Dili iliyokufa - 31
ILIPOISHIA
Maisha hayakuwa mabaya. Mashaka alikuwa meneja wa kampuni binafsi. Alikuwa akiishi katika nyumba ya kampuni.
Mtu wa kwanza kufahamina naye katika mtaa uliokuwa na nyumba yetu ni Mwanaisha, mke wa jamaa mmoja aliyekuwa jirani yetu. Mwanaisha akaja kuwa rafiki yangu mkubwa.
SASA ENDELEA...
Mimi naamini katika kubadilika kwa tabia ya binaadamu. Tulipoanza maisha na mume wangu, alikuwa akinijali na kunisikiliza sana. Alikuwa anapotoka kazini hatoki nyumbani, na kama atatoka, tutatoka wote. Ikitokea ametoka peke yake, haifiki saa tatu anakuwa amesharudi.
Isitoshe, nikimuomba pesa anakuwa si mgumu wa kutoa na anakuwa hana maswali mengi. Lakini ghafla alianza kubadilika. Alikuwa hatoki na mimi mara kwa mara, na anapotoka, kurudi kwake ni saa sita usiku.
Kwa upande wa pesa, alianza kunibania. Ukimuomba pesa anakuwa na maswali chungu nzima. Huenda akupe au asikupe, na akikupa ni nusu ya ile uliyoitaka.
Mimi na jirani yangu Mwanaisha tulikuwa tukielezana siri zetu. Vile nilivyomuona mwenzangu anazidi kunawiri, nikahisi kwamba mume wake alikuwa akimjali.
“Mwenzangu, naona mambo yako si mabaya,” siku moja nilimwambia hivyo. Alikuwa amekuja nyumbani kunitembelea.
“Kwanini, shoga?” akaniuliza.
“Muonekano wako tu unaonesha, tuache mbali mavazi.”
“Mmh... shoga! Unataka uniambie mambo yako wewe ni mabaya?”
“Mabaya, shoga,” nikamwambia kwa unyonge.
“Kwanini?”
“Zamani mume wangu alikuwa akinijali sana lakini siku hizi... mmh!...”
“Hakujali?”
“Hanijali kabisa.”
“Kwanini asikujali mke wake?”
Nikabetua mabega yangu kwa huzuni.
“Sijui, mwaya.”
“Kusema kweli, mume wangu ananijali sana na kwa hilo nashukuru Mungu.”
“Sijui huyu wangu amepata mwanamke mwingine...?”
“Hawa wanaume vijana hawaaminiki, inatakiwa umchunguze. Inawezekana kuna mwenzako anayemjali. Wanawake wa mji huu wanataka waume za watu tu. Wakiona watu wanapendana wanataka kuharibu.”
Maneno ya Mwanaisha yakanitisha. Nikaduwaa kimya.
“Mimi wangu nilimshitukia muda mrefu nikamdhibiti. Sasa hivi ameshika adabu,” Mwanaisha akaniambia.
“Umemdhibiti vipi?”
“Nimemdhibiti kwa dawa... hivi hivi maisha hayaendi, shoga yangu...”
“Niambie na mimi, nifanyeje?”
“Huyu mwanaume wangu alikuwa mgumu sana wa pesa. Pesa anapata, lakini ukimuomba anakuwa na maneno mengi. Nikahisi labda ana mwanamke anayemharibu akili yake, nikamuendea kwa mganga.
Nilimlisha madawa mpaka amekaa sawa. Sasa ninachotaka nakipata. Zile safari za ovyo ovyo hana tena.”
“Sasa nipeleke na mimi kwa huyo mganga.”
“Kwa hilo tu usijali. Wewe tafuta siku, nitakupeleka.”
“Kama atakuwa sawa kama zamani nitashukuru, shoga, kwa maana anaitesa akili yangu. Nimemuomba laki moja tu, sasa ni mwezi wa pili kila siku napewa ahadi. Lakini zamani anakupa hata laki mbili. Amebadilika hivi sasa.”
“Wala usijali, shoga, atakuwa sawa. Utakuja kuniambia.”
Mwanaisha akanitia tamaa.
Baada ya mazungumzo yetu ya siku ile, tulikaa kama wiki moja hivi, Mwanaisha akaja nyumbani na kuniambia kama niko tayari anipeleke kwa huyo mganga.
Kwa vile mume wangu alikuwa amekwenda kazini na asingerudi hadi saa kumi jioni, nikamwambia Mwanaisha tunaweza kwenda. Nikajiandaa. Nilipokuwa tayari, tukatoka.
“Ni wapi?” nikamuuliza.
“Ni Mwang’ombe. Itabidi tupande daladala.”
Mwang’ombe ni kitongoji kilichoko nje kidogo ya jiji la Tanga, kikiwa pembezoni mwa barabara inayoelekea wilaya ya Pangani.
“Kwa hiyo tunakwenda stendi ya mabasi?”
“Ndiyo, twende stendi tukapande daladala.”
“Sawa.”
Tukaenda zetu stendi.
Tulipofika, tukapanda daladala inayokwenda Mwahako. Daladala ikatushusha Mwang’ombe na kuendelea na safari.
Tukaanza mwendo wa miguu. Tulitembea mwendo wa kama nusu kilometa hivi tukatokea katika hiyo nyumba ya mganga.
Lilikuwa ni banda la uani lililokuwa na vyumba sita. Mbele ya banda hilo kulikuwa na nyumba ambayo ilikuwa haijakamilika kujengwa. Tofali zilikuwa zinapandishwa sasa.
Tulipofika, tulikuta wanawake wawili wakitwanga mahindi na wengine wawili wakiwa na shughuli nyingine.
Wanawake hao wakatukaribisha. Mwanaisha, aliyeonekana kuwa mwenyeji, akawambia kuwa tulikuwa tunahitaji kumuona mganga.
“Mganga yuko ndani, karibuni,” mwanamke mmoja akatuambia.
Mwanaisha alikuwa akikijua chumba cha mganga. Akaniambia:
“Twende.”
Tukaenda. Kilikuwa chumba cha mwisho kwenye lile banda. Mlango wa chumba hicho ulikuwa wazi. Tulipofika kwenye mlango huo, tulimuona mtu mmoja amekaa kwenye jamvi akikatakata vipande vya mizizi.
“Hodi,” Mwanaisha akamshitua.
Mtu huyo, aliyeonekana kuwa ndiye mganga mwenyewe, akainua uso na kututazama.
Alikuwa amevaa upande wa kaniki aliokuwa amejifunga kiunoni. Kifua chake kilikuwa wazi.
“Karibuni wageni,” akatuambia huku akitabasamu.
Tukaingia katika kile chumba. Mwenzangu ndiye aliyetangulia. Kama kilivyo chumba cha mganga yeyote, hakikuwa na kiti bali kulitandikwa jamvi.
Mganga mwenyewe alikuwa amekaa kando ya ukuta wa upande mmoja, mbele yake kukiwa na kimeza kidogo ambacho upande mmoja kulikuwa na vitabu na vichupa vichupa. Upande mwingine kuliwekwa rundo la mizizi aliyokuwa akiikata vipande vipande.
Tulipoingia tulimsalimia. Alipotuitikia, Mwanaisha akaniambia:
“Tukae.”
Tukakaa kwenye lile jamvi.
“Kama nakukumbuka. Sura yako si ngeni machoni mwangu,” mganga huyo akamwambia Mwanaisha.
“Ni kweli. Nafikiri umenisahau tu kwa vile wateja wanaokuja kwako ni wengi.”
“Ulishawahi kuja hapa kwangu?”
“Mara nyingi tu, lakini ilikuwa mwaka jana.”
“Ni kweli. Hivi sasa kumbukumbu zinanijia vizuri. Ni kweli uliwahi kuja. Habari za siku nyingi?”
“Nzuri tu, sijui za kwako.”
“Sisi tupo. Tunaendelea na kazi. Ulikuwa hapa hapa mjini au ulitoka kidogo?”
“Nilikuwa sipo. Nimerudi hivi juzi tu.”
Hapo Mwanaisha alidanganya. Sidhani kama aliwahi kusafiri katika kipindi hicho cha mwaka mmoja. Siku zote tulikuwa tupo pamoja.
Mganga akaniitazama mara moja kisha akamuuliza Mwanaisha:
“Mna shida gani?”
“Mwenye shida ni huyu mwenzangu...”
Mganga huyo akanitazama mimi.
“Karibu mama,” akaniambia, kisha akamtazama tena Mwanaisha.
“Ni nani wako?” akamuuliza.
“Ni jirani yangu, halafu ni rafiki yangu.”
“Ndiyo. Haya mama, nieleze shida yako,” mganga akaniambia.
“Shida yangu ni matatizo ya mume wangu...”
“Mume wako ana matatizo gani?”
“Simuelewi siku hizi. Zamani tulikuwa tunaishi vizuri. Alikuwa akinisikiliza sana na kunijali, lakini siku hizi hanithamini, hanipi pesa, anarudi usiku mwingi na haonekani kunijali kama zamani. Sasa sijui amepatwa na nini?”
“Subiri nitakwambia,” mganga akaniambia.
Alisimama akachomoa moja ya tunguri miongoni mwa tunguri kadhaa alizokuwa amezitundika kwenye ukuta. Akakaa chini na kuiweka ile tunguri mbele yake.
“Mume wako anaitwa nani?” akaniuliza.
“Anaitwa Mashaka,” nikamjibu.
“Kituta, tueleze Mashaka ana matatizo gani, kwanini hamjali mke wake?” mganga akauliza huku akichungulia kwenye mdomo wa ile tunguri.
Wakati anachungulia aligutuka kidogo akasema:
“Mashaka ameshakuja, ninamuona hapa.”
Na mimi nikashituka na kumuuliza:
“Ameshakuja?”
“Yuko kwenye tunguri yangu. Hii inaitwa Kituta. Inanasa kama umeme,” akaniambia, kisha akacheka peke yake kuisifia ile tunguri.
Akaendelea kuchungulia kisha akatuambia:
“Pembeni mwake kuna msichana mweupe amemlalia kwenye bega....”
Niliposikia hivyo nilishtuka na kuuliza:
“Huyo msichana ni nani?”
“Huyu ndiye anayeharibu akili ya mume wako. Pesa zote zinakwenda kwa msichana huyu!”
Maneno yale yaliingia katika moyo wangu kama umeme wa radi. Hapo hapo nikajiona nimefadhaika na kupatwa na hasira.
“Nikichungulia naweza kumuona?” nikamuuliza yule mganga.
“Huwezi kumuona. Macho yako si ya kiganga.”
“Yukoje?”
“Ni mweupe, mrefu kidogo, na si mnene wala mwembamba. Mwili wake ni wa kati na kati.”
Umbile lililoelezwa lilizidi kuniiumiza.
“Yaani ni mzuri sana kuliko mimi?” nikamuuliza mganga huyo.
“Kila mtu ana uzuri wake. Yeye ana uzuri wake na wewe una uzuri wako.”
“Sasa kwanini anamjali huyo na kunidharau mimi?”
“Ni mapenzi tu yamezidi kwa mwenzako.”
“Sasa nataka umuondoshe huyo msichana, halafu unifanyie dawa huyu mwanaume anipende mimi peke yangu, yaani kila nitakachomwambia anisikilize mimi.”