Z Anto anarejea kwa kishindo

Tuesday June 08 2021
z anto pic
By Olipa Assa

Mkali wa bongo fleva, Z Anto ambaye aliwahi kutamba na ngoma  ya Binti Kiziwi, amesema ukimya wake wa muda mrefu wa kutoachia kazi,  nyuma ya pazia alikuwa anaandaa vitu vya kumrejesha kwa kishindo.

Ameliambia Mwanaspoti leo Jumatatu ya Juni 7, mwaka 2021 kwamba ukimya wake alikuwa chimbo kuandaa albamu mpya yenye nyimbo sita, anayotarajia kuachia wakati wowote kuanzia sasa.

Amesema tayari ameishafanya video,  kilichobakia wanafanya vikao vya kujadili jina la albamu na kujua wataziachia  kwa mashabiki ili wajue kwa nini alikaa kimya.

"Nilikuwa chimbo kuandaa mawe, zitakuwa kazi nzuri maana nimefanya na wasanii tofauti ambao watakuwa sapraizi siku ambayo nitaachia kazi zangu, ambazo nitaziuza sana online kuliko kwa mfumo wa albamu ambao kibiashara ni ngumu kwasasa, kutokana na sayansi na tekinolojia inavyokuwa kwa kasi;

Ameongeza kuwa"Muziki unahitaji ubunifu na kuyasoma mazingira kwa wakati tuliopo,ndio maana nilipata muda wa kujua nahitaji kuipa ujumbe gani jamii, kisha nikaanza kuyafanyia kazi yale niliyoyaona kwamba yanafaa kwa wakati gani,"amesema.
Mbali na hilo, amegusia changamoto iliopo sokoni kwamba bila kuandika mashairi ya akili ambayo mtu akikaa kusikiliza ataambulia kitu, anaona mapokeo yanakuwa changamoto kwa mashabiki.
"Muziki ni maisha ndio maana kuna wakati ambapo mtu anapenda mdundo ili kupata mzuka wa kucheza, kuna wakati wa kusikiliza ujumbe ili umfunze na kumfariji, hivyo vyote lazima msanii avizingatie na kwa wakati sahihi,"amesema.

Advertisement