Rose Ndauka kuachia wimbo wa pili

Monday May 03 2021
ndaukaa pic
By Nasra Abdallah

Licha ya watu kumponda kwamba hajui kuimba, msanii Rose Ndauka anatarajia kuachia wimbo wa pili.

Rose ambaye amejipatia umaarufu kupitia sanaa ya uigizaji, Aprili 8, 2021 aliwashtua watu baada ya kutangaza kuingia kwenye sanaa ya muziki ambapo siku hiyo pia aliachia wimbo wake unakwenda kwa jina la ‘Sijali’

Hata hivyo leo Mei 3, 2021 ameonekana kuweka pamba masikioni kwa wanaomwambia hajui kuimba na kueleza kuwa anataka kuachia wimbo wake wa pili.

Kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, ameandika” Uwiiiii nataka kutoa goma jengine, kama upo tayari sema woyoooooooo, Sijali ikifika laki mbili naachia mzigo mwingine”.

Hata hivyo wimbo huo ukiwa una siku tatu tangu ulipotoka, hadi kufika leo saa saba mchana ulikuwa umeshatazamwa mara 54,302.

Mara baada ya kuachia wimbo wake huo wa Sijali ambao upo katika mahadhi ya Hiphop, baadhi ya watu walionekana kumponda na kueleza kuwa hajui kuimba, huku wakimshauri kuwa ni bora angebakia kwenye uigizaji huku moja ya watu waliotoa maoni hayo akiwa ni msanii mwenzake Shamsa Ford.

Advertisement

Wengine walienda mbali zaidi na kusema kuwa bora hata angeimba muziki laini kuliko huo wa Hiphop ambao wasanii wengi wa muziki wanachemka nao hadi kubadili staili yao ya kuimba.

Mwanaspoti ilipomtafuta kujua namna gani anayachukulia maoni hayo, Rose amesema kamwe hayamrudishi nyuma katika kupigania muziki wake na badala yake atakuwa anafanyia kazi maoni ambayo ni chanya  na yenye lengo la kumjenga na sio ya kumkatisha tamaa.

“Hata kwenye kusoma maoni ya watu huko mtandaoni, huwa maoni kama hayo nayapita kama siyajui, lakini wale wanaoniambia hapa ungefanya hivi, hii ungekaa hivi, huwa nayazingatia sana,”amesema msanii huyo.

Advertisement