TUONGEE KISHKAJI: Rayvanny kupanda Nandy Festival anaonewa au anajionea?

KISHKAJI kabisa nataka nikusimulie stori ambayo hakuna mtu anayefanya kazi Mwanaspoti anaweza kukusimulia. Hili gazeti limebarikiwa kuwa na waandishi wakali wa michezo yaani mamasta. Na kwa sababu hiyo vyombo vingine vya habari vinawatamani ile mbaya. Vinawamezea mate.

Mmoja wa waandishi wakali anaitwa Khatimu Naheka. Zile habari za ndani ndani kabisa za chini ya kapeti zote anazo yeye utadhani ndiye huwa anapanga zitokee. Sasa hivi juzi alitangaza kuacha kazi. Akaandika barua ya notisi ya kuacha kazi na ikakubaliwa na kilichokuwa kimebaki ni yeye kumalizia mwezi wake mmoja wa mwisho kisha atembee.

Lakini kabla mwezi wake haujaisha Naheka akaibukia kwenye chombo kingine cha habari akiwa ameandika habari kubwa. Uongozi wa Mwanaspoti ukashangaa vipi tena? Ni kweli inafahamika unaondoka, lakini muda haujafika sasa mbona umekwenda kufanya kazi na chombo kingine cha habari - tena kinachofanya shughuli sawa na Mwanaspoti? Na mkataba unasema kwa kufanya hivyo, utalizimika uwajibike, utulipe fidia ya makadirio ya faida ambayo tunadhani tungeipata kama hiyo habari uliyokwenda kuiandika kwenye chombo kingine cha habari huku ukiwa na mkataba na sisi ungeiandika hapa.

Mara Naheka na wapambe wake wakaanza kulaumu. Wakawa wanasema eti Mwanaspoti inamuonea Naheka kwamba ilitakiwa imfanyie ubinadamu tu imuache. Ubinadamu kwenye biashara? Ubinadamu kwenye kazi? Ubinadamu kwenye mikataba? Hiyo inawezekana vipi?

Kama ambavyo ubinadamu hauwezekani kwenye tukio la Naheka ndivyo ubinadamu usivyowezekana kwenye tukio la Rayvanny ambaye inadaiwa kuwa wiki iliyoisha alipanda jukwaani kwenye tamasha la Nandy Festival na baada ya hapo akapokea ujumbe kutoka lebo yake ya zamani ya Wasafi kwamba anatakiwa alipe Sh50 milioni kwa sababu alikwenda kufanya shoo ya bure bila taarifa kwa uongozi wake na uongozi unaamini shoo hiyo ingeweza kumuingizia Rayvanny pamoja na kampuni kiasi cha Sh 50 milioni. Kama unajiuliza kwanini anatakiwa kuilipa lebo ambayo ameshatoka ni hivi, Rayvanny ametangaza kujitoa Wasafi tu, lakini mikataba aliyoingia na lebo hiyo inamtaka alipe kiasi fulani cha pesa kwa sababu yeye ndiye aliyechagua kuvunja mkataba. Na kwa sababu Rayvanny hajalipa pesa hiyo bado anahesabika kuwa yuko chini ya Wasafi. Mtan-daoni kumekuwa na pande mbili - wengine wanasema sawa, lakini wapo wanaodai sio sawa kwa Wasafi kumlipisha kwa kosa la kufanya shoo kwenye tamasha la Nandy. Mimi nasema sawa. Najua kuna tetesi za kwamba mkataba ambao Wasafi walimpa Rayvanny ni wa ajabu kidogo, lakini hiyo haibadilishi ukweli kwamba kama ulishamwaga wino na baadaye ukaja kugundua kuwa mkataba uliomwaga wino hausadifu ukitakacho kuna taratibu za kufuata kushughulikia suala hilo. Huwezi kutoka kienyeji. Na ambao wanasema sio sawa huko mitandaoni wengine ni wasanii ambao kila siku wanalalamika kwamba sanaa inatakiwa kuchukuliwa kwa umakini kwani ni kazi kama kazi zingine. Sasa itachukuliwaje maanani kama watu hawataki kuheshimu mikataba? Rayvanny anatakiwa awajibike kwa alichofanya huku akitafuta msaada wa kisheria wa namna ya kushughulikia suala la mkataba aliosainishwa na Wasafi, ikiwa anadhanihaumfuai. Na kuhusu Naheka nilisema nataka nikusimulie stori ambayo hakuna yeyote anayefanya kazi hapa Mwanaspoti anaweza kukusimulia kwa sababu hiyo stori haipo. Siyo kweli.