Rayvanny sasa mambo yapo hivi

Rayvanny sasa mambo yapo hivi

STAA wa Bongofleva, Rayvanny amesema kwa sasa yeye ni msanii anayejitegemea, hivyo yeyote anayetaka kufanya naye kazi awasiliane na menejimenti yake mpya.
Kauli ya Rayvanny inakuja wiki chache tangu atangaze kuachana na lebo ya WCB Wasafi aliyodumu nayo miaka zaidi ya mitano.
“Kazi yangu ni muziki, nitafanya kazi na msanii yeyote na kufanya matamasha sehemu yoyote kikubwa ni mawasiliano na wasimamizi wangu ambao watakuwa na majibu sahihi ni muda gani napatikana na niko wapi kwa wakati huo wananitafuta,” alisema na kuongeza;
“Muziki ni biashara msanii anatakiwa kujitengeneza mwenyewe kabla ya kusubiri wasimamizi wake wasimamie kila kitu kumuhusu, natamani kuona nafanya mambo makubwa zaidi nikiwa chini ya lebo yangu ili kuwavuta wasanii wengi zaidi kuja kufanya kazi na mimi.”
Rayvanny kwa sasa anafanya muziki wake chini ya lebo yake, Next Level Music (NLM) aliyoizindua mwaka jana, na sasa Rayvanny anafanya vizuri na wimbo wake mpya, Pelepele.