Safari ya Mbosso ipo tofauti kabisa
Muktasari:
- Mbosso, mwanzilishi wa Khan Music, ni wazi katika kipindi kifupi kijacho ataufaulu ule mtihani uliowashinda wasanii wengi walioachana na lebo hiyo kama yeye.
Dar es Salaam. Kama ulidhani ni wahenga pekee yao ndio hawaamini anachofanya Mbosso katika muziki wakati huu, basi utakuwa umekosea kwani hilo limewagusa hadi WCB Wasafi, lebo yake ya zamani.
Mbosso, mwanzilishi wa Khan Music, ni wazi katika kipindi kifupi kijacho ataufaulu ule mtihani uliowashinda wasanii wengi walioachana na lebo hiyo kama yeye.
Ni kupitia wimbo wake, Pawa (2025) ambao umejizolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi kiasi cha kumfanya mwanamuziki huyo kupita huko na kule akifanya show mfululizo.
Kutoka katika Extended Playlist (EP) yake ya pili, Room Number 3 (2025), 'Pawa' ni wimbo wa mapenzi wenye kusisimua unaoelezea nguvu kubwa ya hisia za upendo wa dhati. Kwa sauti laini, Mbosso anaufananisha upendo na nguvu ya kulevya inayomwacha dhaifu na mwenye msisimko wa kihisia.
Maneno ya wimbo huo yamechanganya udhaifu wa kihisia na heshima ya dhati huku Mbosso akimchora mpenzi wake katika picha kubwa na safi kama chanzo cha nguvu na msukumo wa kweli wa maisha.
Kwa jumla wake, kutokana na mchanganyiko wa midundo ya Bongo Flava na ala za muziki wa hisia, wimbo huo (Pawa) umeonyesha uwezo wa Mbosso katika uandishi wa mashairi na uimbaji wenye hisia kali za mapenzi.
Mapokezi ya 'Pawa' hayaonekani mtaani tu, bali hata katika majukwaa ya kidijitali ya kusikiliza muziki, napo umefanya vizuri ukishika namba moja katika chati nyingi kiasi kwamba Mbosso amekuwa akiutaja kama wimbo namba moja nchini kwa mwaka huu.
Huu ndiyo wimbo kutokea Tanzania ambao umesikilizwa zaidi katika mtandao wa Spotify kwa mwaka 2025, huku ukifuatiwa na Me Too (Abigail Chams & Harmonize), Furaha (Harmonize) na Nairobi (Marioo & Bien).
Ikumbukwe hadi mwaka 2024, jukwaa la Spotify lilikuwa na watumiaji milioni 615 wa kila mwezi, huku watumiaji wa kulipia (premium subscribers) wakiwa takribani milioni 239. Hii inaifanya Spotify kuwa huduma kubwa zaidi ya muziki duniani kwa watumiaji wa kila mwezi.
Huko YouTube, 'Pawa' imekimbiza zaidi ukiwa ndiyo wimbo namba moja nchini uliofanya vizuri zaidi katika mtandao huo kwa mwaka huu, kwa kifupi hakuna video ya muziki iliyotoka mwaka huu iliyotazamwa kuizidi ya huo.
Ndani ya miezi mitano tu tangu kuachiwa kwake, video ya 'Pawa' imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 50, ikiwa ni wastani wa kutazamwa mara milioni 10 kila mwezi. Hivyo pia imeweka rekodi kama video pekee iliyofikisha namba hizo katika kipindi kifupi.
Hata hivyo, ikumbukwe hadi sasa wimbo wa Bongo Fleva wenye rekodi nzuri ya kutazamwa YouTube katika muda mfupi zaidi, ni wake Diamond Platnumz, Waah! (2020) akimshirikisha Koffi Olomide kutokea DR Congo.
Huu video yake ilitazamwa mara milioni 1 ndani ya saa nane, mara milioni 4 kwa saa 48, mara milioni 10 kwa siku saba, mara milioni 20 kwa wiki tatu, mara milioni 30 kwa mwezi mmoja, mara milioni 40 kwa miezi miwili na mara milioni 50 miezi mitatu!.
Sasa kwa matokeo hayo, 'Pawa' inapanda hadi nafasi ya tatu katika orodha ya video za Mbosso zilizofanya vizuri zaidi YouTube kwa muda wote na video ya wimbo wake, Baikoko (2021) akimshirikisha Diamond ndiyo inashika namba moja ikiwa imetazamwa mara milioni 69.
Ikiwa video ya 'Pawa' ina wastani wa kutazamwa mara milioni 10 kila mwezi, ni matarajio miezi mitatu ijayo ndiyo itakuwa video yake namba moja YouTube. Na hapa ndipo wahenga na WCB Wasafi hawaamini hilo linaenda kutokea.
Mara nyingi wasanii wanaoondoka WCB Wasafi wamekuwa wakikosolewa wanashindwa kutengeneza nyimbo zinazopata namba kubwa kuzidi zile walizotoa chini ya lebo hiyo. Na hilo limeonekama kwa Rich Mavoko, Harmonize, Rayvanny na Lava Lava.
Hata hivyo, Mbosso kwa mwendo huu wa 'Pawa', wimbo uliotayarishwa na S2kizzy huku video ikiongozwa na Director Folex, anaenda kuonyesha hilo linawezekana tena ndani ya muda mfupi tu.
Ikumbukwe Room Number 3 EP (2025) ilitoka rasmi Juni 13, ikiwa ni takribani miezi mitano tangu Mbosso kuachana na WCB Wasafi. Na huu ndiyo mradi wa kwanza chini ya Khan Music, lebo aliyoianzisha kwa ajili ya muziki wake.
Ndani ya mwezi mmoja, EP hiyo ilikuwa imesikilizwa zaidi ya mara milioni 50 katika majukwaa yote muziki (digital streaming) ikiwa ni ya kwanza kwa Mbosso kufikia namba hizo ndani ya muda huo.
Hata hivyo, wimbo 'Pawa' kwa wakati huo ulikuwa umechangia karibia nusu ya namba hizo ukiwa umesikilizwa zaidi ya mara milioni 20, hivyo ndiyo wimbo uliopata mapokezi mazuri zaidi (most streamed) katika EP hiyo ambayo kwa sehemu kubwa imeandaliwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic.