TUONGEE KISHKAJI: Muda wa kuwa msanii nusu nusu umepita

NIKIKUPA orodha ya wasanii wa muziki ninaowasikiliza sana Mbosso atakuwa ni mmoja wao. Sikumbuki kama kuna siku nimewahi kusikiliza nyimbo tano halafu ikakosekana ngoma ya Mbosso.

Na sio peke yangu, namba za jamaa kwenye majukwaa ya kuuza na kusikiliza muziki zinaonyesha kuwa tupo wengi tu ambao tunabanjuka sana na ngoma za mwana.

Na kwa sababu hiyo niamini mimi nikikwambia, wimbo wa mwisho alioutoa Mbosso, Amepotea, ni wimbo mzuri sana, pia niamini mimi nikikwambia unafanana na nyimbo zake kibao alizozitoa miaka ya nyuma. Naomba nisikaririwe vibaya, nyimbo zake kufanana sio tatizo kubwa sana.

Lakini ngoma hiyo hiyo tunayosema inafanana na ngoma zingine zilizopita inatoa hisia za upya ukiitazama kwenye TV. Wimbo wa Amepotea una kavideo fulani hivi ambako ukikatazama unaacha kabisa kusikiliza kinachoimbwa, wewe unakomaa kuzingatia kinachoonekana. Video inachekesha, ina stori nzuri, ina endenana na kinachoombwa.

Na hapo ndipo ninapopata nguvu ya kusema, enzi za kuwa msanii nusu nusu zimeisha. Yaani enzi za kuwa mwanamuziki ambaye unachoweza kufanya ni kuimba vizuri pekee zimeshapitwa na wakati. Mashabiki huko nje wanataka msanii mwenye ngoma kali na video kali za ngoma zake.

Ndiyo maana kuna baadhi ya wasanii, mfano Jay Melody, ngoma zake zinafanya vizuri sana kwenye majukwaa ya kuuza na kusikiliza muziki, kwenye maredio na mitaani, lakini linapokuja suala la video, maoni ambayo yanakuja kwa kujirudia kuhusu Jay Melody ni kwamba video zake ni mbaya.

Nyimbo inatrend, watu wanategemea kupata video kali, lakini mwisho wa siku wanapata video haieleweki wala haiendani na kinachoimbwa. Wanamuona dogo anazingua, wanamuona dogo ni msanii nusu nusu.

Ndiyo maana siku hizi kuna wazo la wimbo linaanzia kwenye video. Yaani msanii anakuwa na wazo la video yake itaonekana vipi, kisha kutokea wazo hilo ndiyo sasa anaanza kutengeneza ngoma itakayoendana na wazo hilo. Ndiyo maana leo hii kuna ngoma hatuzikumbuki kutokana na nini kilichoimbwa bali tunazikumbuka kwa video.

Ndio maana kuna wasanii wanatoa video zaidi ya moja kwa wimbo mmoja kwa sababu pengine mwanzo walitoa video ikabuma. Jiulize kwanini video ibume wakati wimbo mzuri? Au jiulize kuna haja gani ya kutoa video nyingine? Kama wimbo ni mzuri watu si wataupenda tu. Lakini haiko hivyo. Enzi hizi watu hawataki vitu nusu nusu, kama unatengeneza ngoma nzuri, kama unaimba vizuri, hakikisha pia video zako zinatubamba.

Jiulize kwanini kina Domokaya na Mandojo wanatoa video ya ngoma zao za zamani ambazo hawakuwahi kuzifanyia video? Kama shida yao ni kupata mashabiki wa kizazi kipya kwanini wasiziachie tu ngoma zao bila video? Kwa sababu wanajua enzi hizi, watu hawataki vitu nusu nusu, wanataka ngoma kali na video kali.