TUONGEE KISHKAJI: Vita ya Amapiano imetushinda, tuicheze sasa

KWENYE sanaa kuna falsafa inasema "hakuna msanii anayeweza kutengeneza sanaa mpya." Wakimaanisha kwamba hakuna kitu ambacho hakijawahi kufanyika kwenye sanaa. Yaani usitegemee kuona filamu ambayo haijawahi kutengenezwa, muziki ambao haujawahi kuimbwa, mchoro ambao haujawahi kuchorwa au shairi ambalo halijawahi kuandikwa.

Lakini kama ni hivyo mbona kuna filamu mpya zinaendelea kutoka? Utajiuliza hivyo; lakini wanaoamini falsafa hiyo watakuuliza filamu mpya inayotoka inahusu nini? Ukisema ni kisa cha majambazi kuiba benki watakuambia kuna filamu zaidi ya 100 zimewahi kutengenezwa kuhusu majambazi kuiba benki. Na huo ndiyo ukweli.

Utasema mbona Alikiba, Nandy, Harmonize, Zuchu na Marioo wametoa nyimbo mpya? Anayeamini falsafa hiyo atakuambia nyimbo mpya zinahusu kuachwa au utamu wa mapenzi, kuna nyimbo milioni zinazohusu kuachwa au utamu wa mapenzi. Atakwambia nyimbo hizo zimeimbwa mahadhi ya R&B na Hip Hop, wakati kuna nyimbo zaidi ya Bilioni zilizoimbwa kwa mahadhi hayo  - kwahiyo hakuna kitu kipya.

Swali ni kama hakuna sanaa mpya chini ya jua kwanini wasanii wanaendelea kuzaliwa kila siku, wanaendelea kuibuka kila kukichwa na kila siku wanaanchia kazi mpya?

Anayeamini hakuna sanaa mpya duniani atakwambia hao hawatengenezi kitu kipya, baliu wanafanya kitu ambachi kilishawahi kufanyika lakini katika namna mpya.

Binafasi mimi ni muumini wa falasafa hiyo. Naamini sanaa tulirithi kutoka kwa Mungu. Wasanii wa rangi wanakmwambia hakuna rangi zikiwekwa pamoja hupendeza kama kijani na zambarau.

Sasa nenda kaitazame bilinganya, ina zambarau na kikonyo cha kijani na ni moja ya tunda linapendeza zaidi kutazama kutokana na mpangilio wake wa rangu, Mungu alijua hivyo na sisi tukarithi kutoka kwake.

Naamini hakuna sanaa mpya ndiyo maana siungwi mkono wanauwarushia mawe wasanii wetu wa muziki bongo na tabia yao ya kuiba ladha kutoka mataifa mengine. Kipindi cha kati wakati kwaito inavuma mtaani tuliimbishwa kwaito sana. Nakumbuka mpaka Suma Lee alipotea kwenye gemu lakini kwaito lake la Hakunaga likamrudisha kwenye ramani.

Ikaja midundo ya Kinaija, tukaimbishwa sana wanangu kiasi kwamba tumefikia hatua tumezoea kuona Harmonize wa Tandahimba akiimba ‘Baby A go die for you’ kama Davido na Wizkid hatushangai.

Na hivi sasa wasanii wanatupiwa mawe kwa kudandia aina mpya ya muziki wenye asili ya Afrika Kusini unaoitwa ampiano. Wanaambiwa wanaiga, waache waimbe muziki wa kinyumbani.

Kimsingi kama tunataka muziki wa kinyumbani labda tuimba mangoma ya Saida Karoli na zile za Kila Mwana Ave na Kwao au kwa mbali tucheze mchiriku kwa sababu miziki yote ya kisasa asili yake sio Tanzania, bali wasanii wetu waliiga sehemu kisha wakaiboresha kuwa ya kinyumbani.

Hata taarabu ambayo tunaona ni ya kwetu nayo sio, tuliletewa kutoka Misri na waarabu.

Bongoleva ambayo tunadhani ni ya kwetu pia sio, ni mchanganyiko wa Hip Hop, R & B na Pop inayoimbwa kwa lugha ya kiswahili; na hiyo ni kwa mujibu wa prodyuza nguli wa muziki nchini Majani.

Maana yangu ni kwa sasa bado hatuna muziki wetu wa kututambulisha kama ilivyo Nigeria na Afrika ya Kusini. Yaani tunalo jina lakini Bongofleva lakini muziki wake ni ngumu kuelezea kama unatokea huku Tanzania. Kwahiyo tuache wasanii wetu waendelee kujitafuta kwa kujaribu kufanya muziki mingine, siku wataamka na mziki ambao utakuwa ndiyo sound ya ‘Tanzania’.