RIYAMA ALLY Miaka 10 ya ndoa na Mysterio... hatuachani ng’o!
Muktasari:
- Dakika 5 Na... lilizipata tetesi hizo na fasta kumvutia waya (kumpigia simu) Riyama ili kuthibitisha au kupinga madai hayo ya kuachana na mumewe.
NI takriban miaka 10 sasa tangu msanii wa Bongo Movie, Riyama Ally afunge ndoa na Leo Mysterio. Hata hivyo, kumekuwa na tetesi zinazosambaa wawili hao wameachana na kuzua mjadala mkubwa.
Dakika 5 Na... lilizipata tetesi hizo na fasta kumvutia waya (kumpigia simu) Riyama ili kuthibitisha au kupinga madai hayo ya kuachana na mumewe.
Riyama ameamua kuvunja ukimya juu ya madai hayo na kudai jambo hilo halimshangazi kwani tangu walipofunga ndoa Juni 16, 2026 imekuwa ikifuatiliwa na wengi na kuibuka kwa tetesi kama hizo mara kwa mara.
Pia amezungumzia safari ya miaka 10 ya ndoa yao, changamoto walizopitia na matumaini yake ya kupata mtoto siku moja na mume wake huyo, ikiwa ana mtoto mmoja aliyewahi kuzaa na mwanamume mmoja kabla hajaolewa.
MWANASPOTI: Kumekuwa na taarifa zinazosambaa mitandaoni umeachana na mume wako Leo Mysterio. Ukweli ni upi?
RIYAMA: Huo ni uzushi wa kawaida ambao nimeuzoea. Mimi na mume wangu tupo pamoja, tunaendelea vizuri na maisha yetu. Watu wamekuwa wakiifuatilia ndoa yetu tangu siku ya kwanza tuliyofunga ndoa, hivyo sikushangazwa kuona tena habari za kututenganisha. Ukweli ni hatujaachana na tunaendelea kujenga familia yetu kwa amani.
MWANASPOTI: Unaona sababu gani zinazofanya ndoa yenu iwe gumzo mara kwa mara?
RIYAMA: Nadhani ni kwa sababu tangu mwanzo watu walikuwa na maoni yao kuhusu sisi. Wapo waliokuwa wakisema nimeolewa na mwanamume mdogo kuliko mimi, wengine wakasema ndoa haitadumu. Lakini leo hii tunatimiza miaka 10 tangu tufunge ndoa na bado tupo pamoja. Hivyo naamini watu wengi walikuwa wakisubiri kuona kile walichokitabiri kinatokea.
MWANASPOTI: Juni 16 mwaka huu mnatimiza miaka 10 ya ndoa. Unajisikiaje kufikia hatua hiyo?
RIYAMA: Ni jambo kubwa sana. Siyo rahisi kwa wanandoa wowote kufikisha miaka 10 ya ndoa. Tumepitia mengi, mazuri na magumu, lakini bado tumeshikamana. Ninamshukuru Mungu kwa kutuwe zesha kufika hapa tulipo. Miaka 10 ni ushahidi upendo wetu haukujengwa kwa maneno ya watu bali kwa uamuzi wetu wenyewe.
MWANASPOTI: Wakati mnafunga ndoa mwaka 2016 kulikuwa na maneno mengi kuhusu tofauti ya umri kati yenu. Yaliwaathiri?
RIYAMA: Mwanzoni yalikuwa mengi sana. Kila mtu alikuwa na lake la kusema. Lakini tulijifunza mapema, ukisikiliza sana maneno ya watu huwezi kuishi maisha yako. Leo Mysterio ni mume wangu na nimekuwa nikimheshimu kama mume wangu. Naye amenihesh imu ka ma mke wake. Hicho ndicho kilichotusaidia kuvuka changamoto zote.
MWANASPOTI: Katika miaka hiyo 10 bado hamjapata mtoto wa pamoja. Hilo linakupa presha?
RIYAMA: Hapana. Mimi naamini kila kitu kina wakati wake. Mtoto ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kama Mungu ameandika tutapata mtoto, tutampata. Mimi bado nina matumaini makubwa sana. Sijakata tamaa hata kidogo. Japokuwa mimi nina mtoto wa kike ambaye nilizaa kabla sijaingia kwenye ndoa na Mysterio.
MWANASPOTI: Umewahi kufikiria kuachana na ndoto ya kupata mtoto na mume wako?
RIYAMA: Hapana. Bado naamini ipo siku nitakuwa mama. Pia nimejifunza kutokuweka presha kubwa kwenye jambo ambalo liko mikononi mwa Mungu. Maisha hayaendi kwa ratiba ya mwanadamu kila wakati.
MWANASPOTI: Kuna wakati uliwahi kusema hata msipopata mtoto mnaweza kulea watoto wanaohitaji malezi. Pamoja na mtoto wako au kama na yeye ana watoto awalete. Bado msimamo huo upo?
RIYAMA: Ndiyo. Mtoto ni mtoto tu. Kama Mungu atatupa mtoto wetu tutashukuru. Kama itakuwa tofauti, bado tuna nafasi ya kugusa maisha ya watoto wengine wanaohitaji upendo. Kikubwa ni kuwa na moyo wa kutoa upendo.
MWANASPOTI: Leo Mysterio amekuwa akizungumza vizuri sana kuhusu wewe tangu mwanzo wa uhusiano wenu. Hilo lina maana gani kwako?
RIYAMA: Linanifanya nijisikie mwenye bahati. Mume wangu amekuwa mtu anayeniheshimu hadharani na faraghani. Hata kabla ya ndoa alikuwa akisema amepata mwanamke anayemfaa. Hivyo ni jambo la kumshukuru Mungu kuona bado tunadumisha heshima hiyo.
MWANASPOTI: Siri ya kudumu kwa ndoa yenu ni ipi?
RIYAMA: Kusikilizana. Watu wengi wanadhani ndoa ni furaha tu, lakini kuna nyakati za changamoto. Kikubwa ni kuheshimiana, kuvumiliana na kuzungumza ukweli. Mimi na mume wangu tunajitahidi kufanya hivyo kila siku.
MWANASPOTI: Kumekuwa na vipindi ambavyo watu waliwahi kuandika mmetengana hata miaka ya nyuma. Unakumbuka hilo?
RIYAMA: Nakumbuka sana. Hata muda mfupi baada ya ndoa kulikuwa na taarifa kama hizo. Lakini zilipita kama zilivyokuja. Ndiyo maana hata hizi za sasa sizipi uzito mkubwa. Watu wamekuwa wakitabiri mwisho wa ndoa yetu kwa miaka mingi, lakini bado tupo pamoja.
MWANASPOTI: Leo ukitazama nyuma, unajivunia nini zaidi kwenye ndoa yako?
RIYAMA: Najivunia hatukuruhusu kelele za watu zitutawale. Tumekuwa tukijenga maisha yetu kwa misingi yetu wenyewe. Miaka 10 sio mchezo. Ni safari ndefu yenye mafunzo mengi. Ninamshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa na ninaamini bado ana mipango mizuri zaidi mbele yetu.
MWANASPOTI: Ujumbe wako kwa wanaofuatilia ndoa yenu?
RIYAMA: Waendelee kutuombea mema. Mimi na mume wangu hatujaachana. Tunaendelea na maisha yetu, tunaendelea kupendana.