Marioo akili zote zipo gereji

Muktasari:
- Marioo alisema kitu kingine alichokuwa kichwani kwake kitakachowasapoti vijana wengine ni kufungua lebo anayoimiliki ya Bad Nation iliyosajili wasanii wengi walioanza kutoa kazi hewani.
NYOTA wa Bongo Fleva, Marioo amesema anatamani kufungua gereji nyingi ambazo zitakuwa ni sehemu ya ajira kwa vijana ambao wapo mtaani.
Mkali huyo anayetamba na ngoma kama 'Tete', 'Hakuna Matata' na 'Na Na Naa', aliliambia Mwanaspoti katika suala la wanamuziki wakiambiwa kurudisha fadhila kwa jamii kutokana na kufanya vizuri kwenye kazi zao za sanaa, yeye anatamani kufungua gereji kitu ambacho ana uzoefu nacho na kitaweza kuajiri vijana kwa wingi.
"Sababu ya mimi kutaka kufungua gereji nyingi, ni Kwa kuwa nilianza kuwa fundi gereji kisha nikaingia kwenye muziki. Maana isingekuwa muziki ningekuwa fundi gereji tena wa kuchomelea, ndiyo maana nataka kuwa na gereji nyingi ili vijana wengi wapate ajira na najua mazingira yake ya upatikanaji wa kipato," alisema Marioo.
Marioo alisema kitu kingine alichokuwa kichwani kwake kitakachowasapoti vijana wengine ni kufungua lebo anayoimiliki ya Bad Nation iliyosajili wasanii wengi walioanza kutoa kazi hewani.
"Kutokana na kutamani pia kuwainua vijana ambao wanapenda kufanya muziki kama nilivyokuwaga mimi, ndio nikaamua kufungua lebo yangu ya Bad Nation na tayari nishaanza kusajili wasanii ambao wameshaanza kufanya kazi kama Stan niliyeshirikiana kwenye wimbo mpya wa 2025 na wapo madansa ambao wanashiriki sana katika shoo zangu na bado naendelea kusajili wengine tena hapo baadaye."