Prime
Utofauti kati ya Young Killer na Young Lunya

MOTO umewaka kati ya wasanii wa Hip Hop Bongo, Young Killer na Young Lunya baaada ya kupigana spana za kutosha katika ngoma zao mpya za Freestyle zilizotoka hivi karibuni.
Young Lunya ndiye alianza kwa kuachia, Freestyle Sessions 5 ambapo kuna baadhi ya mistari inaonekana wazi inamlenga Young Killer ambaye kwa muda mrefu ilikuwa inadaiwa wana bifu la chini kwa chini.
Baada ya siku mbili Young Killer Msodoki akaamua kujibu mapigo kwa kuachia, Freestyle Sessions 6, hatua hiyo inatoa picha kamili kuwa wasanii hao wameamua rasmi kuinua mapanga katika vita vya ulimwengu wa Rap.
Kwa kawaida hivi ndivyo vitu wanavyopenda mashabiki siku zote hasa upande wa Hip Hop kuona wasanii husika wananyukana vilivyo katika mistari ya ngoma zao, hii ndio burudani kabambe kwao na sasa kila shabiki anavutia upande wake.
Hata hivyo, licha ya kushindanishwa kwa sasa kuna utofauti mkubwa kati ya Young Lunya na Young Killer upande muziki, chapa, mafanikio na mengine mengi kama makala haya yanavyoenda kudadavua;.
Mosi; hadi sasa Young Lunya ameshinda tuzo mbili za muziki Tanzania (TMA) wakati Young Killer ameshinda moja, licha mmoja wapo kumzidi mwenzake kwa idadi ya tuzo, pia aina ya vipengele walivyoshinda vinatoa picha ya nani zaidi.
Young Lunya alishinda TMA 2021 kama Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop na Wimbo Bora wa Hip Hop (Mbuzi), huku Young Killer akishinda TMA 2014 kama Msanii Bora Chupukizi.
Hivyo hadi sasa Lunya ana tuzo mbili zinazohusisha moja kwa moja muziki wa Hip Hop wakati mwenzake hana, ila ikumbukwe tuzo za TMA zilisimama tangu mwaka 2015 hadi ziliporejea mwaka 2021, hivyo Young Killer huwenda angeshinda hapo katikati.
Pili; tayari Young Killer ameachia albamu moja, Super Nyota (2022) ikiwa na nyimbo 15 na imefanya vizuri katika majukwaa ya kidigitali ya kusikiliza muziki kama YouTube, Boomplay Music n.k.
Hata hivyo, Young Lunya hajafanikiwa kuachia albamu ingawa wakati anatangazwa kusainiwa Sony Music Africa hapo Juni 2022 ilielezwa kuwa albamu yake imekamilika na amewashirikisha wasanii kama Diamond Platnumz, Khaligraph Jones na Shomadjozi.
Wakati Young Lunya akitarajia kumshirikisha Diamond katika albamu yake ijayo, kwa upande wake Young Killer alishirikishwa na Diamond katika albamu yake ya tatu, A Boy From Tandale (2018) ambapo alisikika katika wimbo, Pamela.
Tatu; Young Killer baada ya kutoka kimuziki alijiunga na kundi la Mtu Chee akichukua nafasi ya Young Dee aliyejitoa, Young Killer akaungana na Stamina na Country Boy kuendeleza kundi hilo ila halikuwa na maisha marefu.
Hiyo ni tofauti na Young Lunya ambaye alitoka kimuziki chini ya kundi la OMG akiwa na wenzake wawili, Salmin Swaggz na Conboi, pia kundi la OMG la Lunya lilitoa kazi nyingi zilizofanya vizuri kuliko la Mtu Chee la Young Killer.
Ikumbukwe OMG waliachia ngoma kama Fit, Wanangu na Wanao, Staki, Swing, Uongo na Umbea, Paradiso, ila Mtu Chee ambayo alikuwepo Young Killer ilitoa ngoma chache ikiwemo, Mtu Tatu.
Nne; Young Lunya anafanya muziki chini ya RockStar Africa na Sony Music Africa akiwa ndiye msanii pekee wa Hip Hop Bongo kupata dili la kusimamiwa na lebo hiyo kubwa duniani ambayo pia kwa sasa inafanya kazi na Aslay na Abigail Chams.
Utakumbuka Lunya pia alishawahi kusainiwa Switch Music Group (SMG) yake Quick Rocka kama msanii solo na kama kundi (OMG), kwa kifupi Lunya amapata dili nyingi za usimamizi.
Naye Young Killer aliwahi kusainiwa na Wanene Entertainment ingawa alifanya nao kazi kwa muda mfupi, ngoma yake na Khaligraph Jones, Shots (2018) ndio ikuwa ya kwanza kutoka chini ya Wanene. Ni Khaligraph huyu ambaye Lunya anatarajia kumshirikisha katika albamu yake.
Tano; Young Killer alitoka rasmi baada ya kushinda mashindano ya Supa Nyota ila alianza harakati za kutoka akiwa sehemu ya Tamaduni Muzik, alifanya kazi na Maproduza kama Deey Classic na Duke Tachez pamoja na wasanii kama One The Incredible, Songa, Nash MC n.k.
Wakati Young Lunya kabla ya kujiunga na OMG alipoweza kutoka kimuziki, alipambana kutafuta upenyo katika Menejimenti ya Mkubwa na Wanawe yake Fella akiwa na wenzake, Mabantu, hapa hawakupata nafasi hadi walipojiongeza kivyao.
Utakumbuka ngoma kubwa ya kwanza ya Young Killer ni Dear Gamba (2012) akimshirikisha Belle 9, huku ngoma kubwa ya kwanza ya OMG ni Uongo na Umbea (2017) wakimshirikisha Barakah The Prince.
Hata hivyo, Young Lunya anaamini amekaa katika muziki kwa muda mrefu na kufanya kazi zake kwa ubora na ndio sababu ya kujiita "Mbuzi", yaani (G.O.A.T) akimaanisha the Greatest of All Time.
"Mtu anaweza kuwa ameniona sasa hivi lakini nina miaka 11 katika huu muziki na ndani ya hiyo miaka yote nilikuwa nafanya ngoma nzuri na kali toka siku ya kwanza." Young Lunya aliliambia gazeti hili mwaka 2022.
Kama alivyosema Lunya, tukirudia nyuma miaka 11 tunamuona Young Killer akifanya makamuzi katika show kubwa ya Hip Hop yake Fid Q, Fidstyle Friday, Killer alipasuka vilivyo akifanya freestyle kwa zaidi ya dakika 20 na ni show iliyomtangaza na kutabiriwa atakuja kufanya makubwa.