Kisa pombe, Gigy Money aomba radhi

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Gigy alisema kuna mambo alikuwa anafanya akiwa amekunywa pombe na baadae hujutia baada ya kuona jamii inamzungumzia tofauti kwa kumuona kituko.
MSANII wa Bongo Fleva na mwigizaji wa Bongo Movie, Gigy Money amesema pombe ndiyo imemharibia kila kitu na kusababisha aonekane kituko kwenye jamii, hivyo anaomba radhi kwa wote waliowakwaza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gigy alisema kuna mambo alikuwa anafanya akiwa amekunywa pombe na baadae hujutia baada ya kuona jamii inamzungumzia tofauti kwa kumuona kituko.
"Kiukweli ulevi umenisababishia hadi sasa najutia, ndiyo maana nimeamua kupunguza kabisa, kuna matukio huko nyuma nilikuwa nayafanya yote sababu ya unywaji wa pombe kupitiliza, nilikuwa kila kukicha nalewa sana na hii imenisababishia hadi kuonekana kituko kwa baadhi ya jamii," alisema Gigy na kuongeza;
“Unajua pombe inaweza kukuharibia kila kitu na ndivyo ilivyotokea kwangu, yaani imenifanya kwa sasa niichukie na natamani kuicha kabisa, tangu nimegundua hivyo kuna vitu kwangu vingi vimebadilika sana na hata baadhi ya watu tumekuwa tunaongea lugha moja kwa sasa."
Gigy alisema kwa hali hiyo anaomba jamii imsamehe tu kwa matukio yote mabaya aliyoyafanya hadharani au yaliyofichuliwa na watu wakiwa kwenye faragha kwani na yeye ni binadamu.
"Mimi naiomba jamii inisamehe tu kwa yale yote mambo mabaya yasiyofaa kwa jamii niliyokuwa nayafanya, kwa sasa jamii isinihukumu kwa mambo ya zamani. Hadi nilipofikia nimevuka hatua kubwa sana, hata mkiangalia kwa kipindi cha muda hakuna mambo mabaya niliyoyafanya, hii ni hatua nzuri."
Kwa upande wa muziki, Gigy Money alisema kwa sasa amekuwa mtu wa kutulia na siyo kutoa nyimbo mara kwa mara kama zamani kwani hapo nyuma amekuwa akigombana sana na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) pindi anapotoa nyimbo zake kwa kuambiwa hazina maadili.
"Sitoi nyimbo kila wakati sababu natumia muda mwingi wa kufikiria mashairi ya kutunga ili nisije kutoa wimbo mpya nikagombana na Basata kwa kuambiwa hauna maadili, kwani nilishafungiwa mara kadhaa kwa kazi zilizowahi kuzitoa siku za nyuma."