Hadithi
HADITHI: Bomu Mkononi - 17
Muktasari:
- Pakapita ukimya mfupi. Mustafa alikuwa ametulia akiwaza. Mimi nilikuwa nikimtazama huku mawazo ya ndoa ya pili ikipita kwenye akili yangu. Nilikuwa nimeshaamua kuoana naye. Nilijua ulikuwa ni utapeli lakini niliamini kuwa usingefahamika.
NIKAWA najiuliza kama kweli Mustafa amedhamiria kunioa mimi, hiyo posa yangu ataipeleka kwa nani? Kama ni kwa shangazi yangu, si atakwenda kushangaa kuona mke wa mtu anatolewa posa nyingine?
Shangazi ataniuliza imekuwaje napeleka watu wanitolee posa wakati nikijijua ni mke wa mtu? Umbea wangu utaishia hapo. Mustafa akijua kuwa nilikuwa namtapeli ataniacha siku hiyo hiyo.
Kwa hiyo nifanye nini? Nikajiuliza.
Nikapata jibu kwamba nimwambie Mustafa kuwa mimi sikuwa na wazazi, baba yangu na mama yangu walikuwa wameshakufa. Nilikuwa naishi mwenyewe tu.
Na akiniuliza kuhusu ndugu yangu yeyote, nimwambie kuwa nilizaliwa peke yangu, sina ndugu.
Baada ya kupanga uongo huo nikabaki nao kichwani mwangu hadi siku ambayo Mustafa alilirudia tena lile suala.
“Nataka nijitokeze kwenu niwajue wazazi wako,” aliniambia
“Ndio unataka kupeleka hiyo posa?” Nikamuuliza.
“Ndio lengo langu.”
“Sasa ngoja nikwambie kitu, mimi sina wazazi. Sikuwahi kukwambia jambo hilo.”
“Kwanini huna wazazi?” Akaniuliza kwa mshangao.
“Wazazi wangu walishakufa zamani.”
“Sasa unaishi na nani?”
“Ninaishi mwenyewe tu.”
“Pole sana. Lakini hilo si tatizo, ndugu wengine si wapo?”
“Mimi sina ndugu, nilizaliwa peke yangu.”
“Kweli?”
“Kweli kabisa.”
“Hata ndugu wa mbali pia huna?”
Nikaona nikisema sina ataona mimi ni muongo. Nikatafuta la kumjibu.
“Ndugu wa mbali hawakosekani lakini ndugu ni wale mnaopatilizana. Hao ndugu zangu hatupatilizani. Kila mmoja ana lake. Sina shida nao.”
“Ni kweli, kama ndugu hampatilizani si ndugu tena.”
“Mimi naendesha mambo yangu mwenyewe, sishirikishi ndugu kwa sababu nimeshajihisabu sina ndugu.”
“Sawa. Sasa tutafanyaje?”
“Tunaweza kuoana wenyewe tu.”
“Mahari yako nimpe nani?”
“Nipe mwenyewe. Unataka umpe nani wakati nimeshakwambia sina ndugu? Kwanza mahari kwetu Waislamu ni halali ya mke, wazazi au walii wa mke kazi yao huwa ni kuipokea tu na kuikabidhi kwa mke.”
“Hilo nalifahamu,” akasema Mustafa.
“Kama unalifahamu ni vyema. Kama mpokeaji hayupo utanipa mwenyewe hiyo mahari,” nikamweleza ili kumtoa kwenye reli asiendelee kuulizia kuhusu japo walii wa kuipokea mahari hiyo.
“Kwa hiyo mipango ya harusi tutaipanga mimi na wewe tu?”
“Au wewe hupendi iwe hivyo?”
“Kama hapana budi tutafanya hivyo.”
“Kwanza itakuwa nafuu kwako, tunapanga ndoa yetu tunaoana wenyewe kwa utashi wetu vile ambavyo tunataka.”
Mustafa alifikiri kidogo kisha akaniuliza
“Ungependa nikutolee mahari ya kiasi gani?”
“Shilingi milioni tatu,” nikamjibu haraka
“Nitakupa nusu kwanza.”
“Nataka zote.”
“Nitakupa milioni moja na nusu halafu nitakuja kupa milioni moja na nusu nyingine.”
“Kwani ukinipa zote kabisa itakuwaje?’
“Ni makubaliano yetu. Kaka yangu alioa mke alilipa mahari nusu. Baada ya ndoa akamalizia.”
“Sasa na wewe unataka umuige kaka yako?”
“Si kumuiga, ni mipango tu Mishi. Kukupa milioni tatu kwa sasa nitaharibu mambo mengine.”
“Kwani utanipa lini hiyo nusu na hiyo nusu nyingine utanimalizia lini?”
“Naweza kukupa hata kesho, nusu nyingine nitakupa baada ya kuoana.”
“Wewe unataka tuoane lini?”
“Kwa vile tunajipangia wenyewe nataka tuoane haraka iwezeknavyo.”
Nikafikiri kidogo kisha nikamwambia.
“Unaonaje tukioana kwa siri, yaani sitaki hata Amina ajue.”
“Amina anakuhusu wewe, mimi hanihusu.”
“Anakuhusu kupitia kwa Shabir.”
“Kumbe sijakueleza kuwa mimi na Shabir kwa sasa hatuko pamoja Tulishatengana na ninahisi ni fitina zilitoka kwa Amina.”
“Sema kweli?”
“Nakwambia ukweli. Mimi naendelea na biashara zangu.”
“Lakini si unaweza kumualika.”
“Nani…mimi? No! Kwanza urafiki wenyewe haupo. Alinishutumu mbele ya Amina kuwa namuibia pesa zake. Ana pesa gani za kunitambia mimi…?”
“Sasa huyo Amina alimtia fitina gani?” Nikamuuliza.
“Ninahisi tu kwamba anaweza kuwa anamtia maneno kutugombanisha kwani tangu alipoanzana naye ndio Shabir akaanza kuwa na maneno madogo madogo.”
“Kwani utaratibu wenu wa biashara ulikuwaje?”
“Shabir anapenda pesa lakini ni mvivu wa kazi. Yeye ametoa mtaji lakini ninayefanya kazi ni mimi. Mimi ndiye ninayetafuta oda kwa wafanyabiashara halafu ninakwenda kununua bidhaa zinazotakiwa aidha Dubai au China, wakati mwingine Japan au India.”
“Unapoleta hizo bidhaa mgawano wenu unakuwaje?”
“Siri ya hii biashara ninaijua mimi, wateja wetu wote niliwatafuta mimi na wananijua mimi. Shabir kazi yake ni kuuliza faida. Wakati mwingine dola inakuwa juu, faida yetu inakuwa ndogo. Inapofikia hapo anasema nimemuibia.”
“Sasa kama ni hivyo endelea na biashara mwenyewe.”
“Ndio najipanga. Shabir nimeshamrudishia pesa zake zote, hanidai kitu. Nataka nianze kazi na pesa zangu mwenyewe. Ni mtovu wa shukurani lakini mimi ndiye niliyemtajirisha.”
“Sasa umemtajirisha mwenzako, wewe je?”
“Ninajua mwenyewe, kila mtu na akili yake. Nitafanya biashara mwenyewe, uwezo ninao.”
“Utaenda wapi?”
“Nimepanga niende Dubai.”
“Lini?’
“Baada ya kuoana na wewe. Ndio maana nataka tuoane haraka.”
Pakapita ukimya mfupi. Mustafa alikuwa ametulia akiwaza. Mimi nilikuwa nikimtazama huku mawazo ya ndoa ya pili ikipita kwenye akili yangu. Nilikuwa nimeshaamua kuoana naye. Nilijua ulikuwa ni utapeli lakini niliamini kuwa usingefahamika.
Baada ya kimya hicho kilichodumu kwa sekunde chache nikamwambia Mustafa. “Sasa sikiliza, utakaponipa hiyo nusu ya mahari yangu ndio tutaweza kupanga harusi yetu itakavyokuwa. Kwa vile itakuwa ndoa ya haraka haraka nataka isiwe na sherehe, iwe kimya kimya tu. Sherehe zitafuatia utakapotulia. Unaonaje?”
“Sawa. Itabidi katikati ya wiki hii nikakutambulishe kwetu.”
“Wapi?”
“Bagamoyo. Baba yangu alishakufa lakini mama yangu yupo ingawa ni mzee sana.”
“Basi nitatafuta siku twende, kwani kuna ulazima wa kulala huko?”
“Tunaweza kwenda na kurudi.”
“Mimi nataka twende asubuhi turudi jioni.”
“Sawa.”
Siku ile tuliyozungumza maneno hayo, siku ya pili yake Musa akawasili kutoka Congo DRC ambako alikuwa amepeleka mzigo. Kuondoka kwake kulinipa nafasi ya kutosha ya kuwa na Mustafa.
Aliporudi nikazima simu yangu ili Mustafa asije akanipigia. Usiku wa siku ile aliyorudi nikamuweka kikao Musa.
“Unajua kwamba unaposafiri unaniacha peke yangu?” Nikamuuliza.
“Sasa nitafanyaje mke wangu?’
“Lakini unajua kuwa mimi ni mwanamke?’
“Ninajua ndio.”
“Na unajua kwamba unaposafiri wakati mwingine unakaa mwezi mzima?’
“Ndio ninajua. Kwani unataka kuniambia nini?’
“Nataka kukwambia kwamba, mimi ninaogopa kuishi pake yangu unapoondoka. Naona usalama wangu ni mdogo sana nikiwa hapa.”
“Sasa tufanyeje?”
“Ninataka uajiri mlinzi. Nikilala ndani, nje kuwe na mlinzi.”
“Ni wazo zuri, nitatafuta mlinzi.”
“Tena nataka wale walinzi wa makampuni ya ulinzi. Anakuja jioni anaondoka asubuhi. Mchana hakuna tatizo.”
“Sawa. Nitafanya mpango huo.”
“Yaani ikiwezekana umpate huyo mlinzi kabla hujasafiri.”
“Sawa.”
“Utasafiri lini?”
“Sijajua bado.”
“Utajua lini?”
“Ni mpaka niambiwe na tajiri.”
“Safari zenu hazieleweki, kesho tu unaweza kuambiwa kuna safari. Kwa hiyo ni vizuri uwahi kwenda kwenye hizo kampuni za ulinzi. Vile ukiondoka ujue mlinzi ameshapatikana.”
“Sawa.”
Siku ya pili yake Musa alikwenda kufuatilia suala la mlinzi. Akanipigia simu na kunijulisha kuwa ameshapeleka maombi ya kuletewa mlinzi.
“Atakuja lini kuanza kazi?’ Nikamuuliza.
“Atakuja kesho.”
“Sawa.”
Nilimtaka mlinzi huyo kwa akili yangu kwani nilishapanga kuhamia nyumbani kwa Mustafa pindi mume wangu awapo safarini, hivyo nilitaka nyumba yetu iwe inalindwa usiku ili wezi wasije wakatuibia.
Siku iliyofuata mlinzi akaja nyumbani. Musa alikwenda ofisini kwao akamchukua na kuja kumuonyesha nyumba. Nilionana naye tukasalimiana.
Musa akamwambia kwamba mimi ndiye mama mwenye nyumba na kwamba atakuwa anawasiliana na mimi. Nikachukua namba yake na yeye akachukua yangu.
“Tuna utaratibu wa kubadilishwa mara kwa mara lakini itakapokuwa hivyo nitakujulisha,” mlinzi huyo akaniambia.
“Hakuna tatizo,” nikamjibu.
Kutoka siku ile nyumba yetu ikawa na mlinzi. Alikuwa anakuja saa kumi na mbili jioni na kuondoka saa moja asubuhi. Anapokuja ananijulisha na anapoondoka asubuhi pia ananipa taarifa.
Inaendelea...