Bomu mkononi - Sehemu ya 9
Muktasari:
- “Inakuwaje unatangulia kulala, tena unajifanya unakoroma wakati mume wako anaoga. Wakati mume wako anapanda kitandani ana mahitaji yake kwako, wewe umeshalala, itakuwa ni haki kweli?”
KUNGWI wangu akanitazama kisha akaniuliza.
“Inakuwaje unatangulia kulala, tena unajifanya unakoroma wakati mume wako anaoga. Wakati mume wako anapanda kitandani ana mahitaji yake kwako, wewe umeshalala, itakuwa ni haki kweli?”
“Si haki.”
“Sasa kesho akapata mwanamke wa nje ambaye anamjali na kumuenzi utamlaumu?”
“Hapo ni pa kujilaumu mwenyewe.”
“Ila jambo moja zingatia sana, mpe mume wako kila anavyotaka lakini usikubali kitendo ambacho ni kinyume na maumbile. Akikutamkia hivyo njoo unishitakie kwangu. Nitamuita na nitamuonya akome kabisa!”
“Umenielewa vizuri?’ Kungwi wangu aliniuliza baada ya kunieleza hayo.
“Nimekuelewa.”
“Nadhani kwa leo yametosha. Tumalize chai. Nataka kwenda sokoni.”
Tulipomaliza kunywa chai, niliondoa vyombo. Kungwi wangu akaniambia anakwenda katika chumba chake kingine kubadili nguo ili aende sokoni.
“Mume wangu leo ametamani kula mseto, naenda kununua choroko na nazi,” akaniambia.
“Haya mimi nipo,” nikamjibu.
Yule mwanamke akatoka. Sikujua kama alikuwa na mume. Na kama alikuwa naye, nilijiuliza, mbona haendi kulala naye. Analala na mimi?
Au kwa sababu ya kazi yake ya ukungwi, akipata mwari anahama kwa mumewe? Niliendelea kujiuliza.
Nilishukuru kwamba hakunipa jukumu la kuosha vyombo kwa vile sikutakiwa kutoka uani labda kwa ajili ya kwenda msalani tu. Na hapo pia ni lazima nisindikizwe na yeye au wasaidizi wake.
Nilikaa kwenye kochi nikiwaza. Nikamkumbuka rafiki yangu Amina. Kwa vile kungwi wangu hakuwepo nilitoa simu kutoka katika mkoba wangu nikampigia.
Amina alipokea simu, akaniuliza.
“Shoga, si upo kwa kungwi?”
“Ndio nipo kwa kungwi, nilitaka nikusalimie tu.”
“Kwani unaruhusiwa kuzungumza kwenye simu?’
“Sijui, nimeona kungwi wangu ametoka, ndio nikakupigia.”
“Haya, unaendeleaje huko?’
“Mh! Mwenzangu, huku kuna mafunzo kama niko chuo!”
“Unafundishwa nini sasa na mambo yote unayajua.”
“Sijaona jambo lililo kubwa sana lakini kuna maarifa nayapata.”
“Kama yapi?’
“Ya kumuenzi mume.”
“We Mishi kuna usilolijua!”
“Nitajua kila kitu kwani mimi ni Mfalme Njozi?”
Amina akacheka.
“Haya fundwa na mimi uje unifunde.”
“Basi mwenzako nitakuwa hapa mpaka jumapili, harusi ni jumapli usiku.”
“Nimeambiwa na shangazi yako lakini ameniambia siruhusiwi kuja kukutembelea.”
“Sijui, mimi sijaambiwa kitu ila wewe utakuja hiyo siku ya jumapili wakati napelekwa saluni.”
“Sawa, nitaongea na shangazi.”
“Hatutaongea sana shoga, huyu mwanamke asije akarudi ghafla akanigombesha.”
“Sawa shoga, basi ni hapo jumapili.”
Nikakata simu na kuirudisha kwenye mkoba wangu.
Haukupita muda mrefu kungwi wangu akarudi.
“Mishi leo utakula mseto, waupenda?” Akaniuliza.
“Naupenda na sijaula siku nyingi,” nikamjibu.
“Basi leo utakula mseto, ngoja nikashughulike, wewe endelea kupumzika tu.”
Akatoka tena na kuniacha. Mara kwa mara alikuwa akija mle chumbani na kukaa kidogo kisha huondoka. Mpaka inafikasaa saba mseto ukawa tayari, akaniletea chumbani.
“Utakula peke yako, leo nakwenda kula na mume wangu.” Akaniambia na kutoka.
Nilikaa kwa kungwi yule nikipata mafunzo yake hadi siku ya jumamosi ambapo shangazi yangu na shoga yangu Amina pamoja na dada zangu wawili walifika asubuhi.
Wakajadiliana na kungwi wangu kwa karibu saa mbili. Mazungumzo yalihusu jinsi nitakavyotolewa kesho yake kupelekwa saluni na hatimaye kurudishwa nyumbani kwa ajili ya harusi. Walipanga kila kitu kitakavyokuwa kisha wakaondoka.
Usiku wake wakati nimekaa na kungwi wangu tukizungumza simu yangu iliyokuwa kwenye mkoba wangu ikaita, nikajifanya sikuisikia.
“Simu yako inaita.” Kungwi wangu akaniambia.
Nikaitoa kwenye mkoba wangu na kuona aliyenipigia alikuwa Musa.
Sikukimbilia kuipokea isipokuwa nilimwambia kungwi wangu.
“Ni Musa anayenipigia.”
“Ipokee umsikilize,” akaniambia.
Nilipopewa ruhusa hiyo ndipo nilipoipokea.
“Hallo!” Nikasema kwenye simu.
“Hujambo Mishi?” Sauti ya Musa ikasikika.
“Sijambo. Vipi huko?”
“Huku poa tu, niambie…”
“Nimekumis Musa wangu.”
“Nilikuwa nimekwenda Mwanza. Kwa vile niliona umepelekwa kwa kungwi nilishindwa kukupigia.”
“Umerudi lini?”
“Nimerudi leo. Nilipanga kurudi jana ili nijiandae kwa ajili ya harusi lakini nilishindwa kuja kwa sababu nilichelewa kupata mzigo.”
“Vipi sasa umeshajipanga, si unajua mambo yenyewe ni kesho?”
“Kwa upande wangu nimeshajiandaa. Si unajua mimi sina makubwa. Kama ratiba ni ile ile sawa.”
“Ratiba ni ile ile ya kesho.”
Kwa sababu kungwi wangu alikuwa karibu na alikuwa akinisikiliza sikuzungumza mengi na Musa, tukaagana.
“Moyo wako umetulia kidogo?” Kungwi wangu akaniuliza mara tu nilipoirudisha simu kwenye mkoba.
“kwanini?” Nikamuuliza.
“Si umeongea na mchumba wako ambaye kesho atakuchukua jumla.”
Nikacheka tu, sikumjibu kitu. Baada ya hapo kungwi wangu akaniambia kuwa nijiandae kwenda kuoga ili niweze kusingwa tena.
Muda ulipofika kungwi alinitoa kama kawaida kunipeleka bafuni. Baada ya kuoga akanirudisha tena chumbani na kuketi kwenye mswala. Kulikuwa na mwanamke mmoja ambaye alikuwa msaidizi wake, naye aliingia mle chumbani. Siku ile alinisinga yeye.
Asubuhi yake nilisingwa tena. Wakati narudi kutoka kuoga , safari hii kungwi wangu aliniweka mgongoni mwake huku msaidizi wake akitufuata nyuma.
Tulipofika chumbani nilimuuliza kungwi.
“Mbona leo umenibeba?”
“Nimekuweka mgongoni kwa sababu leo ndio siku yako ya mwisho, unakwenda kuolewa. Hutakiwi kukanyaga chini. Wewe ni mwari!” Akaniambia kwa msisitizo.
“Kumbe ni hivyo?”
“Ndio hivyo mwari wangu. Nataka uchukue haya mafunzo.”
Nikajilazimisha kucheka lakini nilicheka kidogo tu kwani moyo wangu ulikuwa na tashiwishi la ile harusi.
Siku ile pia nilikula kwa kubembelezwa. Nilijisikia kutokuwa na hamu ya kula. Saa saba mchana Amina alifika na wenzake wapatao watano. Wao ndio waliopewa jukumu la kunipeleka saluni. Walikuja kabisa na nguo ya harusi.
Baada ya kuandaliwa na kungwi wangu, saa nane tukatoka. Kungwi wangu pia alikuwemo kwenye msafara. Kulikuwa na teksi mbili zilizokuwa zimekodiwa kwa ajili hiyo.
Ndani ya teksi niliwekwa katika siti ya nyuma. Kulia kwangu alikuwepo Amina na kushotoni kwangu alikaa kungwi wangu. Uso wangu ulizibwa kwa mtandio uliokuwa unaonya.
Kitu ambacho kilinifurahisha, kungwi wangu alikuwa ameshika upepeo uliokuwa umetengenezwa kwa ukili akinipepea usoni kwangu ingawa sikuwa nikisikia joto.
Msafara wetu huo ulikwenda hadi Ilala kwenye saluni ambayo nilizoea kwenda. Nilifurahi Amina alipoelekeza twende katika saluni hiyo kwa kujua kuwa walikuwa marafiki zangu.
Hapo saluni nilishughulikiwa hadi saa kumi na mbili jioni. Nilipambwa nikapambika. Kungwi wangu na Amina pamoja na wale wasichana, walikuwa wakinipigia vigelegele pamoja na kunisifia.
Saa kumi na mbili na nusu nikapakiwa tena kwenye teksi na kurudishwa nyumbani. Nilikuta sherehe zilikuwa zimepamba moto. Kigodoro kilikuwa mbele ya nyumba yetu.
Baada ya kushuka kwenye teksi niliingizwa ndani. Sikupelekwa chumbani kwangu. Kulikuwa na chumba kingine kilichoandaliwa kwa ajili ya harusi ambacho kilikuwa kimepambwa. Nikaingizwa humo.
Shangazi yangu alikuja kuniangalia. Nilipomuona nilimuamkia huku machozi yakinitoka. Sikujua nilikuwa nalia nini wakati kulikuwa na furaha.
Kungwi wangu na Amina ndio waliokuwa karibu yangu wakati wote. Ilipofika zamu ya ndugu na jamaa kuja kunitazama niliinamisha uso wangu kwa aibu. Kipindi hicho cha waalikwa kuja kunitazama kilinikera. Nilikuwa sitaki watu wanione.
Lakini zilikuwa ndio mila za kipwani. Kulikuwa na mama mmoja aliyekuwa akiimba wimbo kwenye kipaza sauti kuwataka waalikwa waje wanione. Sehemu ya wimbo huo ilisema hivi.
“Kina mama njooni, njooni mumuone mwari, kapendeza.”
Wimbo huo uliimbwa kwa karibu robo saa. Baada ya hapo kungwi wangu akaniambia kuwa sheikh ambaye atatufungisha ndoa atakuja kuniuliza kama nimekubali kuolewa na Musa.
Ilipofika saa moja na nusu sheikh huyo akafika.