Zari The Boss Lady anavyomponza Wema

Monday June 21 2021
zari pic

WIKI iliyoisha Madam Wema Sepetu alipost kwenye akaunti yake ya Instagram anataka kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wakubwa kwa kuweka matangazo ya biashara zao kwenye ukurasa wake ambao una zaidi ya wafuasi 8.7 milioni.

Kwa mujibu wa tangazo lake, Wema alisema amefikia hatua hiyo kwa sababu watu wengi wamekuwa wakimtumia ujumbe ana roho mbaya kwa kukataa kuweka matangazo yao kwenye ukurasa wake kwa hiyo akaamua kutoa ofa kwa muda wa siku 30 tu huku akiwatoza gharama kidogo.

Post ikiwa haijamaliza hata dakika 30 tayari ilikuwa imekusanya zaidi ya komenti 100 huku nyingi zikiwa zinamshambulia Miss Tanzania huyo wa mwaka 2016, anachokifanya sio kwa sababu anataka kusaidia wafanyabiashara kama alivyodai, bali ni kwa sababu amefulia hivyo anatafuta pesa ya kuendesha maisha kama watu maarufu wengi wanavyofanya mtandaoni.

Maoni ya aina hiyo hayakuishia hapo, yaliendelea baada ya Wema kuanza kupost matangazo ambayo mengi ni ya waganga wa kienyeji wanaonadi wanasaidia kusafisha nyota, utajiri, mvuto, nguvu za kiume, kurudisha mpenzi aliyepotea na kawaida matangazo ambayo kwa mujibu wa watu wengi wanaoandika maoni, hayaendani na Wema, wanadhani jina lake ni kubwa na haliendani kabisa na aina hiyo ya matangazo.

Inawezekana jina la Wema ni kubwa kweli, lakini amini, kinachomponza Wema sio jina tu, bali ni watu anaohusishwa nao, nitakufafanulia.

Likitajwa jina la Wema, watu gani wengine wanaokuja akilini mwako haraka haraka?

Advertisement

Bila shaka litakuja jina la Diamond kwa sababu Wema ndiyo staa wa kwanza kuhusishwa kutoka kimapenzi na Diamond, kiasi wengine wanasema bila Wema kuingia kwenye maisha ya Diamond kipindi kile, huenda Diamond asingekuwa mkubwa kama alivyo leo.

Lakini sasa hivi ukiwalinganisha unawaonaje? Wema anatangaza matangazo ya waganga Instagram wakati Mondi anapiga madili ya matangazo kutoka kampuni kubwa.

Pia ukimuwaza Wema, utajikuta umemfikiria Zari, kwa sababu mganda huyo ndiye aliyekuja kuchukua nafasi ya dada yetu kwa Diamond na hakuchukua kirahisi, bali kwa vita, jasho na damu, vijembe na kurushiana maneno, jambo ambalo linaendelea mpaka leo. Lakini ukiwalinganisha unawaonaje?

Kila mtu anaamini Zari wa Instagram ni Boss Lady, ana biashara kubwa, madili na kampuni kubwa, magari mazuri, maisha safi, wakati Wema wa Instagram, anatangaza matangazo ya Bibi Nanyumbu, mganga wa kusafisha nyota kutoka Newala.

Pia yatakuja majina ya mamiss Tanzania wengine kama Nancy Sumari na Faraja Kotta. Lakini tena ukiwalinganisha na Wema utaona ni kama Wema wa mtangazo ya waganga anapotea.

Alipoulizwa kuhusu ishu hii juzi alijibu: “Nilichoamua kukifanya ni kusaidia watu, kwahiyo kama kuna yeyote amekipokea kinyume na lengo langu ni juu yake.”

Advertisement