17: Albamu ya ushuhuda wa uhai kwa Mimi Mars!
Muktasari:
- Mtangazaji huyo wa zamani wa show ya Weekend Gossip kupitia TV1, anakuja na albamu hiyo baada ya kuachia Extended Playlist (EP) mbili, The Road (2018) na Christmas with Mimi Mars (2021).
Leo staa wa Bongo Fleva, Mimi Mars a.k.a Chuga Queen anatarajia kuachia albamu yake mpya, 17 (2026) ambayo ni ya kwanza tangu alivyoingia rasmi katika muziki takribani miaka tisa iliyopita chini ya Mdee Music.
Mtangazaji huyo wa zamani wa show ya Weekend Gossip kupitia TV1, anakuja na albamu hiyo baada ya kuachia Extended Playlist (EP) mbili, The Road (2018) na Christmas with Mimi Mars (2021).
"Miaka miwili iliyopita yote haya yalionekana kama ndoto, kutoka kupigania maisha yangu hadi kurudi studio na kurekodi tena 17 albamu," anazungumza Mimi Mars katika utambulisho (trailer) wa albamu hiyo.
"Si albamu ya kwanza tu, bali ni ushuhuda wa imani Mungu anaweza kuponya, kurejesha, na kukuinua tena. Sifa na shukrani zote ni kwa Mungu. Albamu hii ni kwa ajili yenu mashabiki zangu - Marshearts," ameeleza.
Kauli hiyo ya Mimi Mars imetokana na tukio la kupata ajali ya gari na aliumia sehemu ya kichwa kiasi kwamba alikaa muda mrefu bila kufanya sanaa yake hadi kuacha kuigiza katika tamthilia ya Jua Kali na alitambulika kama Maria.
Hivyo baada ya muda mrefu kupita, ndipo akarejea katika muziki na kuamua ndio muda sahihi wa kuwapa mashabiki wake albamu ambayo walikuwa wakiiulizia kila mara.
"Nawashukuru sana wote tulioshirikiana katika albamu yangu ya kwanza, 17. Kufanya kazi na kila mmoja wenu imenipa uzoefu wa kipekee sana," amesema na kuongeza.
"Kila kipindi cha kurekodi kilikuwa cha aina yake kikiwa na mazungumzo yenye maana yaliyonisaidia katika safari nzima ya kutengeneza albamu hii," ameeleza Mimi Mars.
Kwa jumla ni wasanii watatu pekee walioshirikishwa katika albamu hiyo ambao ni Lady Zamar na Cici, wote kutokea Afrika Kusini, huku msanii chipukizi kutokea kwenye Bongo Fleva, Itare akipata nafasi.
Mimi Mars, mshindi wa tuzo za Entertainment Arts Excellence Awards (EAEA) 2025, ameeleza kwa nini ni watatu hao pekee alioamua kuwashirikisha katika albamu hiyo yenye nyimbo 15.
"Lady Zamar nimejifunza mengi sana kwa vipindi tulivyokuwa pamoja, nina shauku kubwa sana dunia isikie nyimbo tulizotengeneza. Wewe ni mtu mwenye roho nzuri na upendo mwingi, na kwa kweli nimefurahia kila muda tuliotumia kufanya kazi pamoja," ameeleza Mimi Mars.
Katika albamu hiyo Lady Zamar amesikika katika wimbo namba saba unaokwenda kwa jina la With You.
"Cici, Dada yangu pacha - wanasema tunafanana, na kwa kweli naamini hivyo!. Umekuwa kama mwalimu na mshauri wangu katika mradi huu wote. Maneno yako ya kunitia moyo na jinsi unavyojiamini na kujieleza vimenipa nguvu ya kusonga mbele na kukamilisha albamu hii. Nimejifunza mengi kutoka kwako, na ninashukuru sana."
"Itare, Mwanangu, ninatamani dunia isikie wimbo wetu maana naupenda sana!. Pia nimefurahia mazungumzo yetu yote wakati wa kurekodi. Juhudi zako na mtazamo wako chanya vinatia moyo sana, na kila mahali unapoenda unaacha sifa mzuri. Asante tena kwa kila kitu," ameeleza Mimi Mars.
Itare amesikika katika wimbo namba 13 uitwao 'Feel in Love', huku Cici akishiriki katika wimbo namba 3 unaokwenda kwa jina la 'Crazy' ambao ndio wa utangulizi ukiwa umeachiwa takribani miezi miwili iliyopita.
Mimi Mars anakuja na albamu baada ya kupumzika uigizaji wa tamthilia, sehemu aliyofanya vizuri hadi kushinda tuzo mbalimbali zilizotambua mchango wake mkubwa katika tasnia hiyo.
Ikumbukwe Kwa mara ya kwanza Mimi Mars alisikika katika Bongofleva kupitia wimbo wake, Sugar (2017) uliotayarishwa na Dee Classic katika studio ya High Table Sound ambayo inamilikiwa na mwanamuziki Barnaba.
Wimbo huo uliachiwa muda mfupi baada ya kusainiwa katika lebo ya dada yake Vanessa, Mdee Music akiwa ndiye msanii wa kwanza kisha akaja kufuata Brian Simba.
Vanessa alimsaini Mimi Mars ikiwa ni baada ya kupata matokeo mazuri kupitia nyimbo zake zilizotoka mwaka 2015 - 2016, ambazo ni 'Niroge', 'Hawajui', 'Never Ever' na 'Nobody But Me' aliyomshirikisha K.O wa Afrika Kusini.
Sugar ni wimbo mtamu kama jina lake lilivyo na Mimi Mars ameeleza jinsi anavyoufurahia uhusiano wa kimapenzi ambao unampa raha kiasi kwamba anaweza kuufananisha na sukari (sugar).
Video yake yenye rangi nzuri na mvuto mkubwa ilisimamiwa na Director Hanscana, huku ikipambwa na ushiriki wa mastaa wa Bongofleva kama Navy Kenzo, Rosa Ree, Wildad na Quick Rocka.
Kwa jumla mafanikio ya Sugar yaliwashawishi Coke Studio Africa kumpa nafasi ya kutumbuiza kama Msanii Chupukizi (Big Break Artist) 2018 na ikatazamiwa miaka michache mbeleni atakuja kuwa mwanamuziki mkubwa.
Kwa mujibu wa Mimi Mars, tangu akiwa mdogo alipenda muziki na miongoni mwa wasanii waliomvutia ni Usher Raymond IV, mshindi wa Grammy mara nane aliyepata umaarufu mwishoni mwa miaka ya 1990 baada ya kuachia albamu yake ya pili, My Way (1997).