Sababu ya kifo cha mwigizaji Kitundu, baba mdogo aeleza

Muktasari:
- Akizungumza na Mwananchi leo Juni 26, 2025, Matei amesema Kitundu alianza kusumbuliwa na maradhi hayo miaka miwili iliyopita lakini familia ilimuuguza hadi akarudi katika hali yake ya kawaida.
Matei Anamboka ambaye ni baba mdogo wa aliyekuwa mwigizaji wa filamu nchini, Radainus Vitalis 'Kitundu', amesema kilichoondoa uhai wa kijana wao ni maradhi ya kifua na tumbo.
Akizungumza na Mwananchi leo Juni 26, 2025, Matei amesema Kitundu alianza kusumbuliwa na maradhi hayo miaka miwili iliyopita lakini familia ilimuuguza hadi akarudi katika hali yake ya kawaida.
"Marehemu alikuwa anasumbuliwa sana na kifua pamoja na tumbo. Hiyo hali ilianza kutokea mwaka au miaka miwili nyuma. Tukamuuguza ambavyo tunaweza na tunamshukuru Mungu kwa muda ule baada ya kumuuguza kwa miezi sita akawa yupo vizuri, akarudi katika shughuli zake," amesema Matei.
Amesema kabla ya umauti wake, hali yake ilibadilika tena wiki mbili zilizopita mpaka kupelekea kifo.
"Tukapata taarifa anaumwa kama wiki mbili kabla ya kifo chake, sisi kama familia imetushitua hatukutegemea. Kingine marehemu hakuwa mtu wa kukaa hapa nyumbani, alikuwa anaishi huko anapofanyia shughuli zake mara nyingi tulikuwa tunawasiliana naye tu.
"Lakini baadaye tulifanya udadisi tukaambiwa alikuwa anaugua kama wiki tatu alikuwa anajiuguza mwenyewe, hali ilivyomzidia akarudi kwa familia ndiyo hivyo ndani ya wiki moja baada ya kulazwa umauti ukamkuta," amesema Matei.