Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zuchu yasije kuwa ya Wema Sepetu?

Muktasari:

  • Kwa miezi ya karibuni, Zuchu ameonekana akiwa na mwonekano tofauti kidogo na ule ambao mashabiki wake waliuzoea. Mashavu yake yanaonekana kujaa zaidi, mwili umeongezeka kidogo huku mavazi anayovaa yakionekana mapana na yenye kufunika mwili wake kuliko ilivyokuwa awali.

KAMA kuna staa wa kike ambaye kwa sasa anaibua maswali mengi kuliko majibu kwenye mitandao ya kijamii, basi ni Zuchu. Kila anapoweka picha au video mpya, mashabiki hawaonekani tena kujadili muziki wake pekee, bali macho yao yamehamia zaidi kwenye mabadiliko ya mwonekano wake.

Kwa miezi ya karibuni, Zuchu ameonekana akiwa na mwonekano tofauti kidogo na ule ambao mashabiki wake waliuzoea. Mashavu yake yanaonekana kujaa zaidi, mwili umeongezeka kidogo huku mavazi anayovaa yakionekana mapana na yenye kufunika mwili wake kuliko ilivyokuwa awali.

Mabadiliko hayo ndiyo yamezua mjadala mkubwa mitandaoni, huku baadhi ya mashabiki wakianza kujiuliza kama huenda tetesi za ujauzito zinazomhusu zina ukweli wowote nyuma yake au ni mabadiliko ya kawaida yanayoweza kumpata mtu yeyote.


Video na picha zilizoongeza maswali

Si siri kila video au picha mpya ya Zuchu siku hizi hupokelewa kwa macho tofauti. Mashabiki wamekuwa wakichunguza kila hatua yake, kuanzia aina ya mavazi anayochagua kuvaa hadi namna anavyojitokeza mbele ya kamera.

Wapo wanaodai siku hizi Zuchu amekuwa akipendelea mavazi makubwa zaidi, huku wengine wakisema sura yake imebadilika na kuonekana yenye afya zaidi kuliko ilivyokuwa miezi iliyopita.

Ingawa hakuna jambo lisilo la kawaida kwa mtu kubadilika mwonekano kutokana na maisha, lishe au ratiba zake, kwa upande wa mastaa hali huwa tofauti. Kila badiliko huwa habari.


Yasije kuwa ya Wema Sepetu?

Kilichofanya wengi waendelee kuhoji ni historia iliyowahi kutokea kwa msanii wa bongo movie na Miss Tanzania 2006 Wema Sepetu. Kabla hajajifungua, kulikuwa na kipindi ambacho mashabiki walikuwa wakibashiri kuhusu ujauzito wake kutokana na picha na video mbalimbali zilizokuwa zikisambaa.

Wakati huo kulikuwa na wanaoamini na wanaopinga, lakini ukweli ulijulikana baadaye. Ndiyo maana leo hii baadhi ya mashabiki wanapotazama mabadiliko ya Zuchu, hawaachi kujiuliza kama huenda kuna simulizi inayofanana na ile ya Wema.

Tofauti ni kwamba mpaka sasa hakuna kauli rasmi iliyotolewa na Zuchu kuhusu madai hayo.


Khadija Kopa alivyovunja ukimya

Katika mahojiano na Mwanaspoti mama mzazi wa Zuchu, Khadija Kopa amezungumza  kuhusu mjadala unaoendelea juu ya mwanaye.

Kwa mujibu wa maelezo yake, watu wasishangae kuona mabadiliko ya mwonekano wa Zuchu kwa sababu anakua na maisha yanabadilika.

"Zuchu anazidi kukua sasa hivi, hawezi kuwa vilevile kila siku. Kuhusu hizo habari nyingine, muulizeni yeye mwenyewe au mume wake, Diamond Platnumz," anasema.

Kauli hiyo ilionekana kutotoa jibu la moja kwa moja kuhusu uvumi huo, jambo lililoendelea kuongeza hamu ya mashabiki kutaka kujua ukweli.

Ukweli wanaujua wao

Katika ulimwengu wa mastaa, si jambo geni kuona habari kubwa zikibaki siri kwa muda mrefu. Wengine huchagua kulinda maisha yao binafsi hadi pale watakapokuwa tayari kuzungumza.

Kwa sasa, kinachoendelea kuonekana ni mabadiliko ya muonekano wa Zuchu na mjadala mkubwa unaoendelea miongoni mwa mashabiki wake. Je, ni mabadiliko ya kawaida ya maisha au kuna jambo jingine kubwa zaidi?

Jibu kamili wanalijua Zuchu mwenyewe na Diamond Platnumz. Mashabiki wataendelea kubashiri, lakini hadi wahusika watakapozungumza, yote yataendelea kubaki katika kiwango cha tetesi na maswali yasiyo na majibu rasmi.