TUONGEE KISHKAJI: Movie ya Bob Junior inakuja, tujiandae

NAOMBA tutafutane baada ya miaka 10 kuanzia sasa twende tukatazame filamu kuhusu tukio la kifo cha Simba, Bob Junior iliyotengenezwa na watu ambao sio Watanzania. Nakwambia hivyo kwa sababu nafahamu jinsi Waafrika hususan Watanzania tulivyo na hadithi nyingi za kusimulia kupitia filamu zetu, muziki wetu, riwaya zetu lakini hatuna muda nazo, hatuzizingatii, tunaacha watu wa nje waje kusimulia hadithi zetu.

Na unajua ni nini matokeo ya hadithi yako kusimuliwa na mtu mwingine? Ni kwamba ataisimulia kwa namna ambayo inamnufaisha na kumpendeza yeye. Ni kama vile unavyoona kwenye mitandao Wakenya ‘wanaposemaga’ Diamond ni msanii wa Kenya; sasa kama sisi hatumtangazi na kujivunia na kusimulia hadithi zake, kwanini wengine wasifanye hivyo? Wasimtangaze na kumsimulia kwa namna inayowanufaisha na kuwapendeza wao?

Waafrika tuna hadithi nyingi sana za kusimulia, Tanzania tu peke yake tunahadithi nyingi za kusimulia kwenye Vita vya Majimaji, kwenye maisha ya Chifu Mkwawa, maisha ya Mwl Nyerere, maisha ya Sheikh Karume, maisha ya Bilionea Bakhresa, Maisha ya Mr. Nice. Yaani tuna hadithi nyingi kuliko unavyoweza kudhani, lakini mpaka leo hatuna filamu zinazosimulia hadithi hizo vizuri kutokea upande wetu.

Na hili wala sio kosa la wasanii kwa asilimia mia moja, zaidi ni kosa la serikali zetu za Afrika. Kimsingi, kwenye mataifa kama Tanzania ambayo soko la sanaa kama filamu bado halijawa na miguu ya kusimama lenyewe, usitegemee Mtanzania akaja kuwekeza kwenye filamu ya Kinjekitile ilihali hajui wapi atakwenda kuiuza filamu hiyo.

Kwahiyo mara nyingi kinachofanyika ni serikali kuwa na mifuko inayowawezesha wasanii kupata mitaji ya kufanya kazi kubwa za aina hiyo, huku lengo kuu likiwa sio kuuza na kupata faida, bali ni kusaidia watu kujifunza kuhusu mashujaa wao kupitia filamu hizo.

Ni kama tulivyofanya kwenye Royal Tour, serikali ilitoa mabilioni ya pesa, lakini haikuwa filamu kwa ajili ya kuuza na kupata pesa. Ilikuwa ni filamu ambayo ingetangaza vivutio vya utaliii tulivyo navyo Tanzania, kisha ingerudisha pesa kupitia watalii ambao wangekuja Tanzania kutalii baada ya kuitazama Royal Tour.

Na niliposema sio wasanii hawahusiki kwa asilimia 100 nilikuwa namaanisha wanahusika kwa kiasi fulani. Wasanii wa Tanzania na wenyewe ni wavivu sana, hawataki kabisa kujaribu kutuma ma-proposal serikalini na kwenye mashirika ambayo yanaweza kuwasaidia mitaji ya kutengeneza kazi kubwa kubwa.

Ni wasanii wachache wenye ujanja kwenye upande huo na ndiyo hao hao unaowaona kila siku wanajirudia kwenye kupata mitaji kutoka mashirika na serikali; kwa kuwataja wachache, kina Seko Shamte, Amili Shivji.

Ndiyo maana kuna siku, kwenye ukurasa huu huu, niliwahi kuwaomba, hawa wasanii wanaojua kutafuta mitaji kwenye mashirika, wawafundishe na wenzao, pengine inaweza kusaidia tasnia kwa ujumla.