Dili iliyokufa -29
ILIPOISHIA
Baada ya daktari kumsikiliza, Wakwetu alianza utaratibu huo. Daktari aliwachukua Wakwetu na Majaliwa kwenye chumba chake cha maabara na kuchukua damu ya Majaliwa. Majaliwa baada ya kutolewa damu, Wakwetu alimpa pesa ya nauli akamwambia arudi nyumbani.
Majaliwa akiwa ameshangazwa na kitendo hicho alitoka na kwenda kupanda daladala. Hakujua ni kwa nini Wakwetu alitaka achukuliwe damu wakati hajamwambia kuwa anaumwa.
Baada ya Majaliwa kuondoka, Wakwetu naye alichukuliwa damu. Damu ya Wakwetu na damu ya Majaliwa ilikwenda kufanyiwa vipimo. Wakwetu aliambiwa asubiri katika sehemu ya kusubiri majibu.
Baada ya kusubiri kwa karibu saa nzima, Wakwetu aliletewa bahasha iliyokuwa na majibu. Aliifungua pale pale na kuisoma. Majibu yalionyesha kuwa damu yake na damu ya Majaliwa zilikuwa zimekataana, jambo lililoonesha kuwa Majaliwa hakuwa mtoto wa Wakwetu..
SASA ENDELEA...
MATOKEO hayo yalimfanya Wakwetu ashushe pumzi ndefu kama mtu aliyekuwa ametua mzigo mzito kichwani mwake.
“Nilitarajia kuwa itakuwa hivi” alijisemea peke yake na kuongeza.
“Yule mtoto si wangu na tabia zake pia hazioneshi kuwa ni mtoto wangu”
Alimfuata tena daktari na kumwambia.
“Nimeona matokeo. Yule mtoto si wangu. Sasa nitaleta watoto wengine wawili nao nataka uchukue vipimo vyao kwanza kujua kama wao ni ndugu na pia kujua kama ni wanangu”
“Hakuna tatizo”
“Sampuli yangu ya damu uitunze, sitapenda kutolewa tena damu”
“Sawa. Sampuli yako ya damu tutaendelea kuwa nayo”
Wakwetu akatoka. Alikwenda moja kwa moja hotelini walikokuwa James na Masumbuko. Kwanza walikunywa chai ya asubuhi kisha akaondoka nao. Aliendesha mwenyewe hadi kule hospitali.
Walipofika aliwakabidhi James na Masumbuko kwa daktari. Walichukua damu zao na kuambiwa wasubiri kwenye sehemu ya kusubiri majibu.
“Tunachunguzwa kitu gani?” Masumbuko akamuuliza Wakwetu.
“Kwanza nataka nipate uhakika kama nyinyi ni ndugu kweli halafu kuna kitu kingine atatuambia daktari” Wakwetu aliwambia.
Baada ya kusubiri kwa karibu saa nzima daktari aliwafuata.
Safari hii hakumpa bahasha kwanza isipokuwa alimuuliza.
“Kwanini ulitaka kuhakikisha kuhusu hawa vijana kuanzia yule wa kwanza na hawa?”
“Kuna sababu za kihistoria. Nataka nipate matokeo halafu nitakueleza”
“Hawa wenyewe ni ndugu na ni watoto wako” Daktari alimwambia na kuongeza. “Majibu yako haya hapa”
Alimpa ile bahasha.Wakwetu kwa vile alishaambiwa matokeo hayo hakuifungua ile bahasha kwa haraka.
“Kama una muda kaa nikueleze”
Daktari akakaa.
***********
Mara tu Majaliwa alipofika nyumbani kwa Wakwetu Sharifa alimuuliza.
“Mmekwenda wapi na baba yako?”
“Alinipeleka hospitali kunitoa damu” Majaliwa alimjibu huku akiketi. Alionekana mnyonge sana.
Sharifa alikuwa ameshituka.
“Ulimtolea nani damu?’
“Sikumtolea mtu damu bali nilichukuliwa damu kidogo tu kama ya kipimo”
“Kipimo cha nini?”
Majaliwa akabetua mabega.
“Sijui”
“Halafu ulipochukuliwa damu uliambiwa nini”
“Baba alinipa nauli akaniambia nirudi”
“Yeye mwenyewe yuko wapi?”
“Nimemuacha huko huko”
“Umemuacha na James?”
“Hapana. James tulimuacha kwenye hotelini, ndio tukenda huko hospitali”
Sharifa akanyamaza kimya kwa muda akiwaza.
“Sasa amekwenda kukuchunguza nini?” Sharifa akamuuliza Majaliwa hatimaye.
“Sijui. Hakuniambia kitu”
“Tangu juzi huyu mzee simuelewi. Nadhani kuna kitu alichokigundua, si bure. Lakini kama kuna kitu hatanyamaza siku zote, atakisema tu”
“Amegundua kama mimi si mtoto wake?”
“Ndio hapo hatujui, mpaka atakapokuja kutuambia mwenyewe”
“Kama amegundua hivyo si angekwisha tuambia. Kwanza nani atamwambia?”
“Utajuaje. Tanga hii, umbea mwingi….”
Baada ya hapo wote wakawa kimya.
****************
Wakwetu alimueleza daktari pamoja na vijana hao historia ya maisha yake alivyoondoka kwenda Afrika kusini na kumuacha mke wake Zainab akiwa mjamzito.
Aliendelea kueleza matatizo yaliyomtokea alipokuwa Afrika Kusini. Maelezo yaliendelea hadi alipoanza kufanikiwa akiwa mfanya kazi wa kwenye meli.
Akaeleza kwamba alirudi Afrika kutoka Ulaya akiwa mtu mzima baada ya kuondoka akiwa kijana mdogo. Akaeleza usumbufu alioupata kumtafuta mke wake ambapo alielezwa kuwa mke wake alifariki dunia na kwamba alikuwa amezaa watoto pacha waliokuwa wakilelewa na bibi wa marehemu mke wake.
Akaeleza kwamba aliambiwa bibi mwenyewe pia alikwishakufa na watoto walikuwa wamechukuliwa na mwanamke mmoja wa kiarabu ambaye naye aliondoka kurudi kwao Uarabuni lakini haikujulikana wale watoto aliwaacha wapi
Wakwetu aliendelea kueleza kwamba wakati amekata tamaa ya kuwapata watoto wake alioa mke kwa tamaa ya kupata mtoto anagalau mmoja lakini akaja kutokea kijana mmoja aliyedai kuwa yeye ni mtoto wake.
Alieleza kwamba kijana huyo ambaye ni Majaliwa alijitokeza baada ya kulisoma tangazo la Wakwetu alilolitoa kwenye gazeti kuwatafuta watoto wake. Aliendelea kueleza kuwa alimlea kijana huyo kama mwanawe mpaka siku za karibuni ambapo tabia yake ilianza kumtia mashaka.
Pia Wakwetu alilieleza lile tukio lililosababisha ajuane na Masumbuko na hatimaye kugundua kuwa dereva wake ni ndugu na Masumbuko…
Palitokea mshangao na mshituko mkubwa si tu kwa daktari aliyekuwa akimsikiliza, bali pia kwa James na Masumbuko baada ya Wakwetu kuueleza mkasa huo mwanzo hadi mwisho ambapo anagundua kuwa Majaliwa si mwanawe bali wanawe ni Masumbuko na James.
“Umetueleza mkasa mzito sana!” Daktari alimwambia Wakwetu na kumuuliza.
“Sasa huyo kijana mwingine aliyejitokeza na kudai wewe ni baba yake ni nani?”
“Ndiye yule uliyempima damu kwanza na ikagundulika kuwa si mwanangu”
“Swali langu lilikuwa ni kujua alitokea wapi?’
Wakwetu alibetua mabega yake.
“Sijui na kinachonishangaza ni kuwa alinitajia asili yake ikalingana na hii inayowahusu wanangu, ikabidi nimuamini”
“Nenda kamuulize vizuri…” Daktari alimwambia kisha akanyanyuka na kuondoka.
Wakwetu akawatazama James na Masumbuko.
“Wanangu leo mmempata baba yenu!” akawambia.
Nyuso za Masumbuko na James zilikuwa zimetota kwa machozi.
“Isiwe siku ya huzuni kwenu, nataka iwe siku ya furaha” Wakwetu aliendelea kuwambia.
James alinyanyuka akaenda kumkumbatia baba yake kisha Masumbuko naye akafuatia.
“Leo tunamshukuru Mungu kujaalia tukio kama hili” Masumbuko alisema na kuongeza.
“Ulinitembelea hospitali, ulinihudumia kumbe vile ni damu yako”
“Na mimi uliniajiri kama dereva wako na ulinitendea wema ambao sitausahau na nikakuhishimu, kumbe vile ni baba yangu! Mungu ashukuriwe!”
Maneno ya wanawe yalimtoa machozi Wakwetu akajifuta kwa kitambaa cha mkononi kisha akawambia.
“Twendeni nyumbani”
Walitoka nje ya hospitali wakajipakia kwenye gari, safari hii aliendesha James. Ilikuwa siku ya furaha kwao wote lakini ilikuwa siku ya maswali makali kwa James na masumbuko.
“Kwanini baba ulimtekeleza mama mpaka akafa?” Masumbuko aliuliza.
“Sikumtekeleza bali ni misukumo ya kimaisha. Katika safari yangu ya kutafuta maisha nilikutana na matatizo mengi ikiwemo kufungwa” Wakwetu alijitetea.
“Lakini ulimuacha mama na mimba yetu ilikupasa uwasiliane naye kujua hali yake” James akaongeza.
“Wakati ule hakukuwa na mawasiliano ya simu za mikononi kama ilivyo siku hizi. Ingekuwa vigumu kuwasiliana naye. Vinginevyo ingebidi niache kazi nirudi na kama ningerudi isingesaidia kwa sababu kulichoniondoa Tanzania ni kutafuta kazi”
“Sijui amezikwa wapi mama yetu?” James akauliza kama aliyekuwa akijiuliza mwenyewe lakini Wakwetu alimjibu.
“Tutafanya utafiti tutakuja kugundua”
Walipofika nyumbani kwa Wakwetu, Wakwetu aliwakaribisha wanawe ndani. Alimkuta Majaliwa amekaa na mama yake sebuleni.
Uso wa Majaliwa ulionyesha wazi kugutuka alipomuona Masumbuko.
Kumbukumbu zikaanza kumjia alivyokwenda kumpiga risasi….
Masumbuko alikuwa ndio amefika Tanga kutoka Lusaka. Lengo lake lilikuwa ni kwenda katika kituo cha yatima alikotokea kabla ya kuchukuliwa na mzungu aliyekwenda naye Zambia.
Kwa kufika katika kituo hicho Masumbuko alihisi angeweza kuipata familia yake. Dereva wa teksi aliyokodi alikuwa ni Sadiki mdogo wake Sharifa ambaye aliwahi kuelezwa na Sharifa kuhusu kumbambikia mtoto mume wake.