Waziri, Esha Buheti wana dunia yao ya mapenzi
KUNA wakati ucheshi wa beki wa Singida Big Stars, Hamad Waziri unamfanya mtu mgeni kwake ajisikie amani kuzungumza naye, mkarimu na nyuma ya pazia ni mpambanaji anayeiwaza kesho yake imara itakayomfanya alie kivulini.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Singida, Waziri alizungumzia mambo mbalimbali kuhusu maisha yake binafsi na soka na anaonekana moyo wake haubebi mitazamo hasi ya watu dhidi yake, anaangalia zaidi namna ya kujenga maisha ayatakayo.
Kabla ya kujiunga na SBS msimu huu, Waziri alikuwa majeruhi kwa muda wa miezi sita baada ya kuumia akiwa na timu yake ya mtaani ya Sinza Stars, hivyo akamkuta Pascal Wawa ambaye ni mshindani wake wa namba akiwa kwenye kiwango cha juu.
"Kwa sasa nipo fiti kabisa, ni suala la kupata nafasi ya kucheza, ndiyo maana sijali kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii watu wanaoona kuoa kwangu ndiko kumemaliza kiwango changu ni suala la muda kuonyesha ubora wangu utakaowafanya waache kuongea," anasema.
Anasema alikuwa anafurahishwa na uchezaji wa Fabio Cannavaro na Pepe ambao walikuwa mabeki wa zamani wa Real Madrid, alijifunza ufundi na mbinu zao.
"Kwa hapa Tanzania nilikuwa nawaangalia zaidi Kelvin Yondani na Juma Nyoso, kaka zangu hao hadi sasa wamebakia na maarifa yao ya kazi, napenda soka ndio maana najifunza kutoka kwa watu mbalimbali, jambo la msingi mchezaji akiwa benchi haimaanishi kipaji chake kimekufa zipo sababu nyingi," anasema.
Mchezaji huyo anayekiri maisha ya SBS ni mazuri, wanapata mahitaji muhimu kwa wakati na uwepo wa mastaa wengi wenye ushindani, unatoa somo kwake kuendelea kukomaa hadi atakapoona kocha anaanza kumtumia.
"Namna tunavyoishi kila mtu na mishe zake, ila tukikutana mazoezini, tunakuwa na umoja kwa ajili ya timu kufanya vizuri maana ndicho kilichotuunganisha," anasema.
MAISHA, FAMILIA
Waziri ni mtoto wa nne kati ya saba kwa upande wa baba na wa pili kati ya watatu kwa upande wa mama. Anasema kwenye ukuaji wake amepitia maisha yaliyomfunza hekima na kutokuogopa kupata ama kukosa.
"Nimeishi sana na baba, kuna kipindi alitengana na mama kabla ya kurudiana na mzee kufariki dunia, yale maisha yalinifanya nione ubora wa malezi yake, alikuwa na maamuzi magumu bila kujali yanamuumiza ili mradi mbele yake kukiwa na jambo la msingi zaidi.
"Kupitia mzee nilijifunza jinsi ya kutunza pesa, kuwekeza, ninachokiamini kukisimamia na kumwabudu Mungu, nikijua duniani tunapita, mama nimeanza kuishi naye baada ya baba kufariki dunia."
NDOA
Staili ya maisha ya beki Wazir na mkewe Esha Buheti wanavyoonyeshana mapenzi, kama huna mwenza unaweza kutamani kuingia kwenye mahusiano ili kufurahia kama wao, hawajali mitazamo ya wengine zaidi ya kulinda amani ya mioyo yao.
Katikati ya mahojiano, Waziri alimpigia simu mkewe ili amkumbushe filamu aliyocheza na marehemu Omary Majuto 'King Majuto' ni baada ya kuuliza kazi ipi ya sanaa ya mkewe aliyokuwa anaifuatilia kabla ya kumuoa.
"Ilikuwa ni zamani sana, aliigiza kama jini na mzee Majuto, ngoja nimpigie simu nimuulize inaitwaje, kisha tuendelee na mahojiano yetu," kisha akanyenyua simu na kuipiga na haikuchukua dakika moja ikapokelewa, jinsi walivyosalimiana na kutaniana utadhani wana ulimwengu wao.
Esha anasikika akisema mume wangu, Wazir naye akajibu shosti yangu; "Nina mwandishi wa Mwanaspoti amenihoji muvi yako niliyowahi kuipenda inaitwaje ile niliyokwambia? akaitaja kwa jina la 'Why this room' na akamalizia kwa kumwambia nina umbea naweza nikakusimulia ama niache umalize kwanza.
Waziri akajibu "Ngoja nimalize mke wangu, nataka nikupe nafasi ya kuongea na mimi hadi ujisikie amani ya moyo, najua utakuwa na mengi, baadaye basi kipenzi cha moyo wangu," kisha mahojiano yakaendelea.
Akaulizwa kwenye mitandao ya kijamii anasemwa ameoa mwanamke aliyemzidi umri. Anajibu "Sijaoa umri, nimeoa mwanamke anayestahili kuitwa mke wa mtu, sijawahi kuoa kwenye maisha yangu yeye ndiye wa kwanza, nimeona wanawake wengi hadi nilipofikia ila jicho na moyo wangu vikampokea yeye."
"Esha alinikuta kwa mshikaji wangu anayechora tatoo, wakati anachorwa tofauti na wanawake wengine ambao hawajiheshimu kwenye maneno yao, alikuwa anaongelea maisha.
"Baada ya kuondoka nikamwambia rafiki yangu kama una namba yake naomba, akanipa nikashinda kama siku mbili nikampigia, nikamueleza nampenda hakuwa mrahisi kama wanavyodhani wengi, baadaye akanikubali, tukaanza mahusiano kama ya miezi tisa kabla ya kumuoa.
"Siku moja kabla ya ndoa nikamwambia nakuoa, hakuamini nikafanya hivyo tunafuraha hadi leo, kwa sasa anakaa na mama yangu mzazi kwa amani, mcheshi, smati, mpambanaji ana heshima, anajua nini maana ya mume, anaheshimu muda wangu wa kazi, tofauti na mitandao ya kijamii inavyotutazama na kuona kiwango changu kinakwenda kupotea."
ANA TATOO 8
Kati ya tatoo nane alizonazo kwenye mwili wake, ipo na aliyoandika jina la mkewe (Esha), huku ya gharama kuliko zote ni ya mchoro wa Simba aliyopunguziwa na rafiki yake kwa Sh600, 000, ila ni zaidi ya bei hiyo.
"Siku aliyoona jina lake kwenye mkono wangu alifurahi sana, ukiachana na hilo tatoo ya Simba inamaanisha ujasiri wa kukabiliana na kila changamoto ya maisha yangu kama alivyokuwa ananifundisha marehemu baba yangu aliyefariki 2019, nikiiona napata nguvu hata kama napitia magumu kiasi gani," anasema.
Anaulizwa hayo yote hayapunguzi umakini wa kuzingatia kazi zako? "Labda nijibu kwa nini sijapata nafasi sana SBS wakati najiunga na timu hiyo nilitoka kuuguza majeraha kwa miezi sita, hivyo sikuwa fiti, najiamini najua nitacheza tu, pia mke wangu ananipa moyo sana wa kupambana."
Beki huyo anaeleza kama isingekuwa soka angefanya biashara; "Nikiwa likizo, tunasaidiana na mke wangu kufanya biashara zake, ili kumuonyesha kwangu ni malkia nawajibika kumpa mapenzi yangu yote ni zaidi ya rafiki, maisha mafupi hayahitaji makasiriko, ukipata muda wa kupenda na kupendwa furahia."
Waziri ambaye aliwahi kucheza nchini Zambia, Kenya klabu ya Son Sugar na KCB anasema hakuna kitu anathamini kama karia yake ambayo kwa asimilia 90 ndiyo inaendesha maisha yake.
"Kuna wakati nacheka tu ninapoona mitandaoni nikizungumziwa ndio mwisho wa kiwango changu baada ya kumuoa Esha, sijui vinahusiana nini na kazi yangu ya soka, nimehaso wengi hawajui, kwa sasa nipo fiti kazi yangu itazungumza zaidi uwanjani," anasema.
Kwa upande wa mkewe kila anapofanya mahojiano mbalimbali haachi kujivunia mumewe na kumshukuru kumstiri kwa kumchagua miongoni mwa wanawake wengi.
"Nampenda mume wangu, wengi wanadhani hawezi kunitunza ila niwaambie ananitunza na tunafanya vitu kwa umoja."