TUONGEE KISHKAJI: Wapinzani Harmonize hamumkomoi yeye na Konde Gang

Tuesday September 14 2021
kishkaji pic
By Kelvin Kagambo

N’JOMBA Nchumari kaenda Marekani kufanya shoo wakaja watu sita tu, hivyo ndivyo wapinzani wa Harmonize wanavyoweza kukusimulia kuhusu shoo aliyopiga majuzi akiwa Marekani.
Shoo ilifanyika jijini Columbus, Ohio na kwa video tulizoziona ni kweli kabisa shoo ilikuwa na watu wachache, ingawa wanaosema ilikuwa na watu sita wanaongeza chumvi.
Lakini wasichoelewa wapinzani wa Harmonize ni kwamba, jamaa ni msanii namba tatu kama sio namba mbili kwa ukubwa hapa Bongo ukiachana na Diamond na Alikiba ni yeye.
Sasa kama msanii wetu mkubwa namna hiyo anakwenda nje kufanya shoo wanakuja watu sita hiyo inatoa picha gani kuhusu muziki wetu?
Yaani ni kama Simba au Yanga ama Azam, timu tatu ku-bwa zaidi Bongo ziende kucheza Klabu Bingwa Afrika halafu ziishie hatua ya makundi hiyo inatoa picha gani kwa soka la Bongo? Na je inakuwa ni aibu ya nani? Timu peke yake au taifa?
Wapinzani wa Harmonize wanachukulia poa. Wanaona ni suala la Konde Boy tu na Konde Gang yake, lakini kiukweli ni suala la kiwanda kizima cha muziki Bongo. Matukio kama hayo yanatakiwa yawashtue. Yanatakiwa yawape taarifa kwamba kwa graundi mambo ni tofauti na tunavyodanganya hapa nyumbani na ‘views’ na ‘trends’ za Youtube.
Mambo ni tofauti kwa sababu watu tunaotamani wawe wapinzani wetu - wasanii wa muziki kutoka Nigeria washavuka hizo hatua kabisa.
Wakati juzi Hamronize anapiga shoo yake, wiki moja nyuma Burna Boy alijaza Uwanja wa O2 Arena jijini London, Uingereza - uwanja unaochukua zaidi ya watu 20,000 na wote hao walilipa viingilio vikubwa. Burna Boy mwenyewe alikuwa anajitapa Instagram akidai “Nimejaza O2 Arena peke yangu, kwa bei ninayoitaka mimi.”
Sio Burna Boy, Wizkid pia atapiga shoo hapohapo O2 Arena Novemba 18, mwaka huu na mpaka hivi tunavyozungumza tiketi zote zimeshauzwa. Na si kuuzwa, ziliuzwa na kuisha ndani ya dakika mbili tu. Na kumbuka hiyo ni shoo inayofanyika nje ya Nigeria - mbali na nyumbani kwao.
Upinzani ni mzuri. Unasaidia kunogesha gemu na kukuza muziki, lakini tukiwa na upinzani usio na macho, kwamba hata kwenye mambo ya kujenga tunaleta utimu unadhani tutafika basi.
Nd’o matokeo yake tutakuwa tunaitana wasanii wakubwa humu ndani halafu tukitoka nje, tukienda kwenye maeneo ya watu tunaonekana chekechekea tu.
Ni kama vile mwanafunzi mbumbumbu anayeshika namba moja kwenye darasa la mambumbu. Ni namba sawa lakini ni mbumbumbu, ila akiwa na mambumbu wenzake yeye nd’o godfather, lakini akitoa mguu nje ya darasa tu ni takataka.
Shoo ya Harmonize iwe funzo. Na kama tutajitia upofu wa kuona kila kitu kipo sawa tutegemee kuona muziki umeganda hapahapa tulipo sasa hivi au ukaporomoka zaidi. Tunaua muziki wetu kwa mikono yetu wenyewe.


Advertisement