Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dili iliyokufa -19

HADITHI 19 Pict

ILIPOISHIA

“Una kisa gani na yule kijana?”

“Kijana huyo sijawahi kumuona”

“Kesho asubuhi tutafanya gwaride la utambulisho. Wale watumishi wa gesti waliokuona watakuja kukutambua hapa na kesho hiyo hiyo tutakufkisha mahakamani”

“Mimi nasubiri hilo gwaride. Naamini watasema si mimi”

Inspekta Amour akamwambia polisi aliyekuwa amesimama kando ya meza.

SASA ENDELEA...


“Mrudishe ndani.”

James akachukuliwa na polisi huyo na kurudishwa rumande.

Kwa siku mbili alizokaa mahabusi, James alishaanza kuonja adha ya kukaa mahabusi. Kila kitu kilikuwa taabu. Kukaa kulikuwa taabu. Kulala taabu. Kula taabu, na maisha yalikuwa taabu.

Alishuhudia chumba hicho cha mahabusi kikiingizwa watu wa aina mbalimbali; vichaa, wavuta unga, walevi na wahuni. Kilikuwa kama chumba cha watu wasio na heshima.

Wakati mwingine kelele zilizidi. Kulikuwa na watu waliokuwa wakizungumza na wenzao, wengine walikuwa wakizungumza peke yao. Baya zaidi, kulikuwa na wengine waliokuwa wakipiga kelele wakiamrisha polisi wawatoe.

Mara kwa mara polisi walikuwa wanakwenda kuwaonya waache kelele.

Wakati hayo yakijiri, James alikuwa na mawazo yake. Alikumbuka kwamba alitakiwa na bosi wake kujitokeza polisi kwa ajili ya kumuokoa mwanawe aliyegonga mtu, lakini sasa anakutana na kesi nyingine ya kumpiga mtu risasi ambayo haitambui.

Binafsi, hakuamini kuwa Majaliwa angeweza kumpiga mtu risasi japokuwa alikuwa mkorofi. Alichokuwa akiamini yeye ni kuwa tukio hilo lilifanywa na mtu mwingine mwenye gari kama la Wakwetu, hivyo polisi walipoliona gari la Wakwetu wakajua ndiye aliyempiga mtu risasi.

Kwa sababu ya kumheshimu bosi wake, James hakuwa amebadili mawazo yake. Alidhani kuwa kama ataendelea kukana kosa hilo, polisi wangemuachia.

Pia alipata matumaini ya kuachiwa kutokana na gwaride la utambulisho aliloambiwa lingefanyika kesho yake asubuhi. Alijua kuwa watu watakaotakiwa wamtambue wataeleza kuwa hakuwa yeye aliyempiga mtu risasi.

Siku ile nayo ikapita.

Asubuhi ya siku iliyofuata Wakwetu alimuaga Sharifa.

“Mimi naenda huko polisi kushuhudia hilo gwaride la utambulisho.”

“Kama hao watu watasema James siye aliyempiga mtu risasi, watamuachia?” Sharifa akamuuliza.

“Watamuachia, lakini atabaki na kesi ya kugonga mtu ambayo adhabu yake ni faini.”

“Baada ya hapo nini kitafuatia?”

“Watamtafuta Majaliwa.”

“Watampata wapi? Majaliwa ameshakimbia.”

“Akikamatwa kwa bahati mbaya na akitambuliwa, atafunguliwa kesi.”

“Bila ushahidi?”

“Ushahidi ni wa wale waliomwona. Kwanza mimi sitaki arudi tena hapa nyumbani. Ninachofikiria ni ile bastola yangu ambayo bado anayo. Kama atakamatwa nayo, itakuwa kesi nyingine.”

Baada ya mazungumzo hayo, Wakwetu alikwenda kukodi teksi iliyompeleka katika kituo hicho cha polisi.

Gari lake lilikuwa bado linashikiliwa na polisi. Wakati huo Inspekta Amour alikuwa amekwenda Mabawa kuwachukua watu ambao walitakiwa wamtambue James.

Alipofika huko alifanikiwa kumpata mtu mmoja tu, Hashim Seki, ambaye siku mbili zilizopita alimpa maelezo Inspekta Amour kuwa alimwona mtuhumiwa alipofika pale gesti.

Kwa vile Hashim alishapewa taarifa siku moja kabla kwamba kutafanyika gwaride la utambulisho ambapo yeye angetakiwa kwenda kumtambua mtuhumiwa, alikuwa ameshajiandaa. Inspekta Amour alipofika alimchukua kwa gari la Idara ya Upelelezi na kwenda naye.

Gwaride hilo la utambulisho lilifanyika saa tatu asubuhi kwenye eneo la ndani la kituo. Wakwetu alishuhudia zoezi zima lilivyofanyika.

Walisimamishwa watuhumiwa kumi kutoka mahabusi, akiwemo James. Walifanyishwa gwaride na polisi mmoja wa kituo hicho huku Hashim na Inspekta Amour wakiangalia.

Baada ya gwaride hilo, watuhumiwa hao waliambiwa wabaki wima wakiwa katika mstari mmoja. James aliwekwa katikati.

Hashim akaambiwa na Inspekta Amour aende akamtambue mtu ambaye alifika pale gesti na kumpiga risasi mteja wao.

Hashim aliwatazama watuhumiwa hao na kuonekana kusitasita.

“Sogea karibu uwaone vizuri,” Amour alimwambia.

“Simuoni hapa.”

“Sogea karibu uwatazame vizuri.”

Hashim alisogea karibu na watuhumiwa hao.

“Ni yupi?” Amour akamuuliza.

“Naona hapa hayupo.”

“Muangalie mtuhumiwa mmoja mmoja kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho, utamwona tu.”

Hashim akaanza kumtazama mtuhumiwa mmoja mmoja kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho.

Akatikisa kichwa.

“Hapa hayupo,” akasema tena.

“Au umemsahau?”

“Namkumbuka vizuri sana. Siwezi kumsahau. Ni kwamba hapa hayupo.”

“Mtuhumiwa tuliyemkamata yuko hapo.”

“Hapa?”

“Angalia tena vizuri.”

Hashim alirudia tena kuwatazama mmoja mmoja.

Alipofika kwa James alimpita akaendelea mbele hadi kwa mtuhumiwa wa mwisho.

“Nimewatazama vizuri. Hapa hayupo.”

Amour aliposikia hivyo alimwambia mtuhumiwa aliyewekwa kwanza apige hatua tatu mbele. Mtuhumiwa huyo alifanya hivyo.

Amour akamwambia James naye apige hatua tatu mbele.

“Watazame hao watuhumiwa waliotokea mbele halafu utuambie,” Amour akamwambia Hashim.

“Nimewatazama lakini hapa pia hayupo.”

Inspekta Amour alimsogelea mtuhumiwa wa kwanza na kumshika bega.

“Huyu siye?” akamuuliza Hashim.

“Siye.”

Alimfuata James, naye alimshika bega.

“Na huyu je?”

“Huyo pia siye.”

“Yukoje huyo uliyemwona wewe?”

“Ni mweusi halafu si mrefu sana na si mfupi. Mwili wake umenawiri sana.”

“Unasema kweli?” Amour akamuuliza kwa sauti iliyopoteza nguvu.

“Kweli kabisa.”

“Ina maana mtuhumiwa tuliyemkamata siye kabisa?”

“Siye.”

“Lakini lile gari unalikumbuka vizuri?”

“Gari ninalikumbuka.”

“Hebu twende nje ukatuonyeshe kama unalikumbuka.”

Amour alitoka nje ya kituo na Hashim. Akamwonyesha gari la Wakwetu lililokuwa limeegeshwa pembeni.

“Gari ndiyo hilo hilo,” Hashim alisema.

“Umezitambua namba zake za usajili?”

“Namba sikuweza kuziona zote. Niliona za mwanzo, lakini gari ni hili hili.”

“Nani aliziona zote?”

“Kusema kweli hakuna aliyewahi kuzikariri zote.”

“Magari hufanana, namba za usajili ndizo hazifanani.”

“Lakini gari ni hili hili.”

“Haitoshi kuthibitisha. Kama mngekariri namba, ingekuwa bora sana.”

Mkuu wa kituo hicho ambaye alikuwa karibu na Inspekta Amour alimwambia Amour:

“Itakuwa vigumu kumfikisha mahakamani mtuhumiwa kwa kesi hii. Ushahidi tuliokuwa tukiutegemea ni wa Hashim.”

“Itabidi tusitishe kumpeleka mahakamani. Shahidi mwenyewe anamkana mtuhumiwa na namba za gari hakuzikariri vizuri.”

“James atakuwa amefananishwa. Kwanza mtu mwenyewe haonyeshi kuwa na wasifu wa kijambazi.”

“Tutamfikisha mahakamani kwa kosa la kugonga mtu.”

“Unajua Inspekta, hatujui majeruhi mwenyewe yuko vipi!”

“Tatizo ni kuwa hatukufuatilia tangu mwanzo, sisi tulishughulika na kesi hii ya kujaribu kuua.”

“Sasa itabidi tufuatilie tujue kama majeruhi bado yuko hospitalini au kama ameshatoka.”

“Leo nitakwenda hospitalini kumuulizia. Alilazwa Hospitali ya Ngamiani.”

“Sawa.”

Baada ya zoezi la kumtambua James kutofanikiwa, saa chache baadaye Wakwetu alifanikiwa kumwekea dhamana James na kupewa gari lake.

Walitakiwa wafike tena hapo kituoni asubuhi ya siku inayofuata. Wakwetu akampakia James na kuondoka naye.

“Sasa baba, ina maana hawa polisi wamelifananisha hili gari?” James alimuuliza Wakwetu wakati wanarudi Sinza.

“Itakuwa wamelifananisha. Mwanangu hawezi kumpiga mtu risasi. Kwanza ataipata wapi hiyo bastola?”

“Wametupotezea muda sana. Wamenilaza ndani bure. Nimekaa siku mbili lakini naona kama nimekaa mwaka mzima.”

“Pole sana. Mimi nilipotaka ujitokeze wewe, sikujua kama yatatokea yote hayo. Imekuwa kama bahati mbaya, lakini nakupongeza kwa ujasiri wako na uvumilivu.”

Maneno ya Wakwetu yalimfariji James akashusha pumzi.

“Sasa itabaki kesi ya kugonga mtu,” alisema.

“Kesi za trafiki ni za faini. Nitalipa kiasi chochote kitakachotakiwa. Usiwe na wasiwasi. Ila mtu aliyegongwa hajulikani yuko wapi.”

“Kwanini?”

“Polisi walishughulika zaidi na kesi hii ya kujeruhi kwa risasi, wakaipuuza ile. Leo ndiyo wameikumbuka lakini hawana hakika mtu aliyegongwa bado yuko hospitalini au amesharuhusiwa.”

“Vyovyote itakavyokuwa, sina wasiwasi na kesi za trafiki.”