukaketi katika ukumbi wa baa.

“Agiza chakula unachopenda,” akaniambia.

“Wewe je?”

“Mimi nimeshakula, nilikuwa nakunywa tu.”

Muhudumu alipokuja nilimuagiza biriani ya kuku.

Nikaendelea na mazungumzo na Sele. Chakula kilipoletwa nilikula peke yangu huku Sele akiendelea kunywa bia zake.

Akanieleza kuwa alipokuwa Sauzi alijihusisha na biashara ya unga ambayo ilimpa mafanikio makubwa.

“Mama yangu alinisihi sana niache biashara hiyo. Hivi sasa nimepanga niende Mererani,” akaniambia.

“Kufanya nini?” Nikamuuliza.

“Kutafuta machimbo.”

“Ahaa nimekuelewa. Unataka kwenda kuchimba madini?”

“Nimeambiwa kwamba yanalipa sana. Nitakuwa ninakwenda kuyauza nje ya nchi.”

“Ni kweli madini yanalipa. Vijana wengi hivi sasa wamejiingiza kwenye biashara ya madini na wamejenga majumba.”

“Na mimi nitajenga.”

“Ukifanya bidii utajenga tu.”

“Napenda kuwa karibu na watu wanaonitia moyo kama wewe.”

“Sasa unategemea kwenda lini huko Marerani?”

“Siku chache tu zijazo. Nina mwenzangu tayari yuko huko. Mambo yakiwa tayari ataniarifu.”

“Ninaamini kuwa mambo yatakuwa mazuri.”

“Yakiwa mazuri na kwa upande wako pia yatakuwa mazuri kwa vile nitakuwa na wewe.”

“Hakuna tatizo.”

Sele alinipa moyo sana. Nilitamani nikorofishe kule nilikoolewa ili niachike nibaki na Sele. Lakini sikuwa na mbinu yoyote kwani wanaume wote walikuwa wakinijali ila upendo tu ulikuwa umebadilika na kuwa kwa Sele.

Siku ile kwa sababu ya furaha ya kuwa na kijana huyo nililewa sana. Kwa vile Sele alishaniambia kuwa tutalala pale hotelini sikuwa na  wasiwasi. Nilijua tukitoka pale tunaingia chumbani. Hakuna atakayeniona na kupeleka umbeya kwa Musa.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa. Tulipotosheka na bia tuliingia chumbani. Si unajua inakuwaje kwa wapenzi wawili waliopotezana kwa miaka mingi wanapokuja kukutana tena. Yalikuwa mahaba niue, mpaka asubuhi!

******

Kulipokucha ndipo nilipomkumbuka Musa. Simu yangu niliizima tangu ile jana. Nikavizia Sele alipokwenda kuoga nikaiwasha na kumpigia Musa.

“Nilikupigia jana usiku hukupatikana,” Musa akaniambia.

“Simu iliisha chaji, si unajua haya masimu ya siku hizi hayakai na chaji,” nikamdanganya.

Musa akaliacha suala hilo la simu akaniuliza.

“Shangazi anaendeleaje?”

“Hajambo kidogo.”

“Anaweza kuzungumza?’

“Anazungumza hivyo hivyo kwa taabu.”

“Na chakula anakula?”

“Anakula. Hivi asubuhi nimemtayarishia uji mwingi, ameunywa wote.”

“Naamini kuwa atapata nafuu.”

“Uzee pia unachangia kumdhaifisha. Shangazi yangu ana umri mkubwa sana.”

“Sasa utarudi lini?”

“Bado bado nipo kwanza.”

“Haa Mishi! Usifanye hivyo. Si unajua mimi ni mtu wa safari?”

“Kwani utaondoka lini?”

“Safari zangu hazina kanuni, wakati wowote ninaweza kuambiwa niende Burundi.”

“Basi acha nilale leo, kesho ninaweza kuja.”

“Sawa, nisalimie shangazi.”

Kumbe Sele alikuwa ametoka bafuni wakati nazungumza na Musa. Nilishitukia tu akiwa nyuma yangu. Kwa vile nilishamalizana na Musa nikakata simu.

“Ulikuwa unazungumza na nani?” Sele akaniuliza.

Moyo wangu ulishituka Sele aliponiuliza hivyo.

Itakuwa amesikia mazungumzo yetu, nikajiambia.

“Nilikuwa nazungumza na rafiki yangu,” nikamwambia.

“Nilisikia ukimwambia utalala leo, kesho utakwenda. Utakwenda wapi?”

“Kumbe amenisikia!” Nikajiambia.

“Ni rafiki yangu tu anataka niende kwake. Ndio nimemwambia nitakwenda kesho.”

Nilipomjibu hivyo Sele hakusema kitu. Wakati anashughulika kuvaa nikaizima simu.

Siku ile pia nilishinda pale hoteli. Tulipokunywa chai ile asubuhi Sele aliondoka akaniacha hapo hapo hoteli, nikarudia kulala. Saa saba akarudi tukala chakula kisha tukaenda kulala sote hadi saa kumi jioni.

Tulipoamka tulikwenda kuoga, tukarudi chumbani kupiga stori hadi usiku tuliposhuka chini.

Tulikwenda kutembea kidogo kunyoosha miguu. Baadaye tulirudi kula chakula. Baada ya hapo tuliingia chumbani.

Siku iliyofuata ndipo nilipoondoka kurudi nyumbani kwangu Kimara.

Niliuondoka asubuhi nikaenda kukaa kwa shangazi hadi saa sita, ndipo nilipokwenda Kimara. Kabla ya kuondoka pale hotelini, Sele alinipa shilingi laki tatu, nikazitia kwenye mkoba wangu. Hakukuwa na kitu kingine kilichokuwa kikisumbua akili yangu zaidi ya pesa.

Kama kulikuwa na mtu aliyehitaji kuniiba angefanikiwa kwa kutumia pesa. Mbele ya pesa nilikuwa sina akili kabisa. Sababu ya kuwataka wanaume wote watatu ni tamaa ya pesa.

Wakati nikiwa kwenye teksi nikielekea Kimara, Musa akanipigia simu. Jinsi alivyokuwa na wahka hakuwahi hata kunisalimia, aliniuliza.

“Unakuja?”

“Nimeshafika, niko njiani,” nikamjibu.

“Umeshafika wapi?”

“Hapa Dar.”

“Sasa uko njiani wapi?”

“Niko njiani nakuja huko nyumbani.”

“Ahaa…poa. Vipi shangazi anaendelea vizuri?” Moyo wake sasa ulikuwa umetulia, amemkumbuka shangazi.

“Una nini leo, mbona sikuelewi?” Nikamuuliza.

“Kwanini?’

“Unapiga simu hata hutaki kusalimiana na mwenzako, unauliza habari ya safari…!”

“Si ndio nakuuliza, shangazi anaendeleaje?”

“Ni baada ya kukwambia kuwa nimeshafika Dar. Ningekwambia sijaondoka usingemkumbuka shangazi.”

“Ah unajua nimekuuliza hivyo kwa sababu kuna dereva mwenzetu amefariki dunia leo. Alikuwa aondoke kesho kwenda Zambia, sasa ile safari yake nimepewa mimi. Yaani hapa kesho naondoka kwenda Zambia ndio maana nilikuuliza hivyo.”

“Haya. Usiwe na wasiwasi. Zambia utakwenda tu. Mimi nimeshafika na shangazi yako hajambo.”

“Poa, nakusubiri.”

“Uko nyumbani?”

“Ndio niko nyumbani lakini Ramadhani yuko kwa bibi yake.”

“Sawa.”

Nilipofika Kimara nikamwambia Musa anipe hela ya teksi. Aliponipa nililipa kisha nikampiga uongo wa mwaka kwamba shangazi hana mtu wa kumhudumia hivyo ninatakiwa niende Tanga mara kwa mara hadi atakapopona.

Uongo wangu huo haukumfurahisha lakini alinyamaza kimya.

“Sasa kama nilivyokwambia kesho naondoka, na naondoka alfajiri.”

“Uende ukamchukue mwanangu.”

“Nitakwenda kumchukua. Tangu jana ananiuliza mama atarudi lini, namwambia sijui.”

“Basi nenda ukamchukue sasa hivi.”

Musa akatoka kwenda kwa mama yake ambako alikuwa amempeleka Ramadhani, mtoto wetu baada ya mimi kutokuwepo nyumbani.

Siku iliyofuata Musa akaondoka alfajiri kwenda Zambia, siku hiyo hiyo nikaondoka kwenda Mbezi. Mustafa alikuwa bado hajarudi. Nyumba ilikuwa imebaki na mfanyakazi wetu.

Nilikaa kule siku tatu. Sele alikuwa akinipigia simu mara kwa mara. Ile siku ya tatu akaniambia nifike tena kule hotalini tulikokuwa siku ile. Akaniambia alikuwa na habari muhimu.

Nafasi nilikuwa nayo ya kutosha. Nikamuacha mtoto kwa mfanyakazi wetu nikaenda Ilala.

Nilipofika pale hotelini nilimkuta Sele akaniambia kwamba kesho yake anaondoka kwenda Mererani.

“Kumbe unaondoka kesho!” Nikamuuliza.

“Mwenzangu amenipigia simu leo asubuhi ameniambia niende.”

“Ameshapata sehemu?”

“Ameniambia kuwa amepata.”

“Sasa unataka twende pamoja?”

“Kama unataka twende, hakuna tatizo.”

“Nimekutania tu, kwa sasa siwezi kuondoka. Shangazi yangu anaumwa.”

“Lakini nikifika nitakuwa nakupigia simu kukujulisha kinachoendelea.”

“Kwani wewe mpaka sasa unaishi wapi?’

“Niko nyumbani kwetu lakini nimeshapata nyumba ya kupangisha, nikirudi Marerani ninahamia.”

“Poa. Ratiba yako ya leo ikoje?”

“Ratiba ya nini?”

“Umechukua chumba hapa hotelini?”

“Sijachukua, nilikuwa nakusubiri uje.”

“Chukua chumba lakini sitalala, inabidi baadaye niondoke. Shangazi yangu anaumwa na mimi ndiye ninayemhudumia.”

“Kwani shangazi yako yuko wapi?”

“Nimemuhamishia Kimara kwa baba mdogo.”

“Kumbe hayuko pale nyumbani?”

“Tulimuhamisha muda mrefu.”

Baada ya hapo Sele alikodi chumba tukahamia chumbani. Aliagiza bia tukaletewa na kuanza kunywa.

Ilipofika saa moja usiku Sele alikuwa amelewa chakari. Mimi sikuwa nimelewa sana kwa sababu nilikuwa nakunywa kwa kutegea ili nisilewe kwa vile nilipanga nirudi Mbezi.

Kila nilivyojitahidi niondoke mapema nilishindwa, niliondoka saa nne usiku. Teksi ikanipeleka Mbezi. Sele nikamuacha pale pale hotelini. Siku ile nayo alinipa shilingi laki mbili.

Inaendelea...